Sura ya Ash-Shuura, aya ya 19-23 (Darsa ya 889)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 889 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 42 ya Ash-Shuura. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 19 na 20 za sura hiyo ambazo zinasema:
اللَّهُ لَطِيفٌ بِعِبَادِهِ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ ۖ وَهُوَ الْقَوِيُّ الْعَزِيزُ
Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake. Humruzuku amtakaye. Naye ni Mwenye nguvu, Mtukufu.
مَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الْآخِرَةِ نَزِدْ لَهُ فِي حَرْثِهِ ۖ وَمَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِن نَّصِيبٍ
Mwenye kutaka mavuno ya Akhera tutamzidishia katika mavuno yake, na mwenye kutaka mavuno ya duniani tutampa katika hayo, lakini katika Akhera hana fungu.
Katika darsa iliyopita tulizungumzia adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa wakanushaji wa Kiyama. Aya hizi zinasema: Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mpole kwa waja wake wote na anatoa riziki kwao wote, wakiwemo hata wanaomkufuru na wasiomwamini. Tab’an utoaji riziki wa Allah unaendana na hikma yake; na kote kuwili, duniani na akhera kunafanyika kulingana na taratibu alizoweka Yeye Mola. Na utaratibu wenyewe ni kwamba, kila mja atakayejipinda kwa ajili ya akhera, atapata faida ya juhudi zake hapa duniani; na huko akhera pia ataneemeka kwa fadhila za Allah SWT. Lakini mtu asiyeamini kwamba Kiyama kipo; na malengo yake yote yakawa ni kwa ajili ya maisha ya dunia tu, basi katika umri huu mfupi na wenye kikomo wa dunia hataweza kufikia malengo yake yote hayo; na huko akhera hatofaidika na chochote. Qur’ani imetumia tashbihi ya kuvutia ya kuwafananisha walimwengu na wakulima, ambapo kundi moja miongoni mwao wanalima kwa ajili ya akhera na kundi jengine kwa ajili ya dunia na kueleza kwamba, yule anayelima kwa ajili ya akhera tunamtilia baraka na kumzidishia mazao yake; lakini yule alimaye kwa ajili ya dunia tu na hima na bidii yake yote ni kwa ajili ya kufaidika na mazao hayo yamalizikayo na ya kupita, yeye tutampa machache tu katika anayopigania; na huko akhera hatopata fungu lolote. Kwa maelezo hayo tunaweza kusema, dunia hii ni shamba letu sisi waja, na amali tuzifanyazo ndizo mbegu zake. Tab’an mbegu hizo zinatofautiana. Baadhi yao mazao yake hayana mpaka, yana faida isiyo na kikomo na ya milele; lakini baadhi ya mbegu hizo, mazao yake ni machache mno na matunda yake ni makali na ya kukirihisha. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, wema na ukarimu wa Allah SWT unajumuisha waja wake wote; na muumini na kafiri, wote wanafaidika na neema zake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tunatakiwa tulinganishe na kisha ndipo tuchague. Wanaopigania akhera, wananeemeka na dunia pia, hata kama yamkini neema hizo zitakuwa chache na zenye mpaka, lakini wanaopaparikia dunia pekee, hawatafaidika na chochote cha akhera. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, nia na lengo ni muhimu, si dhahiri tu ya tendo; yamkini dhahiri ya matendo ikafanana, lakini yakawa yamefanywa kwa nia na malengo tofauti. Tab’an lile lifanywalo kwa ajili ya Allah, hustawi na kubarikiwa.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 21 na 22 ambazo zinasema:
أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّهُ ۚ وَلَوْلَا كَلِمَةُ الْفَصْلِ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۗ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ
Au hao wana miungu ya kishirikina walio watungia dini asiyo itolea idhini Mwenyezi Mungu? Na lau lisinge kuwako neno la kupambanua basi wangeli katiwa hukumu baina yao. Na hakika wenye kudhulumu watapata adhabu chungu.
تَرَى الظَّالِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا كَسَبُوا وَهُوَ وَاقِعٌ بِهِمْ ۗ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فِي رَوْضَاتِ الْجَنَّاتِ ۖ لَهُم مَّا يَشَاءُونَ عِندَ رَبِّهِمْ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ
Utawaona hao madhaalimu wanavyo kuwa na khofu kwa sababu ya waliyo yachuma, nayo yatawafika tu. Na walio amini na wakatenda mema watakuwamo katika mabustani ya Peponi. Humo watapata wayatakayo kwa Mola wao Mlezi. Hiyo ndiyo fadhila kubwa.
Aya hizi zinawazungumzia washirikina na kuhoji: je ghairi ya Mungu Mmoja wa haki, wao wanaye muabudiwa mwingine ambaye naye pia ameteremsha kitabu na kuleta sheria na dini ambayo wao wanaifuata? Ukweli ni kwamba anayestahiki kuweka sheria ni Mwenyezi Mungu, ambaye ni Muumba na Mwenye kuitawala na kuiendesha dunia; na ghairi ya Yeye hakuna yeyote mwenye haki ya kutunga sheria. Katika dunia ya leo pia, sheria zozote zinazotungwa kitaifa au kimataifa, kama zitapingana na sheria za Mwenyezi Mungu ni batili na si za kudumu. Kimsingi hasa ni kwamba utungaji sheria za aina hiyo ni kuwatendea dhulma wanadamu. Kwa sababu kufanya hivyo ni kumuondoa mwanadamu kwenye hifadhi ya Allah na kumkabidhi kwa watu ambao, mbali na kutokuwa na uelewa wa lenye kheri na maslaha na kiumbe huyo, wao wenyewe hawawezi kutunga kanuni na sheria pasi na kuzingatia maslahi yao ya kimaada. Tab’an Mwenyezi Mungu anatoa muhula kwa watu hapa duniani ili wajichagulie kwa hiari yao njia ya kufuata. Lakini chochote kile watakachofanya watambue kuwa, matokeo yake yatakwenda kudhihiri huko akhera. Kufuru na dhulma zitawasukumiza watu motoni, lakini imani na amali njema zitawaongoza waja kuelekea kwenye mabustani ya kuvutia na kupendeza kabisa ya peponi. Hapana shaka, fadhila za Allah kwa waumini hazitamalizikia hapa duniani. Watapata rehma na fadhila za Mola kwa kuruzukiwa kila zitakachotamani nafsi zao. Malipo yao hayatakuwa na kikomo na tab’an lililo kubwa na bora zaidi ya atiya zote hizo ni kufikia daraja ya kukurubishwa kwa Mola Aliyetukuka. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, maisha ya mwanadamu yanahitaji kanuni na sheria; lakini kama tutachukua na kufuata sheria hizo kwa yeyote asiyekuwa Allah tutakuwa tumejidhulumu sisi wenyewe na jamii yote ya wanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, khurafa, uzushi na bidaa ya aina yoyote ile itakayofanywa kwa jina la dini ni aina mojawapo ya shirki na dhulma. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, khofu ya adhabu ya Mwenyezi Mungu inapasa imfanye mtu ajidhibiti na kujiepusha kufanya madhambi na maasi katika dunia hii; vyenginevyo, kwenda kuikhofu adhabu huko akhera hakutakuwa na manufaa yoyote kwa waovu. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, sharti la kuyashika barabara maamrisho ya dini ni kustahamili na kuwa tayari kujinyima na kuridhia mipaka tuliyowekewa kwa baadhi ya mambo. Subira yetu ya kujikhini mambo hayo itakwenda kufidiwa huko akhera, kwa waumini kukuta wameandaliwa huko peponi kila watakachotaka na kutamani.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 23 ambayo inasema:
ذَٰلِكَ الَّذِي يُبَشِّرُ اللَّهُ عِبَادَهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ ۗ قُل لَّا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا إِلَّا الْمَوَدَّةَ فِي الْقُرْبَىٰ ۗ وَمَن يَقْتَرِفْ حَسَنَةً نَّزِدْ لَهُ فِيهَا حُسْنًا ۚ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ شَكُورٌ
Hayo ndiyo aliyo wabashiria Mwenyezi Mungu waja wake walio amini na wakatenda mema. Sema: Kwa haya sikuombeni malipo yoyote isipokuwa mapenzi katika ndugu. Na anaye fanya wema tutamzidishia wema. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira Mwingi wa shukrani.
Aya hii kwanza inatilia mkazo nukta ya kwamba, kama waumini wamevumilia tabu na misukosuko hapa duniani kwa ajili ya kulinda imani zao, Mwenyezi Mungu anawapa bishara kuwa atawafidia kwa hilo Pepo na malipo makubwa kabisa. Kisha aya inamtaka Bwana Mtume SAW awatangazie waumini kwamba, mimi pia, kama walivyokuwa Mitume walionitangulia, sitaki malipo wala ujira wowote kutoka kwenu kwa kutekeleza jukumu la kufikisha wito wa Mwenyezi Mungu, isipokuwa muwapende jamaa zangu wa karibu. Nilichofanya mimi ni kutekeleza jukumu nililopewa na Allah SWT. Lakini dira ya kufuata nyinyi baada yangu ni kuwapenda Ahlul Bayt zangu, kuwafanya ndio ruwaza na kigezo cha kufuata katika maisha yenu na mufuate watakayokuambieni katika kubaini haki na batili. Kisha aya inaendelea kusisitiza kwamba, waumini wafanye mambo mema na ya kheri kwa wanadamu wenzao ili wapate rehma na fadhila za Allah; na Yeye Mola atawazidishia mema yao na kuwasamehe makosa yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Mitume hawataki malipo ya kimaada, bali wanachotaka ni kutiiwa maamrisho ya Allah; na waumini kuwafuata makhalifa wema wa wajumbe hao wa Mwenyezi Mungu; ambapo faida ya kufanya hivyo huwarudia watu wenyewe, si Mwenyezi Mungu wala Mtume wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, imani huwa imekamilika kwa waumini kuwapenda Ahlul Bayt wa Bwana Mtume SAW. Mapenzi hayo tab'an inapasa yafungamane na masharti mawili. La kwanza ni kuwajua Ahlul Bayt wenyewe, kwa sababu bila kumjua mtu, kumpenda kwako hakutakuwa na maana. Na sharti la pili ni kuwafuata na kuwatii. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, rehma na maghufira ya Mwenyezi Mungu yanapatikana kwa kuwatendea wema waja wake na kufanya mambo mema na yanayompendeza Yeye Mola. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 889 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe maarifa ya kuwajua Ahlul Bayt wa Bwana Mtume SAW na kufuata miongozo na mafundisho yao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/