May 24, 2023 09:22 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 885. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 41 ya Fuss'ilat, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 42 ya Ash-Shuura. Sura hii imeteremshwa Makka na ina aya 53. Jina la Suratu-Shuura limetokana na aya yake ya 38, ambapo katika aya hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu amewausia waumini wafanye mambo yao kwa kushauriana. Baada ya utangulizi huo mfupi tunaianza darsa yetu kwa aya ya kwanza hadi ya nne ya sura yetu hiyo ambayo inasema:

حم

H'a Mim.

عسق

 A'yn Sin Qaf.

كَذَٰلِكَ يُوحِي إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ اللَّهُ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na Mwenye hikima anavyo kuletea Wahyi wewe na walio kabla yako.

لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

Ni vyake vilivyomo mbinguni, na vilivyomo ardhini. Na Yeye ndiye Mtukufu, Mkuu.

Sura hii, kama zilivyo sura zingine 28 za Qur'ani, imeanza kwa herufi za mkato. Na kama tulivyowahi kueleza huko nyuma pia, katika sura hizi, baada ya herufi hizo za mkato yanafuata maelezo kuhusu Qur’ani. Ni kama kwamba Mwenyezi Mungu anataka kusema: Kitabu hiki kimepangwa na kuandikwa kwa kutumia herufi na alfabeti hizo hizo mnazotumia nyinyi; basi kama na nyinyi mnaweza, leteni kitabu kilicho mfano wake. Kwa hakika moja ya sababu zinazoifanya Qur’ani iwe muujiza, ni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ametumia herufi na maneno haya haya ya kawaida yanayoweza kutumiwa na watu wote kupanga ibara na mchanganyiko wa maneno, ambao hakuna mtu yeyote awezaye kuleta mfano wake. Katika sura hii ya Ash-Shuura, aya zinazofuatia baada ya herufi za mkato zinasema, kama tulivyokuletea wahyi wewe, tuliwashushia pia Mitume waliotangulia; na Mungu huyo huyo aliyewateremshia wahyi Mitume waliotangulia kwa ajili ya kuwafikishia watu uongofu katika zama zote za historia, ndiye aliyekuteremshia wewe pia Qur’ani. Kwa hiyo asili ya wahyi ulioteremshwa kila mahali ni moja; na maudhui kuu za wahyi katika usuli na misingi mikuu ilikuwa sawa kwa Mitume wote. Lakini kwa hikma yake Allah imepasa wahyi wenyewe uendane na hekima na ulingane na mahitaji ya mwanadamu kwa ajili ya kumjenga na kumfikisha kwenye ukamilifu. Kisha aya zinaeleza kwamba vyote vilivyoko mbinguni na ardhini ni vya Allah SWT. Ni Yeye Mola aliyeumba ulimwengu, ndiye mwenye mamlaka ya mbingu na ardhi pamoja na viumbe wote na ni Yeye pia ndiye aliyetuma Kitabu na sharia za dini kwa ajili ya kuwaongoza watu na kuendesha mambo yao. Na ndiyo kusema kuwa, chimbuko la ulimwengu wa sharia na wa maumbile ni moja na wala hakuna mgongano baina ya mawili hayo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mitume wote wanaunganishwa na asili moja na wanapokea wahyi kutoka kwenye chemchemi ya nuru moja. Kwa hivyo misingi yao ya ulinganiaji ni mimoja; na kwa mtazamo huo hakuna tofauti baina ya Mtume wa mwanzo na wa mwisho. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wahyi unatoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na hikma; na kuyatekeleza mafunzo yake hupelekea mtu kuwa imara na mwenye izza. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, chimbuko la wahyi ni elimu, ujuzi na hikma ya Allah, kwa hiyo muhtawa na yaliyomo ndani ya Quráni ni mambo madhubuti, ya kudumu na yasiyoweza kutiwa doa.  Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, mwenye ustahiki wa kupanga kanuni na sheria kwa ajili ya maisha ya mwanadamu ni Muumba wa mwanadamu mwenyewe na ulimwengu anaoishi kiumbe huyo ndani yake.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 5 na ya 6 ambazo zinasema:

تَكَادُ السَّمَاوَاتُ يَتَفَطَّرْنَ مِن فَوْقِهِنَّ ۚ وَالْمَلَائِكَةُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِمَن فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِنَّ اللَّهَ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ

Zinakaribia mbingu kupasuka juu huko, na Malaika wakimtakasa Mola wao Mlezi na kumhimidi, na wakiwaombea maghfira waliomo kwenye ardhi. Ama hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ اللَّهُ حَفِيظٌ عَلَيْهِمْ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِوَكِيلٍ

Na wale walio wafanya mawalii wengine badala yake Yeye, Mwenyezi Mungu ni Mwangalizi juu yao. Wala wewe si wakili juu yao.

Baada ya aya zilizotangulia, zilizozungumzia wahyi, aya hizi zinasema, adhama ya wahyi na maneno ya Allah SWT ni kubwa, kufikia hadi kwamba laiti maneno hayo yangeliteremshiwa mbingu, basi zingelipasuka vipande vipande, kama tunavyosoma pia katika aya ya 21 ya Suratul-Hashr ya kwamba, laiti kama Quráni ingeliteremshiwa jabali, basi lingeporomoka kwa hofu ya adhama ya Allah SWT. Kutokana na wahyi huo wanaoteremshiwa Mitume, ambao ni sababu ya kuongoka watu, Malaika huwa daima wanamhimidi na kumsabihi Mola na kumtakasa na kila ila na kasoro. Na kwa watu ambao, yumkini wakateleza na kufanya makosa, wanawaombea pia maghufira na msamaha kwa Allah. Kwa sababu wanajua kuwa Mwenyezi Mungu ni msamehevu na mrehemevu; na alivyojiwekea, ni kuwa msamehevu kwa makosa ya waja wake ili waweze kufungukiwa na njia ya kutubia na kurejea kwake. Lakini ni wazi pia kwamba, wanaopata maghufira na msamaha wa Mola ni watu wasiofanya makosa kwa makusudi na kwa uelewa; ama kwa wale wakaidi na wafanyao makosa na madhambi kwa inadi, hao hawatafunguliwa mlango wa toba. Kisha aya zinafafanua kuhusu nukta hiyo kwa kusema, kuna baadhi ya watu, badala ya kumfanya Mwenyezi Mungu na Mtume wake kuwa ndio walezi wao na hivyo kuwatii wao, wanawaendea wasiokuwa Allah na kuwapa mamlaka ya kuwatawalia mambo yao katika maisha yao. Kwa hakika watu hao wametumbukia kwenye lindi la ukafiri na shirki na wameamua kutouitika wito wa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Ni kawaida kwa Mtume kujihesabu yeye kuwa ndiye mwenye masuulia na jukumu la kuwaongoza na kuwaelekeza watu kwenye uongofu; na hupenda watu wote wafuate uongofu wa Allah; na wakati anapoona baadhi ya watu wanaipuuza na kuipa mgongo njia ya Mwenyezi Mungu husikitika na kuhuzunika. Kutokana na hali hiyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu anamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW katika aya hizi kwamba, usidhani kama wewe ni mlinzi na msimamizi wa watu na kwa hivyo wanalazimika wao kuukubali wito huo. Wewe huna dhima ya matendo yao na wala hukutumwa ukawalazimishe wafuate haki kwa nguvu. Mwenyezi Mungu amewaumba wanadamu wakiwa ni viumbe huru, aliowapa uhuru na hiari ya kuchagua njia ya kufuata. Hata hivyo kila mtu ajue kwamba atakwenda kuona matunda na matokeo ya alichochagua kufuata. Kwa sababu Allah SWT, ambaye ndiye Muumba wao, anachunga amali za waja wake wote. Na kwa hivyo yeyote atakayechagua kufuata njia ya maasi na maovu ataona matokeo ya matendo yake duniani na akhera; na yeyote atakayeamua kufuata njia sahihi ya mema na ya kheri, naye pia ataona matunda na tija ya amali zake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, nyoyo za baadhi ya watu ni ngumu zaidi kuliko mawe. Laiti kama Quráni ingeliteremshiwa mbingu, zingepasuka; lakini watu wakaidi na wenye inadi hawaathiriwi na maneno hayo ya Mwenyezi Mungu na wala hawaonyeshi unyenyekevu mbele yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tuombapo dua, tuwaombee wote walioko duniani na kuwatakia maghufira kwa Allah, kama ambavyo Malaika wanawaombea wote walioko duniani. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, kumwamini Allah hakuendani na mtu kukubali kutawaliwa mambo yake na asiyekuwa Yeye Mola. Aya hizi zinatutaka tujue pia kuwa, Mitume wametumwa kufikisha wahyi kwa watu na kuwapa mwongozo; na wala hawakuwa na jukumu la kuwalazimisha waikubali haki kwa nguvu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 885 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, atukubalie toba zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../