May 24, 2023 09:02 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 881 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 41 ya Fuss’ilat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 37 na 38 za sura hiyo ambazo zinasema:

وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ

Na katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na mwezi. Basi msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliye viumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu Yeye tu.

فَإِنِ اسْتَكْبَرُوا فَالَّذِينَ عِندَ رَبِّكَ يُسَبِّحُونَ لَهُ بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَهُمْ لَا يَسْأَمُونَ

Na ikiwa watafanya kiburi, basi hao walioko kwa Mola wako Mlezi wanamtakasa Yeye usiku na mchana, na wao hawachoki.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia kuwalingania na kuwaita watu kwenye tauhidi na kumwabudu Mola pekee wa haki. Katika aya hizi mbili tulizosoma umeashiriwa mfano mmoja wa shirki ambayo imekuwepo katika zama mbali mbali za historia na kuelezwa kwamba, jua na mwezi ni viumbe vya Mwenyezi Mungu, lakini inakuwaje baadhi ya watu badala ya kumuabudu Allah SWT aliyeumba jua na mwezi, wanaviabudu viumbe hivyo!? Ukweli ni kwamba, usiku na mchana na jua na mwezi, vyote hivi ni katika alama na ishara za Muumba wa ulimwengu. Usiku ni kitu cha kupatia utulivu na mapumziko; na mwangaza wa mchana ni wenzo wa kufanyia shughuli na harakati za maisha. Viwili hivyo ndivyo vinavyozungusha kwa nidhamu na mpokezano maalumu gurudumu la maisha ya wanadamu. Laiti mojawapo kati ya usiku na mchana ungekuwepo milele au ungedumu kwa muda mrefu kupindukia, maisha ya viumbe hai yangetoweka na sayari ya dunia isingelikalika. Jua ni chimbuko la baraka zote za kimaada zilizopo katika mfumo wa maumbo ya sayari. Hapana shaka, maisha katika sayari hii ya dunia, yamewezekana kwa kuwepo kwa jua. Mwangaza, joto, kuvuma kwa upepo, kunyesha kwa mvua, kuota kwa mimea, kuiva kwa matunda na hata rangi nzuri nzuri na za kupendeza za maua, vyote hivyo vinachangiwa na kuwepo kwa jua; na laiti kama jua lisingekuwepo, asingetokea kiumbe hai hata mmoja ardhini. Mwezi kwa upande wake, nao pia uko kwenye mwendo na harakati yenye nidhamu maalumu, ukipita kwenye vituo tofauti na kufanya kazi ya kutoa mwanga na nuru inayowaangazia watembeao uwandani na wapoteao majangwani. Vitu vyote hivyo vya maumbile ni viumbe vya Mwenyezi Mungu Mtukufu na ni katika alama na ishara zake za wazi kabisa. Hata hivyo, kutokana na baraka nyingi mno za mwezi na jua, baadhi ya watu walikuwa wakiyasujudia na kuyaabudu maumbo hayo mawili ya mbinguni yang’arayo. Lakini ingefaa tujiulize, ni nani mwenye akili timamu anayekubali kwamba jua na mwezi vimejizukia vyenyewe tu!? Nyinyi wanadamu inakupaseni mumwabudu na kumsujudia yule aliyeumba jua na mwezi; na Yeye ndiye chimbuko la neema zote hizi. Kuliabudu jua na mwezi huwa ni sawa na mtu kuona picha ya mchoro mzuri sana wa kupendeza, lakini badala ya kumsifu na kumtukuza mchoraji wa mchoro huo akaitukuza picha yenyewe iliyochorwa! Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba, katika kulinganiwa kumwabudu Mola pekee wa haki, kundi moja la watu ambao wana kiu ya kuijua haki, wanaupokea wito huo na kumwabudu Allah SWT; lakini watu wa kundi jengine, na kwa sababu ya moyo wa kutakabari na taasubi za kung’ang’ania kufuata imani na itikadi za waliowatangulia, husimama dhidi ya haki na hawawi tayari kutafakari na kutumia akili zao. Kwa hivyo nyinyi msikereke kwa kuona watu wengi wanang’ang’ania kufuata itikadi zao hizo potofu, kwa sababu malaika waliojikurubisha kwa Allah, wao wanamsabihi na kumhimidi Yeye Mola na katu hawaoni uvivu wala hawachoki kufanya hivyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kupishana kwa usiku na mchana kuna faida nyingi sana kwa mwanadamu na viumbe vingine; na ni miongoni mwa ishara za uwezo na hikma ya Mwenyezi Mungu SWT. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuyatambua maumbile na vitu muhimu vya uhai ndio njia bora ya kumjua Mwenyezi Mungu, tab’an kwa watu walio na nia ya kweli ya kujua asili ya uumbaji. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, kuabudu, asili yake ni suala la kifitra na kimaumbile, lakini kosa wanalofanya watu wengi, ni katika kutambua na kubaini ni kitu gani wanapaswa kukiabudu. Mitume wamekuja kulielekeza hitajio hili la kimaumbile la mwanadamu katika njia sahihi. Vile vile aya hizi zinatutaka tujue kuwa, kutakabari na kujikweza ni miongoni mwa vizuizi vinavyomfanya mtu asiifahamu na kuikubali haki. Halikadhalika tunajifunza kutokana na aya hizi kwamba, Allah SWT si mhitaji wa ibada za waja. Hata kama wanadamu wote watamsahau Mwenyezi Mungu, malaika wamejisalimisha kwa Yeye Mola na wanamsabihi na kumhimidi bila kuchoka usiku na mchana.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 39 ambayo inasema:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنَّكَ تَرَى الْأَرْضَ خَاشِعَةً فَإِذَا أَنزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ ۚ إِنَّ الَّذِي أَحْيَاهَا لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۚ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi kavu na yabisi, lakini tunapo iteremshia maji mara unaiona inataharaki na kuumuka. Bila ya shaka aliye ihuisha ardhi ndiye atakaye huisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.

Baada ya jua na mwezi, aya hii inazungumzia maeneo ya ardhi kavu na yabisi, ambayo huhuika baada ya kunyeshewa na matone yenye kuleta uhai ya mvua na kubadilika kuwa maeneo yenye rutuba yanayojaa juu yake maua, mimea na miti ya kijani kibichi iliyonawiri. Ardhi kavu isiyo na uhai, ambayo haizalishi chochote zaidi ya madongo, matofali na magome ya ufinyanzi, inaponyeshewa na mvua, hutokeza juu yake athari za uhai na vielelezo vyake vya namna tofauti. Wakati mvua inaponyesha, ardhi huwa mithili ya shamba linalochipua na kumea juu yake anuai za miti na mimea na hivyo kujitokeza harakati na vuguvugu la uhai na maisha. Hebu na tujiulize, ni nguvu gani ambayo kwa kumiminika matone ya mvua inawezesha kutokea athari zote hizo za uhai ndani ya ardhi iliyokuwa mfu na yabisi? Bila shaka hiyo ni katika ishara za ujuzi na uwezo usio na kikomo wa Allah SWT. Na je Mungu huyo, ambaye alama na ishara za uwezo wake zinashuhudiwa kila mahali, hatoweza kuwafufua tena wanadamu Siku ya Kiyama? Na je, tuna shaka sisi wanadamu na uwezo wake na tunadhani ni muhali Yeye kuweza kufanya hivyo? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, vitu vya maumbile kama upepo, mvua, udongo na mimea, vyote hivyo ni ishara na alama za uwezo usio na kikomo wa Allah SWT. Kwa hiyo kila inapotuingia shaka kuhusu uwezo wake Mola, tuviangalie na kuvitafakari vitu vya kimaumbile kama hivyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kuutilia shaka uwezo wa Mwenyezi Mungu, ni miongoni mwa sababu za baadhi ya watu kukanusha maadi, yaani kufufuliwa kwa viumbe; na si kwamba watu hao wana hoja hasa madhubuti za kimantiki za kukanushia jambo hilo.

Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 40 ya sura yetu ya Fuss'ilat ambayo inasema:

إِنَّ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي آيَاتِنَا لَا يَخْفَوْنَ عَلَيْنَا ۗ أَفَمَن يُلْقَىٰ فِي النَّارِ خَيْرٌ أَم مَّن يَأْتِي آمِنًا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ اعْمَلُوا مَا شِئْتُمْ ۖ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

Hakika wale wanao upotoa ukweli uliomo katika Ishara zetu hawatufichikii Sisi. Je! Atakaye tupwa Motoni ni bora, au atakaye kuja kwa amani Siku ya Kiyama? Tendeni mpendavyo, kwa hakika Yeye anayaona mnayo yatenda.

Kinyume na Mitume na waliowaamini, ambao wanawalingania watu wito wa Allah na kuwabainishia aya, ishara na alama zake, kuna watu ambao wanawavuta na kuwaelekeza wenzao kwenye dhalala na upotovu. Wao hujaribu kutumia kila njia kuwafanya watu wengine wakanushaji wa dini na wenye kujiweka mbali na njia ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Kwa kutumia lugha ya hadaa, ambayo kidhahiri ni ya maneno sahihi, watu hao huyatafsiri maneno ya Allah na mafundisho ya Mitume kwa namna ya kuyafanya yaonekane hayaendani na akili na busara, na hivyo kupelekea watu kujiweka mbali na Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Ni kama tushuhudiavyo leo hii pia, ambapo kuna fikra na harakati mbali mbali zinazotumia nyenzo tofauti za upashaji habari ili kujaribu kuwapotosha watu kuhusu imani ya dini na kufufuliwa. Ni wazi kwamba malipo ya watu kama hao Siku ya Kiyama, wanaoeneza shaka ili kuwatenganisha watu na njia ya haki ni adhabu kali ya moto wa Jahanamu; kinyume na wale ambao baada ya kuijua haki wanaikubali. Hao watawekwa chini ya kivuli cha amani ya Allah na wataishi peponi kwenye upeo wa utulivu, raha na uneemevu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, ikiwa tunaona Allah anatoa fursa na muhula kwa watu wapotofu, si kama hana uelewa au ameghafilika nao; ni kaida na utaratibu wa Allah kutoa muhula ili watu waitumie hiari ya kuchagua waliyopewa na kuwapatia fursa pia ya kuweza kutubia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, huko akhera, neema muhimu zaidi kwa mtu ni amani ya mwili na roho na utulivu wa fikra. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, kuwa na hiari, maana yake si kumjuzia mtu kufanya lolote lile atakalo. Mambo pekee anayotakiwa mtu kufanya ni yale yanayokubaliana na akili timamu na kuendana na sheria na hukumu za dini. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 881 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, azifanye thabiti imani zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/