Sura ya Fuss’ilat, aya ya 49-54 (Darsa ya 884)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 884 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 41 ya Fuss’ilat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 49 ya sura hiyo ambayo inasema:
لَّا يَسْأَمُ الْإِنسَانُ مِن دُعَاءِ الْخَيْرِ وَإِن مَّسَّهُ الشَّرُّ فَيَئُوسٌ قَنُوطٌ
Mwanaadamu hachoki kuomba dua za kheri, na inapo mpata shari, mara huvunjika moyo akakata tamaa.
Kwa kawaida, watu wasiomwamini Allah au wenye imani dhaifu, huwa na fikra finyu, utovu wa ukinaifu na moyo mwepesi wa kuhimili mambo. Watu wa aina hiyo huwa hawachoki kupaparika kwa ajili ya kutafuta mali na utajiri na kupigania raha na starehe za dunia; na kadiri wanavyozidi kutajirika, hukamia kulimbikiza mali na utajiri mwingi zaidi na katu hawatosheki na kukinai na walichonacho. Lakini kama itatokezea dunia kuwapa mgongo au wakafikwa na masasibu na kuharibikiwa kimaisha, hukata tamaa kwa namna ambayo utadhani mwisho wa dunia umewadia. Kusema kweli, watu hao ambao hawakuleleka, nafsi zao zimeghiriki kwenye ulimwengu wa kimaada tu. Wakati dunia inapowapa uso hufurahi na kuwa na ghururi; na inapowapa kisogo huhuzunika na kukata tamaa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kwa kawaida hulka ya kibinadamu ni kuwa na pupa, tamaa, kupenda uneemevu na kujitakia mtu kila kizuri awe nacho yeye. Lakini mafundisho matukufu ya Mitume humlea mwanadamu ili awe na sifa ya kutoa, moyo wa kujitolea na kuwafikiria na wengine pia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kukata tamaa na kujihisi umeshagonga mwamba katika maisha ni ishara za imani dhaifu na moyo mwepesi wa kuhimili mambo. Muumini wa kweli katu hafiki hatua ya kujihisi ameshaharibikiwa moja kwa moja.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 50 na 51 ambazo zinasema:
وَلَئِنْ أَذَقْنَاهُ رَحْمَةً مِّنَّا مِن بَعْدِ ضَرَّاءَ مَسَّتْهُ لَيَقُولَنَّ هَٰذَا لِي وَمَا أَظُنُّ السَّاعَةَ قَائِمَةً وَلَئِن رُّجِعْتُ إِلَىٰ رَبِّي إِنَّ لِي عِندَهُ لَلْحُسْنَىٰ ۚ فَلَنُنَبِّئَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِمَا عَمِلُوا وَلَنُذِيقَنَّهُم مِّنْ عَذَابٍ غَلِيظٍ
Na pindi tukimwonjesha rehema itokayo kwetu baada ya kumgusa dhara, bila ya shaka husema: Haya nayastahiki mimi, wala sidhani kuwa Kiyama kitakuja. Na hata nikirudishwa kwa Mola wangu Mlezi bila ya shaka nina mema yangu kwake! Basi kwa yakini tutawaelezea walio kufuru hayo waliyo yatenda, na kwa yakini tutawaonjesha adhabu ngumu.
وَإِذَا أَنْعَمْنَا عَلَى الْإِنسَانِ أَعْرَضَ وَنَأَىٰ بِجَانِبِهِ وَإِذَا مَسَّهُ الشَّرُّ فَذُو دُعَاءٍ عَرِيضٍ
Na tukimneemesha mwanaadamu hugeuka na kujitenga upande, na inapo mgusa shari, huwa na madua marefu marefu.
Aya iliyotangulia ilizungumzia sifa za watu wasio na imani na wenye nyoyo nyepesi wakati wanapokuwa katika raha na pale wafikwapo na shida na misukosuko. Aya hizi zinalitolea ufafanuzi suala hilo kwa kueleza kwamba: watu hao hupatwa na majivuno na kuingiwa na ghururi kiasi cha kuhisi kwamba Allah hana nafasi yoyote katika maisha yao. Ukweli ni kwamba kila alichonacho mtu ameneemeshwa na Mwenyezi Mungu, lakini pamoja na hayo, badala ya kuwa mshukurivu kwa neema hizo husema: Haya niliyonayo yanatokana na ustahiki wangu mimi mwenyewe; na wala hayajachangiwa na Mwenyezi Mungu au mtu yeyote yule. Ghururi na majivuno hayo, mwisho wake humfikisha mtu kwenye kufru ya kukanusha kufufuliwa, yaani maadi. Na kwa hivyo hukadhibisha Kiyama na kusema kwa kujiamini kwamba, hakutakuwa na Kiyama. Lakini hata kama tutajaalia kwamba Kiyama kitakuwepo, basi haki yangu mimi ni kuwa na hali nzuri hata huko akhera pia na kuishi kwenye starehe na raha za juu kabisa. Lakini Allah SWT anasema kuhusu wakadhibishaji na wapinzani hao kwamba, karibuni hivi tutawajulisha yale waliyoyafanya na tutawaonjesha adhabu kali Siku ya Kiyama. Kisha aya tulizosoma zinadokeza kuhusu sifa nyingine za watu aina hiyo wasioamini haki na wenye kujisahau mara moja kwa kueleza kwamba, wakati wa uneemevu na furaha na ukunjufu wa neema huwa wanamsahau Mwenyezi Mungu na kuyapa mgongo mafundisho ya dini kwa kiburi na jeuri, utadhani hawaaamini kabisa kuwa Mwenyezi Mungu yupo na ana nafasi katika maisha yao pia. Lakini pale yanapowaandama matatizo na masaibu, humuita Mwenyezi Mungu na kumwomba dua kila mara, huku wakimlilia hali, utadhani Yeye ndiye msababishaji wa matatizo yao! Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, watu waliopotoka na waliokosa malezi ya kidini hujisahau haraka na huwa na majivuno. Wapatapo neema huwalevya na kuwatia ghururi na kujiona wao ndio wao tu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, neema za Allah ni dhihirisho la rehma na ukarimu wake, si kielelezo cha kuonyesha kwamba sisi ni wenye haki na wastahiki. Hatuna chochote sisi tunachodai kwa Allah, bali Yeye Mola anatufadhili sisi na tunapaswa kumshukuru kwa wema na uraufu wake kwetu. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kuwa na madaraka, mali, utajiri na neema zozote za kidunia, si alama ya kuonyesha kuwa waliopewa hayo wanapendwa na Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo isiwapitikie kwamba huko akhera watakuwa vivyo hivyo pia. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujihadhari pale tunapokuwa kwenye raha na uneemevu, tusighafilike tukamsahau Mola wetu na kuyapuuza maamrisho na makatazo yake. Tufikiapo hali hiyo tujue kwamba neema hizo zitageuka kuwa nakama kwetu.
Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 52 hadi 54 ambazo zinasema:
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن كَانَ مِنْ عِندِ اللَّهِ ثُمَّ كَفَرْتُم بِهِ مَنْ أَضَلُّ مِمَّنْ هُوَ فِي شِقَاقٍ بَعِيدٍ
Sema: Mnaonaje! Ikiwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi ikawa ndio mmeyakataa, ni nani aliye potea zaidi kuliko aliye katika upinzani wa mbali?
سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ۗ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ
Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?
أَلَا إِنَّهُمْ فِي مِرْيَةٍ مِّن لِّقَاءِ رَبِّهِمْ ۗ أَلَا إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ مُّحِيطٌ
Ama wao wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao Mlezi! Ama hakika Yeye amekizunguka kila kitu.
Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kuhusu watu washirikina na makafiri; na zinaanza kwa kuwahoji watu hao kwamba, hivi nyinyi hamuwezi kuchukulia kuwa yumkini ni kweli hii Qur'ani imeteremshwa na Mwenyezi Mungu, hata mnasimama dhidi yake na kuipinga? Kama imeteremshwa na Yeye Allah, na yale yaliyoelezwa ndani yake kuhusu Pepo na Moto yakawa ni kweli, mtakwenda kusema nini Siku ya Kiyama? Basi jaribuni kutafakari na acheni kufuata kibubusa na kiukereketwa mliyorithi kwa wazee wenu; na badala yake fuateni ukweli na haki. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba, ishara za kuwepo kwa Mwenyezi Mungu ni nyingi mno katika anga za mbali, kila pembe ya dunia na ndani ya nafsi za watu wenyewe. Kwa nini hamzingatii hayo ili ikubainikieni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mola wa haki? Ikiwa nyinyi mna shaka juu ya kitabu hicho cha sharia, mna shaka pia na kitabu cha ulimwengu wa maumbile, na wala hamtafakari kwamba ulimwengu huu wenye adhama lazima umetokana na Mola na Muumba mjuzi na mweza mutlaki?! Ishara za Allah katika ulimwengu, zikiwemo za uumbaji wa jua na mwezi pamoja na nyota, vinavyofuata nidhamu makini; na uumbwaji wa aina mbali mbali za viumbe wenye uhai, mimea, milima na bahari, ambavyo vyote hivyo vina maajabu yasiyohesabika, huku kila siku kukiwa kunaendelea kugunduliwa siri za kustaajabisha ndani ya vyote hivyo, kila moja kati yao ni ishara na alama ya kuwepo kwa Mola huyo pekee mwenye dhati iliyotukuka na kutakasika. Ishara za Allah SWT zipo katika nafsi ya mwanadamu, katika viungo vyake mbalimbali kama cha mfumo wa kupumulia, mfumo wa usagaji na umeng'enyaji chakula, mfumo wa mzunguko wa damu na harakati zenye nidhamu maalumu za mapigo ya moyo, mfumo na muundo wa kustaajabisha wa ubongo pamoja na viungo vyengine mbalimbali vya mwili; huku kila kimoja kikiwa ni kitabu cha elimu ya kumwezesha mtu kumjua na kumtambua Muumba wa ulimwengu. Kwa kuzingatia kuwa maneno ya aya ya 53 yasemayo "Tutawaonyesha ishara zetu", yamekuja katika muundo wa Fiilu-Mudhaari', inayoashiria hali endelevu, maana yake ni kwamba tutaonyesha ishara zetu hizo katika zama zijazo pia. Kusema kweli, kila hatua ya maendeleo atakayopiga mwanadamu katika elimu na sayansi itamfanya abainikiwe na siri za kustaajabisha zinazodhihirisha ujuzi na uwezo wa Muumba wa ulimwengu. Kwa maneno mengine ni kwamba, ugunduzi wowote ule mpya wa elimu ni dhihirisho la qudra, uwezo na hikma ya Mwenyezi Mungu na upigaji hatua kwa ajili ya kumtambua Yeye Mola. Hata hivyo kwa masikitiko, watu hao wana shaka juu ya asili ya uumbwaji wa ulimwengu na pia juu ya hatima yake na kukutana kwao na Mwenyezi Mungu Mola wao. Lakini ni wazi pia kwamba, shaka waliyonayo wao si ya hali ya kawaida ya kuweza kuondoka kwa uchunguzi na uhakiki, bali ni shaka inayotokana na dhana mbaya na kutokuwa na kiu na hamu ya kuikubali haki na ukweli. Kwa sababu wamejisahau na wameingiwa na ghururi iliyowasahaulisha kukutana na Mola wao; hawaamini kuwepo kwa hisabu na malipo ya amali zao; na kwa sababu hiyo wanafanya kila ubaya na uovu. Hata hivyo inawapasa wajue kwamba, Allah SWT amekizunguka kila kitu; na amali na matendo yao yote yako wazi katika elimu na ujuzi wake mutlaki, kwa hivyo yote wayafanyayo yanarekodiwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kwenda kuhesabiwa katika mahakama ya Siku ya Kiyama. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kwa mtu mwenye akili timamu, hata kukiwepo na uwezekano tu wa kuja kufikwa na hatari na madhara makubwa, basi huchukua hatua ya kujiweka mbali na madhara hayo hata kama hayana uhakika wa kumpata. Kwa hivyo hata uwezekano tu wa kuwepo Kiyama, inapasa umzuie na kumwepusha mtu na kufanya madhambi na maovu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ulimwengu wote wa maumbile ni darsa inayofunza somo la kumjua Mwenyezi Mungu. Kuanzia nafsi ya mwanadamu mpaka viumbe vinginevyo, ikiwemo mimea na wanyama na pia ardhi na mbingu, nyota na sayari zilizoko mbali kabisa. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, imani juu ya asili ya uumbwaji na kufufuliwa viumbe ni vitu viwili visivyotenganika, kwa sababu mwanzo wa ulimwengu na mwisho wake uko mikononi mwa Mola na Muumba pekee, Allah SWT. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 884 ya Qur'ani imefikia tamati na ndiyo inayotuhitimishia pia tarjumi na maelezo ya sura hii ya 41 ya Fuss'ilat. In shaa Allah tuwe tumeaidhika, tumeelimika na tumenufaika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../