Sura ya Fuss’ilat, aya ya 8-12 (Darsa ya 875)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 875 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 41 ya Fuss’ilat. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya ya nane ya sura hiyo ambayo inasema:
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ أَجْرٌ غَيْرُ مَمْنُونٍ
Hakika wanao amini na wakatenda mema watakuwa na ujira usio na ukomo.
Aya ya mwisho tuliyosoma katika darsa iliyopita iliwazungumzia washirikina ambao hawatoi Zaka wala kufanya mambo ya kheri na hawaamini kuwepo kwa ulimwengu wa akhera. Bila shaka watu hao hata kama watafanya jambo la kheri pia, lakini kwa sababu hawaiamini Siku ya Kiyama, hawatopata thawabu na malipo huko akhera. Mkabala na watu hao, aya tuliyosoma inasema: Lakini watu wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama na wanajitahidi kila wakati kufanya mambo mema na ya kheri kulingana na fursa na uwezo binafsi walionao na nafasi yao kijamii, Allah SWT atawalipa Siku ya Kiyama malipo ya thawabu zisizo na ukomo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, imani na amali njema ni vitu viwili visivyotenganika; na kimoja bila kuchanganyika na kingine hakiwezi kumfaa mtu Siku ya Kiyama. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, malipo ya thawabu ya Allah huko akhera hayatokuwa na ukomo wa kumalizika, kinyume na hapa duniani, ambapo malipo, hata yenye thamani ya kiwango cha juu kabisa, yana ukomo wa matumizi na yanamalizika.
Zifuatazo sasa ni aya za 9 na 10 ambazo zinasema:
قُلْ أَئِنَّكُمْ لَتَكْفُرُونَ بِالَّذِي خَلَقَ الْأَرْضَ فِي يَوْمَيْنِ وَتَجْعَلُونَ لَهُ أَندَادًا ۚ ذَٰلِكَ رَبُّ الْعَالَمِينَ
Sema: Hivyo nyinyi mnamkataa aliye umba ardhi katika siku mbili, na mnamfanyia washirika? Huyu ndiye Mola Mlezi wa walimwengu wote.
وَجَعَلَ فِيهَا رَوَاسِيَ مِن فَوْقِهَا وَبَارَكَ فِيهَا وَقَدَّرَ فِيهَا أَقْوَاتَهَا فِي أَرْبَعَةِ أَيَّامٍ سَوَاءً لِّلسَّائِلِينَ
Na akaweka humo milima juu yake, na akabarikia humo na akakadiria humo chakula chake katika siku nne. Haya ni sawa kabisa kwa wanao uliza.
Ukweli ni kwamba ardhi hii tunayoishi juu yake imeumbwa na Allah SWT Mola pekee wa haki; na hakuna kitu wala mtu yeyote yule ambaye ni mshirika wake katika uumbaji huo. Yeye si Muumba tu wa ardhi, bali ni Mola wa ulimwengu wote. Maana yake ni kwamba, aliyeuumba ulimwengu huu mkubwa wenye adhama, ndiye mwendeshaji pia wa masuala ya ulimwengu wenyewe. Kwa sababu hiyo, ukweli unabaki kwamba anayestahiki kuabdiwa ni yule ambaye uumbaji, umilikaji, upangaji na uendeshaji wa ulimwengu uko kwenye mamlaka yake. Baada ya kuumba ardhi, akaumba pia na kukiweka ndani yake kila kinachohitajiwa na wanadamu, wanyama na mimea. Milima mirefu iliyo imara, bahari pana na zenye vina vikubwa, misitu minene iliyotandawaa ardhini pamoja na anuai za madini yaliyotuama chini ya ardhi, yote hayo ni mambo yakidhio mahitaji ya wakazi wa ardhini. Ardhi ina baraka na mengi ya manufaa, zikiwemo aina tofauti za vyakula zinazotoka ndani yake. Hapana shaka baraka na neema hizo ni za kiwango cha kukidhi mahitaji ya wanaozihitajia bila ya kuwa na nakisi au upungufu wowote. Ni kama anavyosema Allah SWT kwamba, ameumba vile vyenye ulazima kwa ajili ya kuwawezesha viumbe waendelee kuishi. Suali ni je baraka hizo na yote hayo yenye manufaa kwa viumbe yamejiotea na kujitokeza yenyewe kwa yenywe ardhini au kuna mtu yeyote pia ambaye amemsaidia Mwenyezi Mungu katika kuyaleta?! Ni wazi kabisa kwamba, sivyo hivyo asilani. Uumbaji wenyewe umefanyika hatua kwa hatua, katika awamu tofauti na kupitia marhala zilizofuatana. Awamu mbili za kwanza zilikuwa za kuifanya ardhi iwe tayari kwa ajili ya kutumika; na marhala mbili nyingine zilikuwa za kuwezesha aina mbali mbali za neema kujitokeza ardhini. Kwa hiyo kwa ujumla awamu na marhala hizo zilikuwa nne ili kuifanya ardhi iwe na utayari wa kupokea na kuwahudumia wakazi wake na kudhamini mahitaji yao yote kikamilifu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, muumbaji wa ulimwengu na mwendeshaji wake ni mmoja. Ni kinyume na mtazamo waliokuwa nao washirikina, ambao wakiamini kwamba Mwenyezi Mungu ndiye muumbaji, lakini wakiitakidi kuwepo kwa vitu au watu ambao ni washirika wake katika uendeshaji wa masuala ya ulimwengu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mfumo wa uumbaji umefanyika hatua kwa hatua na kwa awamu; si jambo lililofanywa kwa mpigo na papo kwa papo. Kama ambavyo uumbaji wa ardhi pia umefanyika hatua kwa hatua kupitia awamu mbili. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, katika ishara za kuonyesha kuwa Mwenyezi Mungu SWT ni Mola Mlezi, ni anuai za riziki na baraka alizoeneza ardhini ili zikidhi mahitaji ya wanadamu wote. Bila ya shaka na kwa masikitiko ni kwamba, ugawaji usio wa kiadilifu, israfu na miamala ya kidhalimu na kionevu vimesababisha watu wengi duniani leo wawe mafakiri na waishi maisha ya ukata na unyonge.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 11 na 12 ambazo zinasema:
ثُمَّ اسْتَوَىٰ إِلَى السَّمَاءِ وَهِيَ دُخَانٌ فَقَالَ لَهَا وَلِلْأَرْضِ ائْتِيَا طَوْعًا أَوْ كَرْهًا قَالَتَا أَتَيْنَا طَائِعِينَ
Kisha akazielekea mbingu, na zilikuwa moshi, akaziambia hizo na ardhi: Njooni, kwa khiari au kwa nguvu! Vyote viwili vikasema: Tumekuja nasi ni wat'iifu.
فَقَضَاهُنَّ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ فِي يَوْمَيْنِ وَأَوْحَىٰ فِي كُلِّ سَمَاءٍ أَمْرَهَا ۚ وَزَيَّنَّا السَّمَاءَ الدُّنْيَا بِمَصَابِيحَ وَحِفْظًا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ
Basi akazifanya mbingu saba kwa siku mbili, na akazipangia kila mbingu mambo yake. Na tukaipamba mbingu ya dunia kwa mataa na kwa ulinzi. Hayo ndio makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye Kujua.
Baada ya kubainisha rehma za Mwenyezi Mungu katika uumbaji wa ardhi na kuweka ndani yake aina mbali mbali za neema zinazohitajiwa na wakazi wake, aya hizi zinazungumzia uumbaji wa mbingu kwa kusema: Wakati Allah alipotaka kuziumba mbingu, kwanza aliufanya uumbaji wake katika sura ya mrundiko mkubwa na uliotandawaa, wa gesi ambazo alizisarifu katika umbo na mfumo maalumu na kuzisimamisha juu ya mhimili madhubuti. Irada ya Allah SWT katika uumbaji wa mbingu na ardhi ilikuwa ya namna na hali maalumu, kiasi cha kuvifanya viwili hivyo visikhitari namna yoyote ile isipokuwa kumtii Muumba wa ulimwengu. Ikiwa na maana kwamba, zitake zisitake ilipasa ziumbike kwa hali na maumbo aliyotaka Allah SWT. Kama ilivyokuwa kwa ardhi, ambayo ilikuwa tayari kupokea wakazi wake baada ya kuzipita awamu na marhala mbili za uumbwaji, mbingu pia pamoja na adhama kubwa ziliyonazo ziliumbika kwa namna alivyotoka Mwenyezi Mungu Mtukufu kupitia marhala na awamu mbili maalumu. Allah SWT, tab’an ameumba mbingu saba; na ile tuionayo sisi imetanda juu yetu angani ni sehemu ya mbingu ya kwanza tu. Kwa maneno mengine ni kwamba, ulimwengu wa maumbile umeumbwa katika sura ya majimui saba adhimu, ambapo kati ya hizo ni majimui moja tu ndiyo tunayoiona sisi wanadamu kwa macho yetu. Kiasi kwamba hata darubini za kisasa kabisa za kuonea mbali zilizotengenezwa na mwanadamu hazijaweza kupenya na kushuhudia yaliyo mbali zaidi ya eneo letu hili la mbingu ya kwanza. Nukta nyingine ni kwamba, wakati wa usiku, nyota hugeuka kuwa pambo la mbingu kwa kung’ara mithili ya taa zenye nuru. Kila moja ya nyota hizo imebeba siri mbali mbali za uumbaji ikimvuta mwanadamu kwenye tafakuri juu ya ulimwengu na Muumba wake adhimu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amezihifadhi na kuzilinda mbingu na hatari yoyote ile. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mbingu mwanzo wake zilikuwa katika sura ya moshi na gesi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ulimwengu wote wa maumbile unatii amri ya Allah SWT. Kwa hiyo sisi wanadamau tujitahidini tusiwe sehemu kinzani iendayo kinyume na urari na utangamano huo uliowekwa na Mola. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, mfumo wa uumbaji ni mpana sana na wa kina mno kupita ulivyo uelewa na ufahamu wetu. Vyote tuvionavyo katika sayari na nyota au tutakavyovigundua katika siku za usoni vinahusiana na hii mbingu ya kwanza tu iliyoko mbele ya macho yetu. Mwanadamu hana elimu wala ujuzi wowote kuhusu mbingu zingine na vitu vinginevyo vilivyoumbwa na Allah katika mfumo mpana wa ulimwengu wa uumbaji. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, kila kilichopo ni dhihirisho la elimu na uwezo wa Mwenyezi Mungu, ambaye ameiumba na anaiendesha dunia kwa mizani na vipimo maalumu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 875 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake washukurivu kutokana na anuai za neema anazotuneemesha katika kila siku ya maisha yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/