May 24, 2023 06:33 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 891 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 42 ya Ash-Shuura. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 29 ya sura hiyo ambayo inasema:

وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَثَّ فِيهِمَا مِن دَابَّةٍ ۚ وَهُوَ عَلَىٰ جَمْعِهِمْ إِذَا يَشَاءُ قَدِيرٌ

Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na wanyama alio waeneza humo. Naye ni Mwenye uweza wa kuwakusanya apendapo.

Katika darsa iliyopita tulizungumzia neema ya kunyesha mvua ambayo ndicho chanzo cha uhai wa ardhi na ishara ya rehma za Allah SWT. Aya hii tuliyosoma inasema, uumbaji wa mbingu na ardhi na kuenezwa ndani yake anuai za viumbe hai wadogo na wakubwa ni ishara bora ya kuonyesha ujuzi na uwezo wa Mola Muumba. Mbingu yenye mfumo adhimu wa sayari, unaojumuisha ndani yake mabilioni ya nyota, ambao humshangaza na kumstaajabisha mwanadamu anapoutalii na kuutafakari; na ardhi iliyoshamiri anuai za mimea na miti ya rangi tofauti pamoja na vivutio vyake vingi vingine, yote hayo ni aya na ishara za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Lakini pia viumbe hai wa mbinguni na ardhini, aina mbalimbali za ndege, aina tofauti za wanyama, wakiwemo wanyama mwitu na wa kufuga pamoja na samaki namna kwa namna kuanzia vidagaa vidogovidogo kabisa mpaka papa na manyangumi yenye maumbo makubwa pamoja na mambo ya ajabu na ya kustaajabisha yanayoshuhudiwa katika uumbaji wa kila kimoja katika vitu hivyo, yote hayo ni katika aya na ishara za Allah SWT. Ni wazi kwamba, aliyeumba mfumo wenye adhama kubwa kabisa kama huu, ni mweza pia wa kukisimamisha Kiyama na kuweza kuwakusanya huko wowote wale awatakao katika viumbe hao. Kuna nukta mbili hapa zenye kutoa mguso katika aya hii: ya kwanza ni kwamba inatoa habari ya kuwepo viumbe hai katika sayari za angani, mbali na sayari hii ya dunia; na nukta ya pili inahusu kukusanywa viumbe vingine vyenye uhai Siku ya Kiyama. Kufufuliwa na kukusanywa huko kunaweza kukawa kwa ajili ya malengo mawili: La kwanza ni kulipwa thawabu na adhabu, tab’an kama tutawachukulia viumbe hao kuwa nao pia wana aina fulani ya hisia na uelewa; na lengo jengine, ni kwa kuwa kwao viumbe ambao huko akhera pia watakuwa na uhai, lakini licha ya kuwa na hisia, havitalipwa thawabu au malipo ya adhabu. Sababu ni kuwa katika aya tofauti, Qur’ani imezungumzia kufufuliwa na kukusanywa viumbe vitembeavyo, pasi na kuelezea malipo ya thawabu au adhabu watakayolipwa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuwepo asili ya uumbwaji wa viumbe ni ishara ya uwezekano wa kuumbwa tena Siku ya Kiyama. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, viumbe hai si wale tuwajuao sisi tu hapa ardhini; kwani huko angani na mbinguni pia wako viumbe hai. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, kuenea au kukusanywa viumbe kunafuata irada ya Allah SWT; na mwanadamu hana nafasi yoyote katika jambo hilo.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 30 na 31 ambazo zinasema:

وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ

Na misiba inayo kusibuni ni kwa sababu ya yaliyotendwa na mikono yenu. Naye anasamehe mengi. 

‏ وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ ۖ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ

Na nyinyi hamwezi kushinda katika ardhi. Na wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi badala ya Mwenyezi Mungu.

Baada ya aya iliyotangulia kuashiria kukusanywa viumbe Siku ya Kiyama, aya hizi zinasema: Bila shaka, hiyo haimaanishi kwamba hapa duniani hakutakuwepo na malipo ya thawabu na adhabu; na kwamba kwa lolote watakalofanya watu, hawatafikwa na adhabu yoyote ile. Ukweli ni kwamba, mengi ayafanyayo mwanadamu kwa chaguo na hiari yake, yana athari za lazima ambazo zitampata papa hapa duniani kwa kuonja uchungu wa mabaya anayoyafanya. Na hiyo ndio adhabu ya Mola ya hapa duniani inayoendana na kanuni za kimaumbile alizoziweka. Hii inamaanisha kwamba, mbali na adhabu za akhera, matendo ya watu yana athari za kidunia na kimaada pia zinazojionyesha hapa hapa ulimwenguni. Ni kama inavyoeleza aya ya 41 ya Suratu-Rum ya kwamba: “Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu.” Sehemu inayofuatia ya aya inaeleza kwamba, baadhi ya watu wanadhani, wanaweza kuyaepuka matokeo na athari za matendo wayafanyayo hapa duniani, wakakanyaga na kukiuka kanuni na taratibu alizoweka Allah na kufanya lolote lile watakalo bila ya kupatwa na masaibu yoyote. Ilhali popote pale wawapo, kama watakimbilia angani au kubaki ardhini, kanuni na taratibu za Allah zinatawala kote huko na hakuna yeyote ghairi ya Yeye Mola anayeumiliki na kuutawala ulimwengu wote huu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, matukio mengi machungu yanayomfika mtu katika maisha yake ni matokeo ya moja kwa moja na yasiyoepukika ya mwenendo na matendo yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, matatizo ya mtu ni sehemu tu matokeo ya makosa anayoyafanya. Kwa sababu msamaha na usamehevu wa Allah ndio unaomfanya mtu anusurike na matokeo mabaya ya matendo mengi maovu ayatendayo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mwanadamu ni dhaifu mno wa kuweza na uwezo wowote ule wa kukabiliana na nguvu za Allah SWT; na hana popote pa kukimbilia ili kujivua na utawala wa Mola Muumba.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya 32 hadi 35 za sura yetu hii ya Ash-Shuraa ambazo zinasema:

وَمِنْ آيَاتِهِ الْجَوَارِ فِي الْبَحْرِ كَالْأَعْلَامِ

Na katika Ishara zake ni vyombo vinavyo kwenda na kurejea baharini kama vilima.

إِن يَشَأْ يُسْكِنِ الرِّيحَ فَيَظْلَلْنَ رَوَاكِدَ عَلَىٰ ظَهْرِهِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ

Akitaka, huutuliza upepo navyo hivyo vyombo husimama tutwe juu ya bahari. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.

أَوْ يُوبِقْهُنَّ بِمَا كَسَبُوا وَيَعْفُ عَن كَثِيرٍ

Au huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyo yatenda hao watu. Naye husamehe mengi. 

وَيَعْلَمَ الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِنَا مَا لَهُم مِّن مَّحِيصٍ

Na ili wajue wanao jadiliana katika Ishara zetu kwamba hawana pahala pa kukimbilia. 

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kuhusu baadhi ya ishara za ujuzi, uwezo na rehma za Allah SWT ikiwemo ya mvua, kwa kuashiria nafasi ya upepo katika maisha ya wanadamu na kueleza kwamba: merikebu na mameli makubwa yabebayo mizigo au abiria, ambayo hukata mawimbi katika maji ya bahari pasi na kuzama ndani ya maji hayo, ni ishara mojawapo ya uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu; kwa sababu Yeye Mola ameyapa maji sifa hiyo maalumu inayozifanya meli zielee na kupasua mawimbi juu yake bila kuzama. Aidha mwendo wa merikebu juu ya maji utokanao na pepo zivumazo na kuyasukuma matanga, nao pia ni miongoni mwa rehma za Allah SWT. Bila shaka leo hii kuna mameli makubwa makubwa ambayo kwa kutumia mainjini yenye nguvu kubwa, yana uwezo wa kukata masafa kwenye bahari kuu na kusafirisha idadi kubwa ya shehena za mizigo na abiria. Lakini meli hizo pia zinaweza kuyafanya hayo kwa kufuata kanuni zinazotawala mfumo wa maumbile alizoweka Mwenyezi Mungu, ambazo zimegunduliwa na mwanadamu na kuziwezesha kukata mawimbi; na si kwamba yeye mwanadamu ndiye aliyepanga kanuni kwa ajili ya maumbile na adai kusema: Haya nimeyafanya mimi! Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Kama Mwenyezi Mungu atataka, ataufanya upepo usiwe na harakati, na hivyo merikebu zitabaki zimesimama na kutulia tuli baharini. Na katika hilo, kuna ishara kwa kila mwenye sifa ya kweli ya subira na ushukurivu. Alaa kulli haal, kutulia tuli au kukata mawimbi meli ndogondogo na kubwa na kufika salama usalimini kokote zinakoelekea, yote hayo yako mikononi mwa Allah SWT. Kwa sababu ikiwa Yeye Mola atataka, atazigharikisha meli na walioabiri ndani yake; na hilo tab'an hutokea zaidi kama adhabu ya matendo waliyofanya watu wenyewe. Ukweli ni kwamba Allah SWT anayafumbia macho madhambi mengi wayafanyayo wanadamu na kuamua kutowaadhibu; kwani kama ingekuwa wanadamu waadhibiwe kwa kila maovu wayafanyayo, asingesalia mtu yeyote juu ya mgongo wa ardhi. Pamoja na yote hayo, bila shaka watu wakaidi na wenye inadi hawako tayari kuukubali uwezo wa Mwenyezi Mungu katika mfumo wa maumbile na daima huzikanusha ishara za Mola katika ardhi na kuamua kupingana na kubishana na walioamini. Lakini wao pia watakuja kuelewa kwamba hawana pa kukimbilia na kuweza kuukwepa uwezo na mamlaka ya Allah SWT. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, si uumbaji wa viumbe pekee, bali hata kanuni zinazotawala juu ya vitu visivyo na uhai na vya hali ya umajimaji, vyote hivyo ni ishara za uwezo na rehma za Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambapo moja ya rehma na uwezo huo ni kukata mawimbi majini vitu vizito na vyenye maumbo makubwa kama meli. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wakati zinapotujia neema za Mwenyezi Mungu, inatakiwa tuwe na subira na pia tuwe washukurivu. Baadhi ya wakati, kwa hikma ya Mola, ujio huo huandamana na tabu na misukosuko, hivyo inatupasa tuwe wavumilivu; na wakati mwingine huandamana na raha na uneemevu, na kwa hiyo tunatakiwa tuwe washukurivu. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, matendo yetu sisi wanadamu, siku zote hutusababishia hatari ya kufikwa na maangamizi. Kwa hivyo tunaponusurika na hilo, tujue kwamba nusra hiyo inatokana na rehma za Mwenyezi Mungu. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa, tusiuhakiki na kuutafsiri mfumo wa maumbile kwa jicho la kimaada tu, bali tuzingatie pia nafasi ya Mwenyezi Mungu katika uratibu na uendeshaji wa masuala ya ulimwengu. Kwa sababu tusipofanya hivyo tutakuwa tumepuuza ujuzi, uwezo na hikma ya Allah SWT katika undeshaji wa mambo ya ulimwengu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 891 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wavumilivu anapotutahini na pia kuwa washukurivu anapotuneemesha kwa neema zake zisizohesabika. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/