Sura ya Fuss’ilat, aya ya 41-44 (Darsa ya 882)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 882 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 41 ya Fuss’ilat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 41 na 42 za sura hiyo ambazo zinasema:
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِالذِّكْرِ لَمَّا جَاءَهُمْ ۖ وَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌ
Kwa hakika wanao yakataa mawaidha haya yanapo wajia (wataangamia), na haya bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu.
لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ
Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia watu wanaotumia maneno ya hadaa na ya kupotosha dini ili kujaribu kuwavuta watu kwenye dhalala na upotofu na kuwafanya wajitenge na kujiweka mbali na dini na aya za Qur’ani. Aya hizi tulizosoma zinasema: Hii Qur’ani imeteremshwa kwa ajili ya kuwakumbusha watu wazinduke kutoka kwenye usingizi wa mghafala na kurejea kwenye fitra na maumbile safi waliyoumbiwa na Mola wao. Lakini kwa masikitiko, baadhi ya watu wanaikanusha na kuukataa ukweli wa dini, wakati ukanushaji wao huo hauwezi kupunguza chochote katika thamani ya kitabu hiki cha mbinguni. Kitabu hiki cha Allah ni cha kudumu milele na wala hakishindiki; ni kitabu ambacho mantiki yake iko wazi kabisa, hoja zake ni madhubuti na mafundisho yake yana chimbuko na misingi imara. Katika kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu adhama ya Qur’ani, aya hizi zinasema, kitabu hiki kimeteremshwa na Allah SWT, ambaye yote ayafanyayo yanatokana na hekima na yako kwenye upeo wa juu kabisa wa usahihi na ukamilifu. Ni wazi kwamba kitabu kilichoteremshwa na Mwenyezi Mungu Mwenye hekima na Mhimidiwa, hakiwezi kuwa na neno lolote la batili, si katika ya kabla wala baada yake. Hauonekani mgongano wowote katika aya zake, hukumu na mafunzo yaliyomo ndani yake hayana kasoro yoyote na hakuna awezaye kuyatia mkono kuyabadilisha. Si hayo tu, lakini pia hakuna mwenye uwezo wa kuubatilisha ukweli uliomo ndani yake; na hata katika zama zijazo pia ugunduzi na maendeleo ya kielimu ya wanadamu havitaweza kuyatia ila au kuyatoa kasoro yoyote ile mafunzo na mafundisho yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ili kuweza kujiepusha na upotofu na mghafala katika dunia ya leo iliyojaa vishawishi na vitamanishi, tusomeni Qur’ani, ambayo ni utajo wa mawaidha na ukumbusho wa hakika za mambo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Qur’ani inatupa habari ya hali ya baada ya kuteremshwa kwake kwa kutangaza kinagaubaga kuwa, hakutatokea wa kuitoa kasoro, wa kuitia mkono ili kuibadilisha na wala halitapatikana abadani, lolote lile la batili ndani yake. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, njama na vitimbi mbali mbali vinavyofanywa dhidi ya Qur’ani havitafua dafu. Kwa hiyo vyovyote vile watakavyojaribu kufanya maadui wa Qur’ani, hawataweza kukiondoa kitabu hicho cha mbinguni katika masuala ya kijamii ya Waislamu. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, kwa vile aya za Qur’ani, ni dhihirisho la ujuzi na hekima ya Allah SWT, basi ziko sahihi kabisa na zimejaa hekima; na ndio msingi imara wa dini tukufu ya Uislamu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 43 na 44 ambazo zinasema:
مَّا يُقَالُ لَكَ إِلَّا مَا قَدْ قِيلَ لِلرُّسُلِ مِن قَبْلِكَ ۚ إِنَّ رَبَّكَ لَذُو مَغْفِرَةٍ وَذُو عِقَابٍ أَلِيمٍ
Huambiwi ila yale yale waliyo ambiwa Mitume wa kabla yako. Hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ni Mwenye maghfira, na ni Mwenye adhabu chungu.
وَلَوْ جَعَلْنَاهُ قُرْآنًا أَعْجَمِيًّا لَّقَالُوا لَوْلَا فُصِّلَتْ آيَاتُهُ ۖ أَأَعْجَمِيٌّ وَعَرَبِيٌّ ۗ قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ ۖ وَالَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ فِي آذَانِهِمْ وَقْرٌ وَهُوَ عَلَيْهِمْ عَمًى ۚ أُولَٰئِكَ يُنَادَوْنَ مِن مَّكَانٍ بَعِيدٍ
Na lau tungeli ifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni wangeli sema: Kwanini Aya zake haziku pambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na (Mtume) Mwaarabu? Sema: (Hii Qur'ani) ni uwongofu na ponyo kwa wenye kuamini. Na wasio amini umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao wanaitwa nao wako pahala mbali.
Aya hizi zinaendelea kuzungumzia yale yaliyoashiriwa katika aya zilizotangulia kuhusu ukanushaji wa wapinzani wa dini na kueleza kwamba, watu hao hawakuwa wakiipiga vita Qur’ani tu, lakini walikuwa wakimvurumizia pia majina mabaya Bwana Mtume Muhammad SAW kwa kumwita mchawi, mshairi na hata mwendawazimu. Mwenyezi Mungu Mtukufu akamfariji Mtume wake kwa kumwambia, Mitume waliopita kabla yako pia walikuwa wakinasibishiwa mambo hayo na walikumbana na watu kama hao pia. Kwa hiyo usiyajali maneno yao bali endelea kufikisha ujumbe wako kwa subira na uvumilivu. Ni wazi kwamba Allah SWT ni mrehemevu na msamehevu kwa watu wajinga na wafanyao mambo kwa kutojua, lakini kwa wale wavurumizao tuhuma kwa uelewa kamili na kwa makusudi, wanaoamua kuipiga vita Qur’ani na kumfanyia uadui Mtume wa Mwenyezi Mungu, hao watafikwa na adhabu kali. Moja ya visingizio na vijisababu walivyokuwa wakivitoa baadhi ya wapinzani wa Bwana Mtume SAW ni kwamba, kwa nini kitabu ulichotuletea ni cha lugha yetu? Kama wewe ni Mtume kweli, muujiza wako inapasa uwe wa kututeremshia kitabu kisichokuwa cha Kiarabu ili tufahamu kama kweli wewe Mtume wa Mungu. Allah SWT akawajibu watu waliotoa kisingizio hicho kwa kuwaambia: Laiti kama tungeliiteremsha Qur’ani kwa lugha isiyo ya Kiarabu, hapo mngepata kisingizio cha kusema, sisi ni wazungumzaji wa Kiarabu, kwa hiyo aya za kitabu hiki haziko wazi na wala hazifahamiki. Lakini wakati sasa kimekujieni kwa lugha ya Kiarabu na mnayafahamu yaliyomo ndani yake, mnatoa maneno ya upuuzi, zogo na ubishi ili kuwapumbaza na kuwazuia watu wasisikilize aya zake. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba Qur’ani ni ponyo na uongofu kwa mwenye kuiamini; na lengo lake ni kukuongozeni kuelekea kwenye maisha safi ya utoharifu ya duniani na akhera. Aidha inataka kuziponya nyoyo zenu na kukutakaseni na uchafu wa kiakhlaqi ili muufikie ukamilifu wa kiutu. Hata hivyo kwa masikitiko, baadhi ya watu hawataki kuiona wala kuisikiliza haki, kama kwamba ni vipofu wasio na macho ya kuonea na viziwi wasio na masikio mazima ya kusikilizia. Lau kama wangeiendea Qur’ani na roho iliyoamini na moyo wenye kuitaka haki, wangeupata uongofu kutoka kwenye aya zenye nuru za kitabu hicho cha mbinguni; na maradhi ya kiroho na kiakhlaqi waliyonayo yangeponywa na kutibika. Lakini wamekuwa kama kwamba ni watu vipofu na viziwi wanaoitwa kutokea mbali, lakini hawaisikii sauti yoyote. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, viongozi na wafanya tablighi ya dini, wanatakiwa wavumilie kauli chafu za wapinzani na maneno mabaya wanayotoa dhidi yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, msamaha na adhabu ya Allah, yote mawili yanafanyika kwa hekima maalumu; na kila moja kwa mahala pake huwashajiisha wema na kuwatia adabu wabaya, japokuwa rehma za Allah zinazitangulia ghadhabu zake. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, utoaji visingizio na vijisababu wa maadui wa haki hauna mwisho; vyovyote watakavyofanya Waislamu, wao watatafuta kitu cha kuwatia ila na kuisema vibaya dini yao. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba Qur’ani ni kitabu cha uongofu. Ni tiba ya maradhi ya kiroho, kiakhlaqi, kijamii n.k. Tab’an watakaonufaika na tiba hiyo ni wale watakaotaka kuangaziwa na nuru hiyo ya uongofu, pasina kuifumbia macho na kuizibia masikio. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 882 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah, atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/