May 24, 2023 08:58 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 880 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 41 ya Fuss’ilat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 31 na 32 za sura hiyo ambazo zinasema:

نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ

Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata kinacho tamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyo vitaka.

نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ

Ni takrima itokayo kwa Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

Aya hizi zinaendeleza yaliyoelezwa katika aya tulizosoma katika darsa iliyopita zilizozungumzia kuteremka malaika juu ya nyoyo za waumini wa kweli na kubainisha kwamba, malaika hao si vipenzi na wasaidizi wa waumini hapa duniani tu, lakini hata huko akhera pia watakuwa mithili ya rafiki waaminifu watakaowasaidia na kuwa pamoja nao mpaka watakapowaongoza kuelekea peponi. Hapa duniani, malaika huwapa waumini wenye istikama na imani thabiti bishara ya ushindi dhidi ya batili. Na huko akhera pia watawakirimu kwa dhifa adhimu katika Pepo ya Allah SW. Huko watakuta wameandaliwa kila aina ya neema ambazo nafsi zao zitatamani. Na si neema za vitu vya kimaada tu, lakini yale ambayo yatazipa roho na nafsi zao raha ya kimaanawi pia wataandaliwa na kuzikuta huko. Na hii ni kwa sababu moja ya majukumu ambayo waumini walikuwa nayo walipokuwa duniani ilikuwa ni kudhibiti nafsi zao kwa kutofuata hawaa na matamanio ya nafsi, kwa sababu kufanya hivyo kungepelekea wapotoke na kuhasirika. Lakini huko akhera, Allah SWT atawafidia yote aliyowakataza na kuwazuilia, na kuwapa kila kitakachotamaniwa na nyoyo zao. Kwa sababu Peponi si mahali pa maovu na upotovu. Wao wataingia kwenye pepo hiyo ya milele wakiwa wageni wa Mwenyezi Mungu. Wageni wa dhifa ambayo, mwenyeji wake ni Yeye Allah Mwingi wa Rehma na Mwenye Kurehemu na wageni wake waalikwa ni waja wake hao wema wa peponi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ikiwa waumini wenye imani thabiti watabakiwa na rafiki wachache duniani, wajue kwamba malaika ni sahibu zao wa mbinguni ambao watawasaidia na kuwa pamoja nao duniani na akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, raha za peponi si za vitu vya kimaada na vinavyotamaniwa na mwili tu wa mtu, bali kila kitakachomburudisha mtu, kitakuwa kimeandaliwa na kupatikana huko. Ni wazi kwamba raha na burudani za kimaanawi watakazopata watu wa peponi hazitakuwa chache kulinganisha na zile za kimaada watakazoneemeshwa huko. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Allah SWT ataamiliana na watu wa peponi kwa rehma na usamehevu na hii inadhihirisha wema, ukarimu na uraufu usio na kikomo wa Mola kwa waja wake hao.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 33 ambayo inasema:

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ

Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu? 

 Kinyume na watu waliokuwa wakiwazuilia wenzao wasisikilize maneno ya Bwana Mtume SAW na aya za Qur’ani na kutoruhusu maneno ya haki yawafikie watu, aya hii inasema: baadhi ya watu wanawalingania wenzao wito wa Allah kwa maneno na matendo yao. Watu hao husema, wao ni miongoni mwa Waislamu na wanajivunia kuwa kwao Waislamu. Kwa mujibu wa aya hii, maneno ya mtu yeyote yule hayana thamani kama ya wafanya tablighi ya kulingania watu wito wa tauhidi wa Allah SWT; watu ambao wanautilia nguvu na kuufanya ukubaliwe na kufuatwa wito huo, kwa vitendo na amali zao njema. Bila shaka haitoshi mtu kuitambua haki lakini akawa anaifuata yeye mwenyewe tu, bali inatakiwa awalinganie na kuwafikishia na wenzake pia wito huo wa Allah; na katika matendo yake, aonyeshe kuwa yeye amejisalimisha kwa Yeye Mola na anayatekeleza maamrisho yake katika maisha ya kila siku. Tab’an katika suala hili, kuna ulazima wa kuwepo baadhi ya watu ambao watajikita katika kusomea na kubobea kwenye elimu za dini na kufanya tablighi na uenezi wa wito wa haki. Hao ndio maulamaa na wafanya tablighi ya dini, ambao jukumu lao ni kuyalinda mafundisho yake na kusafisha kutu za shaka ndani ya nyoyo za waumini. Pamoja na hayo, kazi hiyo inayofanywa na watu hao, haiwaondolei dhima na masuulia Waislamu wengine pia. Kwa kweli kila Muislamu, na kulingana na uwezo wake na suhula alizonazo ana wajibu wa kuwalingania watu dini ya Mwenyezi Mungu na kufanya juhudi za kuutambulisha na kuueneza wito huo wa tauhidi. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, maneno bora kabisa ni ya kuwalingania watu dini ya Allah; tab’an ulinganiaji huo ufanywe na mtu ambaye yeye mwenyewe ni mtekelezaji wa ayasemayo na awe amejisalimisha kivitendo kwa Allah SWT. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, adhana ni njia nyepesi zaidi na mfano wa wazi zaidi wa kuwalingania watu wote wito wa Allah SWT. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, tujivunie na kuona fakhari kuwa Waislamu na kuwa wenye kujisalimisha kwa Allah SWT na wala tusiyumbishwe au kudhoofishwa na kuhofishwa na kejeli na udunishaji wa wapinzani wa haki.

Zifuatazo sasa ni aya za 34 na 35 ambazo zinasema:

وَلَا تَسْتَوِي الْحَسَنَةُ وَلَا السَّيِّئَةُ ۚ ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ

Mema na maovu hayawi sawa. Zuia uovu kwa lilio jema zaidi. Mara yule ambaye baina yako na yeye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu.

‏ وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ

 Lakini hawapewi wema huu ila wanao subiri, wala hawapewi ila wenye bahati kubwa. 

Wapinzani wa haki hutoa maneno machafu, uzushi, kejeli na kauli tofauti za mashinikizo na vitisho. Kwa hivyo ili kuweza kuwalingania watu hao katika njia iliyonyooka, inabidi mtu awe na moyo wa subira na uvumilivu. Na ndiyo maana katika aya hizi, Allah SWT anasema: Ijapokuwa wao wanatumia mbinu chafu katika kupingana na nyinyi, lakini haifai nyinyi kufanya kama wafanyavyo wao. Nyinyi mnapaswa mfanye mambo kwa kufuata haki na wala msilipe ubaya, kwa ubaya mliofanyiwa, wala uovu kwa uovu mliotendewa. Tumieni njia ya upendo na upole. Kwa hivyo amilianeni nao kwa wema na yajibuni maneno yao makali na machafu kwa kutumia lugha ya upole na mantiki. Ni wazi kwamba mkidumisha mwenendo huo, nyoyo za watu hao zitabadilika, chuki na uadui wao utatoweka na upendo na urafiki baina yenu utajengeka. Sira na mbinu ya ufanyaji tablighi ya Bwana Mtume SAW na Ahlul-Bayt zake AS ilifuata misingi ya mafundisho haya ya Qur’ani. Watukufu hao walikuwa wakiamiliana na kulahikiana na wapinzani wao kwa namna iliyowafanya wajutie kauli na mienendo yao. Mfano wake ni wakati ilipokombolewa Makka, ambapo baadhi ya Waislamu walikuwa wakitoa nara na kaulimbiu za ulipizaji kisasi, lakini badala yake Bwana Mtume Muhammad SAW akatangaza msamaha kwa watu wote. Mwenendo huo wa kustaajabisha wa mtukufu huyo uliziteka na kuziathiri mno nyoyo za washirikina wa Makka. Bila shaka si jambo jepesi mtu kuweza kuamiliana hivyo na wenye kumfanyia uadui, bali anahitaji kuwa na kifua kipana cha subira na moyo mkubwa wa uvumilivu. Hakika ni kwamba, inabidi mtu awe amejengeka kiimani na kinafsi na kufikia daraja maalumu ya ukamilifu wa kimaadili na kiakhlaqi mpaka aweze kirahisi kuuzima moto wa ulipizaji kisasi ndani ya nafsi yake na kuamua kulipa wema kwa mabaya aliyotendewa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mfano mmojawapo wa kivitendo wa kulingania watu dini ya Allah ni kuamiliana nao kwa wema licha ya ubaya waliotufanyia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, katika medani ya vita na adui, ni sahihi na inakubalika kumlipizia ubaya sawa na aliotutendea, lakini katika mahusiano ya kijamii, kulipiza kisasi na kumtenda aliyekutenda huwa ni ishara ya kutokuwa na ustahamilivu. Mtazamo wa akutendaye mtende, huzidisha mivutano na uhasama katika jamii. Aya hizi vile vile zinatuelimisha kwamba, kuwavumilia watu kwa maneno yao machafu au mwenendo wao muovu kunahitaji mtu awe na kiwango cha kutosha cha imani na akhlaqi njema.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 36 ambayo inasema:

وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ ۖ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

Na kama Shet'ani akikuchochea kwa uchochezi basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. 

Inatupasa tujue kwamba wasiwasi wa shetani humjia mwanadamu kwa sura na njia tofauti. Mfano mmojawapo ni kwamba, shetani huwa anajaribu kila mara kuchochea vinyongo na uadui baina ya watu na huchukizwa sana anapoona watu wamepatana na kuishi kwa upendo na masikilizano. Kwa hivyo katika aya hii, Mwenyezi Mungu Mtukufu anamhutubu Mtume wake na Waislamu wote ya kwamba, kila mnapovumilia maneno mabaya katika kuwalingania watu dini ya Mwenyezi Mungu na mkazungumza nao kwa upole, huruma na upendo, wale wenye sifa za kishetani watakuchocheeni kwamba haifai kulegeza msimamo kwa anayekufanyia ubaya, bali inatakiwa umtende kama alivyokutenda kwa kumpa jibu kali. Kwa hivyo jihadharani; na mjue kwamba chokochoko za aina hiyo zinatokana na shetani hata kama mtazisikia kupitia ndimi za baadhi ya marafiki zenu. Kwa hivyo msikubali abadan kufuata maneno hayo. Ili kufikia lengo, ambalo ni kuwaongoza watu katika njia ya haki, kuweni thabiti kiimani; na badala ya kuwaghadhibikia watu kwa maneno mabaya wanayokuambieni, amilianeni nao kwa bashasha na lugha ya upole. Muelekeeni Allah, ombeni hifadhi ya nusra Yake na mwaminini Yeye, hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mjuzi wa kila kitu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kutaka kulipiza kisasi kwa mabaya tunayotendewa kunatokana na wasiwasi wa shetani; na kukabiliana kwa upole na maneno mazuri na wanaotufanyia ubaya ni jambo linalousiwa na Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, yeyote anayemchochea mtu kufanya mabaya ni shetani, hata kama atakuwa na sura ya binadamu. Halikadhalika aya hii inatuelimisha kwamba, kutubia na kukimbilia kwa Allah ndio njia ya kumuepusha mtu na wasiwasi wa shetani. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 880 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah awape moyo wa usamehevu tunaowakosea na azijaze nyoyo zetu uvumilivu kwa tunayotendewa na usamehevu kwa wanaotukosea. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/