May 24, 2023 06:09 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 888 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 42 ya Ash-Shuura. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 15 na 16 za sura hiyo ambazo zinasema:

فَلِذَٰلِكَ فَادْعُ ۖ وَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ ۖ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَهُمْ ۖ وَقُلْ آمَنتُ بِمَا أَنزَلَ اللَّهُ مِن كِتَابٍ ۖ وَأُمِرْتُ لِأَعْدِلَ بَيْنَكُمُ ۖ اللَّهُ رَبُّنَا وَرَبُّكُمْ ۖ لَنَا أَعْمَالُنَا وَلَكُمْ أَعْمَالُكُمْ ۖ لَا حُجَّةَ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمُ ۖ اللَّهُ يَجْمَعُ بَيْنَنَا ۖ وَإِلَيْهِ الْمَصِيرُ

Basi kwa haya waite! Nawe simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wala usiyafuate matamanio yao. Na sema: Naamini aliyo teremsha Mwenyezi Mungu katika Kitabu. Na nimeamrishwa nifanye uadilifu baina yenu. Mwenyezi Mungu ni Mola wetu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Sisi tuna jukumu kwa vitendo vyetu, na nyinyi mna jukumu kwa vitendo vyenu. Hapana kuhojiana baina yetu na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu atatukusanya pamoja, na marejeo ni kwake. 

وَالَّذِينَ يُحَاجُّونَ فِي اللَّهِ مِن بَعْدِ مَا اسْتُجِيبَ لَهُ حُجَّتُهُمْ دَاحِضَةٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ وَلَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ

Na wanao hojiana juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kukubaliwa, hoja za hawa ni baat'ili mbele ya Mola wao Mlezi, na juu yao ipo ghadhabu, na itakuwa kwao adhabu kali.

Katika darsa iliyopita tulieleza kwamba dini zote za mbinguni zina chimbuko na asili moja. Aya hizi tulizosoma zinamhutubu Bwana Mtume SAW ya kwamba: walinganie watu wote, iwe ni washirikina au Ahlul Kitab na kuwaita kwenye dini uliyofunuliwa wewe, kwa sababu ndiyo iliyokuja na sharia za mwisho za Mwenyezi Mungu. Wafikishie watu yote uliyoteremshiwa kwa njia ya wahyi bila kuongeza wala kupunguza chochote, simama imara na kuwa thabiti katika njia hii, wala usikhini katika kutekeleza wajibu wako kwa ajili ya kuwaridhisha wao. Kila kundi linajaribu kukuvuta ili ukidhi matashi na maslahi yao binafsi; lakini wewe usifuate hawaa na matamanio ya nafsi zao, bali waunganishe wote kwenye dini moja ya Mola wako. Waambie Ahlul Kitab, wakiwemo Mayahudi na Manasara ya kwamba: mimi ninaamini kitabu chochote kilichoteremshwa na Mwenyezi Mungu. Mimi ninawakubali Mitume wenu na vitabu vyenu mlivyoteremshiwa; na ujumbe wangu unaendeleza ujumbe waliokuja nao wao. Na dini niliyokuja nayo imejumuisha na kukamilisha yote waliyoyaleta wao. Kama Mitume waliotangulia, ambao waliamriwa kutekeleza uadilifu katika jamii; na wao wenyewe kufanya mambo yao kwa uadilifu, na mimi pia nimekuja na ujumbe unaoniagiza kutekeleza uadilifu baina yenu. Mola Mlezi wangu mimi na wenu nyinyi ni mmoja. Mimi nimekubainishieni hoja za ukweli wa Utume wangu. Amali zetu zinatuhusu sisi wenyewe, na amali zenu zinakuhusuni nyinyi wenyewe pia; na kila mmoja, baina ya sisi na nyinyi atawajibika kwa amali zake. Kwa hiyo nimesha timiza dhima yangu kwenu; hakuna haja ya kubishana na kulumbana, wala hakuna hasama ya binafsi kati ya sisi na nyinyi. Mwenyezi Mungu atatukusanya sisi na nyinyi Siku ya Kiyama; na hakimu atakayetuhukumu sisi sote siku hiyo atakuwa ni Yeye tu. Basi tusubirini, tuone wakati tutakapohudhurishwa mbele yake, Allah atatuhukumuje sisi na nyinyi siku hiyo? Kisha aya zinaendelea kwa kueleza kwamba, pamoja na hayo, wao wanaendeleza mabishano na uadui na kutaka kuidhoofisha dini ya Uislamu. Sababu ni kwamba, kuna watu wamesilimu na kuifuata dini hii na kuna wengine wataingia pia katika siku za usoni. Washirikina, ambao baada ya kubainika haki wanaendelea kungángánia kufuata itikadi zao batili kwa sababu ya uadui na ukaidi na kuamua kuhoji juu ya Mwenyezi Mungu, hawafanyi hivyo kwa kutegemea hoja na mantiki. Wao wanatoa hoja za kukataa kusilimu na kuufuata Uislamu, hoja ambazo ni batili na hazina msingi wowote mbele ya Allah. Kufanya hivyo kunawafanya waghadhibikiwe na Mwenyezi Mungu na kufikwa na adhabu kali. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tusikasiri na kuzembea kutekeleza maamrisho ya dini kwa sababu ya kuwaridhisha watu, bali tusimame imara na kubaki thabiti katika kushikamana na misingi ya wito wa haki tunaofuata. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuonyesha istiqama katika imani na itikadi huwa na thamani, ikiwa ni kwa msingi wa kushikamana na haki, vyenginevyo, kuwa na ukereketwa, ukaidi na taasubi juu ya mambo ya batili hakuna maana yoyote. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, kusimamisha uadilifu katika jamii ni miongoni mwa malengo ya dini zote za mbinguni. Ni wazi kwamba utekelezaji wake hauyumkiniki bila ya kuwa na mamlaka na hatamu za utawala. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, midahalo, mazungumzo na majadiliano huwa na mantiki na kukubalika kuyafanya ili haki iweze kubainika. Baada ya kubainika ukweli na haki, tusiendeleze tena majadiliano bali tumwache mtu aamue kufuata atakavyo.

Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 17 na 18 ambazo zinasema:

اللَّهُ الَّذِي أَنزَلَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ وَالْمِيزَانَ ۗ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ قَرِيبٌ

Mwenyezi Mungu ndiye aliye teremsha Kitabu kwa Haki, na Mizani. Na nini kitakujuulisha, pengine Saa ya Kiyama ipo karibu.

يَسْتَعْجِلُ بِهَا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِهَا ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا مُشْفِقُونَ مِنْهَا وَيَعْلَمُونَ أَنَّهَا الْحَقُّ ۗ أَلَا إِنَّ الَّذِينَ يُمَارُونَ فِي السَّاعَةِ لَفِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ

Wasio amini huihimiza hiyo Saa ifike upesi; lakini wanao amini wanaiogopa, na wanajua kwamba hakika hiyo ni kweli. Ama kwa hakika hao wanao bishana katika khabari za hiyo Saa wamo katika upotofu wa mbali kabisa.

Baada ya tuliyoyasikia katika aya zilizotangulia, ambapo Bwana Mtume Muhammad SAW aliwatambulisha washirikina na Ahlul Kitab dini ya Allah aliyokuja nayo, aya hizi zinasema: Mwenyezi Mungu tunayemwamini sisi ni Mungu ambaye ameteremsha kitabu cha mbinguni kwa ajili ya kuwaongoza watu kuelekea uongofu na kubainisha ndani ya kitabu hicho mizani na kipimo cha kupambanua kati ya haki na batili. Hiyo ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, wanadamu hawazipambanui haki na batili kwa kufuata hawaa na matamanio ya nafsi zao, na kuyafanya hayo kuwa ndio kipimo cha kutumia kufanyia mambo yao. Kimsingi hasa ni kwamba Allah SWT ni haki, na kila kitokanacho na Yeye ni haki; na kwa hivyo halipatikani lolote la batili kwake Yeye; si katika kauli wala kitendo. Kadhalika mfumo wa maumbile aliouumba, nao pia umesimama kwa msingi wa haki na uadilifu. Wa aidha mfumo wa sheria aliouleta kwa njia ya wahyi kwa wanadamu kupitia Mitume wake, nao pia umesimama juu ya ukweli na haki, ili kuwabainishia watu baadhi ya hakika na ukweli ambao hawana uwezo wa kuuelewa kwa kutegemea njia tano za hisi au elimu na taaluma zipatikanazo kwa njia za kawaida. Moja ya hakika muhimu, ambayo ina nafasi muhimu sana katika maisha ya mwanadamu, na ambayo Quráni imeibainisha kwa uwazi kabisa, ni kuwepo kwa Kiyama. Kwa sababu, Siku ya Kiyama haki na uadilifu vitadhihiri na kubainika kwa ukamilifu. Na kwa sababu hiyo, ili kumtanabahisha mwanadamu kuhusu Kiyama na kumtahadharisha na hatari zake, Quráni tukufu inasema: si hasha kufufuliwa kwa watu kukawa kuko karibu! Hata hivyo kwa masikitiko, baadhi ya watu ambao walikuwa hawaamini Kiyama, ilhali hawakuwa na hoja na burhani ya kuthibitisha kuwa hakiyumkiniki kuwepo, walikuwa wakiifanyia istihzai imani hiyo na wakawa wanamwambia Bwana Mtume kwa kejeli kwamba: kama usemayo ni kweli, kiharakishe hicho Kiyama, ili wewe uende zako Peponi na sisi tukaselelee Motoni! Pamoja na hayo imani juu ya Kiyama na kuhudhurishwa mbele ya mahakama ya uadilifu ya Allah ina taathira kubwa sana kwa waumini. Kwa sababu ya khofu ya siku hiyo, wao huwa muda wote wanajichunga katika mwenendo na matendo yao, kwa sababu wanajua kwamba Kiyama ni haki. Kwa mtazamo wao wao, dunia hii ni utangulizi wa kuelekea kwenye dunia na ulimwengu mwingine; na bila kuwepo ulimwengu huo, uumbwaji wa dunia hii utakuwa ni upuuzi na usio na maana yoyote, jambo ambalo haliendani katu na hikma ya Mwenyezi Mungu na uadilifu wake! Hapana shaka, saa na lahadha ya kutokea Kiyama imefichika kwa wanadamu wote. Hata Mitume wa Allah, nao pia hawana ilimu na ujuzi wa hilo. Lakini kutokuwa na ujuzi wa wakati halisi wa kutokea jambo si hoja ya kuthibitisha kuwa halitatokea. Na kimsingi hasa ni kwamba, huko kutojua, ndiko kunakomfanya mwanadamu ahisi, yamkini likatokea muda wowote na hivyo kumfanya ajihadhari na kujiweka mbali na maovu na maasi. Lakini watu ambao hawataki kuamini Kiyama, wao huwa kila siku wanazusha shubha na vijisababu ili kuwababaisha na kuwatia shaka wenzao pia juu ya hakika hiyo. Watu hao kwa kweli wanajidhuru na kuzikhasirisha zaidi nafsi zao wenyewe. Ni kama isemavyo Quráni ya kwamba, watu wanaotia shaka kuhusu Kiyama na kubishana juu yake kwa inadi na ukaidi wako kwenye dhalala na upotofu mkubwa. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, Qur’ani ndicho kipimo na kigezo cha kupambanua kati ya haki na batili, kwa sababu inatoka kwa Mwenyezi Mungu na haina lolote lile la batili ndani yake. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa, hakuna mtu yeyote ajuaye saa na wakati wa Kiyama, siku ambayo amali na matendo ya waja yatahesabiwa; na yamkini kujiri kwake kukathibiti wakati wowote ule. Kwa hiyo, tusitekwe na kughilibiwa na matamanio ya kipuuzi, kwani si hasha Kiyama kikawa kiko karibu mno. Aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, moja ya alama za kuwa na imani ya kweli, ni mtu kuchunga kauli na matendo yake, kwa sababu mtu muumini huwa muda wote anachelea kusimamishwa na kusailiwa katika mahakama ya Siku ya Kiyama. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa, moja ya mbinu za wapinzani wa haki ni kuwatia shaka waumini kwa kuibua hoja na masuali yenye shubha na utata. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 888 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/