Sura ya Ash-Shuura, aya ya 7-10 (Darsa ya 886)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 886 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 42 ya Ash-Shuura. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 7 ya sura hiyo ambayo inasema:
وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لِّتُنذِرَ أُمَّ الْقُرَىٰ وَمَنْ حَوْلَهَا وَتُنذِرَ يَوْمَ الْجَمْعِ لَا رَيْبَ فِيهِ ۚ فَرِيقٌ فِي الْجَنَّةِ وَفَرِيقٌ فِي السَّعِيرِ
Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa Kiarabu ili uwaonye watu wa Mama wa Miji na walio pembezoni mwake. Na uhadharishe na Siku ya Mkutano, haina shaka hiyo. Kundi moja litakuwa Peponi, na kundi jengine Motoni.
Katika darsa iliyopita tulizungumzia pamoja na mambo mengine kuteremshwa wahyi kwa Mitume waliotangulia katika zama mbalimbali za historia. Aya tuliyosoma inamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba: Katika mwendelezo wa uteremshaji wa wahyi, kama ilivyokuwa kwa Mitume waliopita, tumekuteremshia na wewe pia; na Qur'ani tumeiteremsha kwa lugha ya Kiarabu, ambayo ndiyo lugha ya watu wa Makka, wahutubiwa wa mwanzo wa kitabu hiki. Madhumuni yake ni kwamba, katika hatua ya kwanza, uwape mwongozo na indhari kwa aya za kitabu hiki wakazi wa Makka na kandokando yake na kuwatahadharisha na mwisho mbaya wa matendo yao maovu ambao utawaandama Siku ya Kiyama. Kisha aya inaendelea kwa kuashiria kuwa, siku hiyo ya Kiyama, watu wote, kuanzia wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao, watakusanywa pamoja ili wahesabiwe amali zao. Huko watu watagawanyika makundi mawili: Wale waliomwamini Mwenyezi Mungu na wakafanya mema, ambao wataelekea peponi; na makazi ya waliomkufuru Mola wao na wakatenda maovu ni adhabuni kwenye Moto wa Jahannam. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, japokuwa Qur'ani imeteremshwa kwa lugha ya Kiarabu, lakini hawakukusudiwa Waarabu peke wao; na ndiyo maana hakuna mahala popote ndani ya Qur'ani lilipotumika tamko la "Yaa Ayyuha-Arab", yaani enyi Waarabu, bali limetumika tamko jumla linalowahusisha wanadamu wote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, katika tablighi na uenezi wa dini inapasa tuzingatie sifa maalumu na mahitaji ya tunaowalingania pamoja na vipaumbele vyao. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, katika sifa maalum iliyonayo Qur'ani ni ya matamko yake kubakia katika sura na hali ile ile ya wakati alipoteremshiwa Bwana Mtume SAW kwa njia ya wahyi, pasi na kubadilishwa, kupotoshwa au kutiwa mkono na wanadamu katika muda wote wa historia ya tangu kuteremshwa kwake. Halikadhalika aya hii inatuonyesha kuwa, hakuna mtu yeyote aliyeweza kutoa hoja za kimantiki kuonyesha kuwa Kiyama hakiwezi kutokea, kwa hivyo tusijitie shaka na tashwishi ya kutupatia sababu ya kufanya maovu na maasi.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 8 na ya 9 ambazo zinasema:
وَلَوْ شَاءَ اللَّهُ لَجَعَلَهُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَلَٰكِن يُدْخِلُ مَن يَشَاءُ فِي رَحْمَتِهِ ۚ وَالظَّالِمُونَ مَا لَهُم مِّن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ
Na lau Mwenyezi Mungu angeli penda ange wafanya wote umma mmoja, lakini anamwingiza katika rehema yake amtakaye. Na madhalimu hawana walii wala msaidizi.
أَمِ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۖ فَاللَّهُ هُوَ الْوَلِيُّ وَهُوَ يُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ
Au wamechukua mawalii wengine badala yake! Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Walii khasa. Na Yeye ndiye anaye huisha wafu. Na Yeye ndiye Mweza wa kila kitu.
Katika sehemu ya mwisho ya aya iliyotangulia, ilielezwa kwamba, Siku ya Kiyama, watu watagawanyika makundi mawili: Kundi moja la peponi na kundi jengine la motoni. Aya tulizosoma zinaendeleza maudhui hiyo kwa kusema, hapa duniani ni vivyo hivyo, kwani watu hawako katika hali moja. Kuna kundi la watu wenye nia safi na wanafanya matendo mema na mazuri na kuna kundi la watu wenye nia chafu wanaofanya matendo maovu na mabaya. Sasa suali linalojitokeza hapa ni, kwa nini Mwenyezi Mungu hakujaalia watu wote wakawa watenda mema hapa duniani ili wote wakaingizwe peponi Siku ya Kiyama? Aya zinatoa jibu kwa kusema: Kama Mwenyezi Mungu angelitaka, angeweza kuwalazimisha watu wote waukubali wito wa Mitume, na wakawa hawana budi kumwamini Yeye na kufanya amali njema. Lakini imani ya kulazimishwa haina thamani yoyote. Kaida na utaratibu aliouweka Allah ni wa watu kuamua kwa irada na hiari yao kuchagua njia wanayotaka kufuata na kufanya amali zao kulingana na chaguo walilofanya. Na sababu ni kwamba ukamilifu halisi wa mwanadamu unapatikana kupitia njia hiyo. Na hiyo ndiyo neema kubwa kabisa ambayo Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu; na kwa kufanya hivyo amemfungulia njia ya kuufikia ukamilifu. Kusema kweli, hii hali ya kutofautiana wanadamu, chimbuko lake ni hiyo hiari na irada ya kuamua wafanye watakavyo. Kwa maneno mengine ni kwamba, kuwepo tofauti hizo kuna maslaha zaidi kuliko wote kuwa na hali moja; kwa sababu asili ya tofauti ni hiari waliyopewa na asili ya kuwa na hali moja ni kufanya mambo kwa kulazimishwa. Hapana shaka ni bora kufanya jambo kwa hiari kuliko kwa kulazimishwa. Lakini tujue pia kwamba, kwa kuwa Allah SWT ni mwadilifu na mwenye hikma, kuamiliana kwake na waja wake kutaendana na machaguo waliyofanya. Yule aliyeamua kufuata njia ya haki kwa irada na hiari yake, atapata rehma maalum za Allah na yule aliyeamua kwa hiari yake pia kuidhulumu nafsi yake na nafsi za wenzake, atakuwa amejikosesha rehma za Mola duniani na akhera. Mtu yeyote anayekubali kutawaliwa mambo yake na asiyekuwa Allah, akaamua kuzifuata sharia pogo na zenye mapungufu za wanadamu badala ya sharia za Mwenyezi Mungu, ajue kwamba amejiweka nje ya mamlaka ya utawala wake Mola. Mtu kama huyo hana msimamizi na msaidizi duniani na akhera. Kisha aya zinaendelea kutilia mkazo suala la kukana mamlaka ya utawala wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu na kuuliza kwa mastaajabu, hivi wao wameamua kuwafanya mawalii wa kuwatawalia mambo yao wasiokuwa Mwenyezi Mungu? Ilhali ni Allah SWT ndiye walii na mtawalia halisi wa mambo ya viumbe wake! Kwa kuzingatia kwamba sharti kuu la kuwa walii na mtawaliaji wa mambo ya mtu ni kuwa na nguvu na uwezo; na muweza mutlaki wa kila jambo ni Allah SWT pekee, kwa hivyo uwalii huo unamhusu Yeye tu. Ni yeye anayewahuisha wafu na mwenye uwezo wa kila kitu. Kwa hivyo kama wanataka kujichagulia walii, msimamizi na mstahiki wa kuwatawalia mambo yao, inapasa wamchague Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye utawala wake umetanda kila mahala na wa milele pia; si mwengine ghairi yake Yeye. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mwanadamu kuwa na hiari na haki ya kuchagua, kunatokana na utaratibu usio na shaka uliowekwa na Mwenyezi Mungu; na hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya kumnyima mwanadamu haki yake hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, makafiri na washirikina, kabla ya kuitendea dhulma dini ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, huwa wamezidhulumu nafsi zao wenyewe, kwa sababu wanakuwa wamejitoa kwenye mamlaka na uwalii wa Yeye Allah SWT. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, utawala na uwalii unamstahikia mwenye uwezo wa kila jambo, ambaye mauti na uhai wa wanadamu uko mikononi mwake Yeye; si mtu ambaye hana mamlaka hata ya uhai na umauti wake mwenyewe.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 10 ambayo inasema:
وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّهِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّهُ رَبِّي عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ
Na mkikhitalifiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Huyo Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi, ninaye mtegemea na kwake Yeye narejea.
Baada ya aya iliyotangulia, iliyozungumzia uwalii mpana wa Allah kwa waja wake, aya hii inaashiria moja ya vielelezo vya uwalii wa Allah na kueleza kwamba: Mtu ambaye ameukubali uwalii na utawala wa Mwenyezi Mungu juu ya mambo yake yote, inapasa ayatangulize maneno ya Mola na hukumu yake katika kila jambo, ikiwemo pale inapotokea hitilafu na tofauti juu ya maudhui mbalimbali; na si kufuata matashi yake, ya marafiki zake, jamaa au wenye fikra sawa na zake. Kwa masikitiko ni kwamba, wengi wetu, badala ya kuzingatia ukweli na haki tunafuata hawaa na matamanio ya nafsi zetu. Kwa hivyo zinapotolewa nadharia na maoni mbalimbali kuhusu maudhui fulani katika jamii, tunayoyakubali sisi ni maoni yanayokidhi maslahi yetu binafsi au yanayoendana na itikadi na utashi wetu. Ilhali ishara ya imani ya kweli ni kwamba katika maudhui za kifikra, kijamii, kisiasa, kiuchumi na kisheria; na vile vile katika masuala mengine tunayotafautiana, turejee kwenye chemchemi ya mafundisho ya dini ya Mwenyezi Mungu. Kwa maneno mengine ni kwamba, hukumu ya kila jambo tuitafute ndani ya Qur'ani na kwenye Sunna za Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt wa mtukufu huyo, (Alayhimu-Ssalaam); na tab'an litakalotubainikia, tulikubali na kulifuata hata kama litakinzana na matashi na matakwa yetu. Ni wazi pia kwamba, kuishika na kuifuata hukumu ya Mwenyezi Mungu kuna gharama; na yumkini watu wa familia au jamii yetu wakatupinga na kutupiga vita. Kwa hivyo tunatakiwa tutawakali na kumtegemea Allah, na kumwomba auni na msaada wake atuwezeshe kuwa thabiti katika kuyakabili matatizo na misukosuko itakayotufika kwa sababu ya kushikamana na mafundisho ya dini yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, mbali ya dini kuzungumzia masuala ya kiitikadi na kiakhlaqi, inayapatia majibu pia mahitaji yote ya mwanadamu katika masuala ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kifamilia. Kwa hiyo turejee kwenye miongozo na mafundisho ya dini kwa ajili ya utatuzi wa mambo yetu yote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, badala ya kutegemea nguvu zenye mihimili dhaifu na zinazomalizika, tutawakali kwa Mwenyezi Mungu, Muweza aliyetukuka; na kumuelekea Yeye kwa shida na matatizo yote yanayotufika. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 886 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../