Sura ya Ash-Shuura, aya ya 44-47 (Darsa ya 894)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 894 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 42 ya Ash-Shuura. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 44 ya sura hiyo ambayo inasema:
وَمَن يُضْلِلِ اللَّهُ فَمَا لَهُ مِن وَلِيٍّ مِّن بَعْدِهِ ۗ وَتَرَى الظَّالِمِينَ لَمَّا رَأَوُا الْعَذَابَ يَقُولُونَ هَلْ إِلَىٰ مَرَدٍّ مِّن سَبِيلٍ
Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana walii baada yake. Na utawaona madhalimu watakapo iona adhabu wanasema: Je! Ipo njia ya kurudi?
Moja ya kaida na utaratibu aliojiwekea Allah, ni kuwaonyesha waja wake uongofu kwa njia ya wahyi na kupitia akili zao wenyewe, ili waweze kubaini njia ipi ya sawa na ipi ya upotofu na kutokuja baadaye kutoa udhuru kwamba hawakuitambua njia ya haki iliyonyooka na hawakujua kama wanayoyafanya si sahihi. Lakini watu walioifahamu njia ya uongofu na wakaamua kuikengeuka, hao watakuwa wamekhitari na kuamua kwa hiari yao wenyewe kuufuata upotofu. Na upotofu huo ni adhabu inayojiakisi kimaumbile na taratibu ndani ya nafsi zao kwa kuwafanya wadhani yale maovu wayafanyayo ni mazuri. Ni wazi kwamba si uongofu wala upotofu unaotokea bila ya khiyari ya mtu, bali ni matunda na matokeo ya amali za mtu mwenyewe. Kuna wakati mtu hufanya maovu na mabaya yanayomfanya afutiwe na Allah nuru ya uongofu ndani ya moyo wake na kumwacha atopee kwenye giza la dhalala na upotofu. Kwa kweli kutokana na tabia na matendo yake maovu, mtu kama huyo huwa amejiandalia mwenyewe mazingira ya kuharibika na kupotoka. Na tab'an, wakati hakika za matendo yote ya wanadamu itakapodhihirika Siku ya Kiyama, waovu watatambua makosa yao na watajuta kwa madhambi waliyofanya. Lakini majuto ya wakati huo hayatokuwa na faida yoyote, na ombi la madhalimu la kutaka warejeshwe tena duniani, litakataliwa, kwa sababu haitakuwepo tena njia ya kurudi ulimwenguni. Kama ambavyo mtu mzee hawezi kurudi kwenye ujana, kijana hawezi kurudi utotoni na mtoto naye hawezi kurudi uchangani na katika hali ya jenini tumboni mwa mama yake, ndivyo vivyo hivyo ilivyo muhali kwa mwanadamu kutoka ulimwengu wa akhera, akarudi tena duniani. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, hakuna upotokaji wa asili, kwa maana kwamba, Mwenyezi Mungu haanzi tu kumpotosha mtu, bali kuna upotokaji wa adhabu; kwa maana kwamba, kutokana na athari za dhulma, ukafiri na ufisadi, ndipo mtu hufungiwa njia ya kuitambua haki na ukweli na kuangukia kwenye shimo la dhalala na upotofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, madhalimu na wapotofu wajue kwamba hakuna mtu awezaye kukabiliana na irada ya Mwenyezi Mungu; kwa hivyo hatatokea mtu yeyote wala nguvu yoyote ya kuweza kuwaokoa wao. Kama ni hivyo tutawakali na kumuelekea Yeye Mola peke yake.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 45 na 46 ambazo zinasema:
وَتَرَاهُمْ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا خَاشِعِينَ مِنَ الذُّلِّ يَنظُرُونَ مِن طَرْفٍ خَفِيٍّ ۗ وَقَالَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا إِنَّ الظَّالِمِينَ فِي عَذَابٍ مُّقِيمٍ
Na utawaona wanapelekwa kwenye Moto, nao wamenyenyekea kwa unyonge, wanatazama kwa mtazamo wa kificho. Na walio amini watasema: Hakika wapatao khasara ni hao walio khasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ama hakika wenye kudhulumu watakuwa katika adhabu ya kudumu.
وَمَا كَانَ لَهُم مِّنْ أَوْلِيَاءَ يَنصُرُونَهُم مِّن دُونِ اللَّهِ ۗ وَمَن يُضْلِلِ اللَّهُ فَمَا لَهُ مِن سَبِيلٍ
Wala hawatakuwa na walii wa kuwanusuru mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana njia yoyote.
Aya hizi zinabainisha upeo wa juu wa hofu itakayowajaa madhalimu Siku ya Kiyama. Watu ambao hapa duniani walikuwa wakiwatisha wenzao kwa kuwaonyesha ubabe na kutumia mabavu na kuwafanya muda wote wawe na hofu na kihoro cha kuandamwa na dhulma na uonevu wa madhalimu hao, siku hiyo watapatwa na khofu na mshtuko kiasi cha kuwafanya washindwe kuinua vichwa vyao. Watasimamishwa wakiwa wanyonge na dhalili, huku wakiona aibu wakati wanangojea kuingizwa motoni. Watakuwa wanaitazama Jahanamu kwa jicho la kificho kutokana na uthakili wa unyonge na hali ya idhilali itakayowapata. Watajawa na khofu na watapatwa na mshituko mkubwa; na hali ya udhalilifu itazitawala na kuzigubika nafsi zao. Lakini gumu zaidi kuliko adhabu na mateso ya kimwili watakayopata watu hao, ni lawama na masimango ya waumini ambao watawaambia: "Nyinyi mliokuwa mkijigamba na kujiona kwa utajiri na nguvu za mamlaka mlizokuwa nazo, mnaona ni hasara iliyoje imekufikeni leo? Hasara ambayo imezifilisisha nafsi zenu na leo mumehudhurishwa hapa mukiwa mikono miputu. Na si nyinyi wenyewe tu, bali mumewatia hasarani pia watu wa aila zenu, wafuasi wenu, wale waliokuzungukeni pamoja na waliokuwa wakikuungeni mkono; kwa sababu walikuwa wakidhani kwamba, wakiwa pamoja na nyinyi watapata saada na fanaka. Lakini leo wanajionea wenyewe kwamba, nyinyi hamna uwezo hata wa kujinusuru nafsi zenu, seuze mtake kuwaokoa na wao. Basi kuna kukhasirika kukubwa zaidi kuliko mtu kuipoteza katika njia ya batili nafsi yake mwenyewe, mke wake, watoto na jamaa zake; na akaihilikisha nafsi yake yeye mwenyewe na za watu wake wote hao, kwenye hasara ya milele? Kisha aya zinasisitiza kwa mara nyingine tena kwamba, mwisho huo mbaya ni matokeo ya mambo yaliyowafanya wao wapotoke walipokuwa duniani na leo akhera yanawasukumiza kwenye shimo la moto wa Jahanamu. Ni adhabu ya kuendelea na ya milele. Huko madhalimu hawatakuwa na msaidizi yeyote wa kuwapa msaada na kuwaepusha na adhabu ya Mola. Wao walikata mahusiano na manabii na mawalii wa Mwenyezi Mungu, kwa hivyo watabaki peke yao na bila ya yeyote wa kuwasaidia mbele ya adhabu ya Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, utukufu na udhalili wa kweli utadhihirika Siku ya Kiyama. Si hasha watu wanaoonekana watukufu na wenye kuheshimika leo hapa duniani, Siku ya Kiyama wakawa madhalili kabisa; na kinyume chake, si ajabu watu wanaoonekana dhalili na wanyonge leo hapa duniani, kesho akhera wakawa watukufu na wenye kuheshimika. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hasara na kukhasirika kukubwa zaidi kwa mtu ni kupoteza rasilimali ya umri wake bila ya tija wala kuwa na masurufu ya kwenda kumfaa akhera. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, imani ndiyo ya kumpatia muumini heshima na utukufu duniani na akhera na sababu ya kupata nusra na uokovu Siku ya Kiyama.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 47 ya sura yetu ya Ash-Shuura isemayo:
اسْتَجِيبُوا لِرَبِّكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا مَرَدَّ لَهُ مِنَ اللَّهِ ۚ مَا لَكُم مِّن مَّلْجَإٍ يَوْمَئِذٍ وَمَا لَكُم مِّن نَّكِيرٍ
Muitikieni Mola wenu Mlezi kabla haijafika siku isiyo epukika itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hamtakuwa na pa kukimbilia wala hamtakuwa na cha kukataa.
Katika zama zote za historia, Mitume wa Mwenyezi Mungu wamewalingania watu wito wa Allah; na si kuwataka wawafuate wao. Kwa hiyo aya hii ya 47 inawahutubu makafiri, madhalimu na wafanya madhambi kwamba: kabla ya kuondoka duniani na kusubiri Siku ya Kiyama mkaombe kurudishwa duniani, acheni kufuata njia ya upotofu; na badala yake shikamaneni na njia iliyonyooka ya uongofu aliyokuwekeeni Mola wenu. Kwa sababu, Siku ya Kiyama itakuwa ni baina yenu nyinyi na Allah na hakuna chochote kitakachothibiti isipokuwa kile atachotaka Yeye Mola tu. Hamtaweza kufanya hila yoyote ili kuyakana mliyoyatenda na hakuna mtu yeyote atakayekuwa na uwezo wa kukulindeni na adhabu ya Moto. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kutii na kutekeleza maamrisho ya Allah SWT ndiko kutakotulinda na kutuepusha na hasara ya milele na ndio wenzo wa uokovu na wa kutuwezesha kupata saada na fanaka ya duniani na akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kabla ya suhula na fursa tuliyopewa duniani hazijamalizika, tufikirie mwisho wa umri na uhai wetu na safari isiyo na marejeo iliyoko mbele yetu ya kuelekea ulimwengu mwingine wa akhera. Wapenzi wasikilizaj, darsa ya 894 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, azifanye thabiti imani zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/