Sura ya Fuss’ilat, aya ya 29-30 (Darsa ya 879)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 879 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 41 ya Fuss’ilat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 29 ya sura hiyo ambayo inasema:
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا رَبَّنَا أَرِنَا اللَّذَيْنِ أَضَلَّانَا مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ نَجْعَلْهُمَا تَحْتَ أَقْدَامِنَا لِيَكُونَا مِنَ الْأَسْفَلِينَ
Na walio kufuru watasema: Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe walio tupoteza miongoni mwa majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni wa walio chini kabisa.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia tapo la makafiri waliokuwa wakiwazuilia watu kusikiliza aya za Qur’ani tukufu. Aya hii tuliyosoma inasema, watu waliopotoka kutokana na vitimbi vya makafiri hao, Siku ya Kiyama watashtaki na kulalamika dhidi ya wapotoshaji hao. Watu hao watamwomba Mwenyezi Mungu awaweke mahali pabaya kabisa na palipo duni zaidi motoni wale wapotoshaji wenye sifa za kishetani waliowaghilibu wao; na vile vile awaruhusu wao wawaweke chini ya miguu yao na kuwatimba na kuwakanyaga wapotoshaji hao ili kwa kufanya hivyo, wawadhalilishe na kuwadunisha japokuwa walikuwa na hadhi na vyeo walipokuwa duniani. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Siku ya Kiyama, watu waliokufuru watajaribu kutafuta wengine wa kuwabebesha mzigo wa ukafiri na upotokaji wao na kutaka kuonyesha kuwa, kupotoka kwao kulisababishwa na watu wengine. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kuna watu na vitu vingi vinavyosababisha mtu kupotoka duniani na kuhasirika akhera. Miongoni mwao ni mashetani wapotoshaji na watu wanaowazaini na kuwaghilibu wenzao. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, wafuasi wa viongozi wapotofu na wanaoshupalia ukafiri, ambao hapa duniani waliwaingiza watu kwenye upotofu kwa kuwatawala na kuwadhibiti, Siku ya Kiyama, watatamani wawadhalilishe kwa kuwaweka chini ya miguu yao na kuwakanyaga viongozi wao hao.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 30 ambayo inasema:
إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ
Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakawa na msimamo, huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiwe na hofu, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa.
Aya hii inatuonyesha kuwa, kinyume na wanaokufuru na wanaopotoka kwa kuitika kila mwito na kufuata kila wanaocholinganiwa ili kuikumbatia dunia na anasa zake, kuna kundi la watu ambao hawaitiki mwito na kufuata, isipokuwa yale yanayolinganiwa na Mitume wa Mwenyezi Mungu. Wao wanamwamini Allah tu SWT na wala hawashughulishwi na wito na maneno mengine yoyote yale. Wao wanatamka bayana kuwa Mola wetu sisi ni Allah. Wanasimama imara bila kuyumba katika kauli yao hiyo. Imani juu ya Kiyama na ahadi walizopewa na Allah ni thabiti na zimekita mizizi ndani ya nyoyo zao, kiasi kwamba, badala ya ahadi za kupita za hapa duniani, lenye uzito na maana kwao, ni ahadi zisizo na chembe ya shaka za malipo mema ya milele, alizowapa Mola wao. Kwa hivyo hakuna chochote cha kuwateteresha na kuwadhoofisha katika kutekeleza wajibu na maamrisho ya dini yao. Hakuna shaka kuwa, wanaodai kwa ndimi zao kwamba wanamwamini Allah ni wengi mno, lakini inapofika hatua ya kuthibitisha imani hiyo kwa matendo, wengine huwa wanayumba. Hao ni wale wenye imani dhaifu, ambao wanapokabiliwa na dhoruba za shahawa na matamanio ya nafsi, au pale maslahi yao ya kimada na ya kidunia yanapokuwa hatarini, hupoteza hata hizo imani dhaifu walizonazo. Kusema kweli ni wachache, watu wanaoweza kuhimili nguvu za ushawishi wa matamanio ya nafsi zao au vichocheo vya kukidhi matakwa haramu ya jamaa zao wa karibu na marafiki zao. Aidha, ni watu wachache ambao wanapokabiliwa na hatua na vitisho vya adui huwa hawaregei wala kuyumba kiimani. Alaa kulli hal, utaratibu wa Allah ni kwamba, Yeye huwapa auni na msaada wake wale walio waumini wa kweli. Na mojawapo ya njia ya kuwafikishia msaada huo ni kuwateremsha malaika kwenye nyoyo za waumini hao, wanaowapa moyo na matumaini, ambayo huwaondolea hofu ya adui na ya kufikwa na hatari yoyote katika mustakbali na vile vile kuwafanya wasiwe na ghamu na huzuni kwa yaliyotangulia. Malaika huwapa watu kama hao bishara ya malipo ya Pepo. Hapana shaka bishara hizo za malaika wa Mwenyezi Mungu hutandawaa juu ya roho na nafsi za watu waumini zikawapa nguvu ya kukabili dhoruba za shida na misukosuko ya maisha na kuendelea kuwa na moyo na msimamo thabiti wanapokaribia kuyumba au kuteleza. Kimsingi hasa ni kwamba miongoni mwa wajibu na majukumu ya waumini hapa duniani ni kudhibiti nafsi zao na maasi, hawaa na matamanio, ambayo yatawasababishia kupotoka na kuhasirika. Lakini watakapofika huko akhera, Allah SWT atawafidia yale aliyowakataza na kuwazuilia duniani ili kuwatahini, kwa kuwapa kila kitakachotakiwa na kutamaniwa na nyoyo zao. Sababu ni kuwa, peponi si mahali pa kuharibika na kupotoka mtu. Waumini hao wataingizwa kwenye Pepo ya milele na kukirimiwa kwenye dhifa waliyoandaliwa na Mola wao aliyetukuka. Mwenyeji wa dhifa hiyo ni Allah SWT, Mkarimu na Mrehemevu; na wageni wake ni waja hao safi na wema wa Peponi. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, ikiwa waumini wenye msimamo thabiti watabakiwa na marafiki wachache hapa duniani kwa sababu ya msimamo wao huo, wajue kwamba malaika wa Mwenyezi Mungu ni vipenzi na marafiki zao wa mbinguni, ambao watawasaidia na kuwapa msukumo hapa duniani na huko akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, raha na starehe za peponi haziishii kwenye starehe na mambo ya kimada na yanayotamaniwa na upande wa kimwili tu wa mtu, bali chochote kile kitakachomstarehesha na kumpa raha kitapatikana huko. Ni wazi kwamba hali za furaha na raha za kimaanawi watakazopata watu wa peponi hazitakuwa chache kulinganisha na raha za kimaada watakazostareheshwa nazo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, Allah SWT ataamiliana na watu wa peponi kwa msingi wa rehma na usamehevu; na hii inadhihirisha ukarimu na uraufu usio na ukomo wa Mola Muumba kwa waja wake hao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 879 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie dhambi zetu, atutukabalie amali zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/