May 24, 2023 10:34 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 895 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 42 ya Ash-Shuura. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 48 ya sura hiyo ambayo inasema:

فَإِنْ أَعْرَضُوا فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا ۖ إِنْ عَلَيْكَ إِلَّا الْبَلَاغُ ۗ وَإِنَّا إِذَا أَذَقْنَا الْإِنسَانَ مِنَّا رَحْمَةً فَرِحَ بِهَا ۖ وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ فَإِنَّ الْإِنسَانَ كَفُورٌ

Na wakipuuza, basi Sisi hatukukupeleka ili uwe mwenye kuwalinda. Si juu yako ila kufikisha Ujumbe tu. Na hakika Sisi tukimwonjesha mtu rehema kutoka kwetu, huifurahia. Na akisibiwa na ovu kwa sababu ya iliyo yatanguliza mikono yao, basi hakika mtu huyu anakufuru.

Moja ya sifa maalumu ambayo walikuwa nayo Mitume ni kuwahurumia watu wao na kuwa na uchungu nao kwa sababu ya kutaka waongoke; na daima walikuwa wakihuzunika kuona baadhi yao hawaiamini haki na kufuata njia iliyonyooka ya uongofu. Kwa ajili hiyo, walikuwa wakifanya jitihada kila mara na kadiri ilivyowezekana, kuwaelekeza watu kwenye njia ya haki. Kuhusiana na hilo, aya tuliyosoma inamhutubu Bwana Mtume SAW ya kwamba: Ewe Mtume, hata ujitahidi vipi, watakuwepo tu baadhi ya watu watakaojitenga na kuukataa wito wako. Wewe huna dhima tena yoyote kwao, kwa sababu umeshawafikishia ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu. Mwenyezi Mungu hakutaka waja wake waiamini haki kwa nguvu na kulazimishwa; na wala wewe hukutakiwa uwalazimishe waikubali haki. Mwenyezi Mungu ametaka watu waamini kwa ridhaa na hiari yao, kwa sababu ni imani ya aina hiyo tu ndiyo yenye thamani. Kisha aya inaendelea kwa kumliwaza Bwana Mtume kuwa, kama baadhi ya watu wanaamua kujitenga na wewe, basi wanafanya hivyo kuhusiana na Mwenyezi Mungu pia. Kwa sababu baada ya neema zote hizo ambazo Allah amewapa, wanadamu wanaingiwa na ghururi kwa walivyojaaliwa, kiasi cha kumsahau Mola wao na kutomshukuru kwa neema hizo alizowapa. Na hata wanapofikwa na shida, masaibu na misukosuko kutokana na madhambi waliyofanya, hakuwasaidii kuzinduka na kutanabahi, bali wanaendelea kubaki kwenye hali ya mghafala. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, jukumu la viongozi na wafanya tablighi ya dini ni kufikisha tu wito wa Allah, si kuwalazimisha watu waukubali. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kawaida ya watu wengi ni kuingiwa na ghururi na kujisahau wanapokuwa katika raha na uneemevu; na kughafilika na wajibu wa kumshukuru Mola wao kwa neema alizowapa. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, shida na matatizo yanayotokea katika maisha ya mwanadamu, mara nyingi huwa ni matokeo ya amali na mwenendo wake mwenyewe, lakini Mwenyezi Mungu huwa hamtakii afikwe na masaibu hayo.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 49 na 50 ambazo zinasema:

لِّلَّهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ يَهَبُ لِمَن يَشَاءُ إِنَاثًا وَيَهَبُ لِمَن يَشَاءُ الذُّكُورَ

Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa kiume, 

أَوْ يُزَوِّجُهُمْ ذُكْرَانًا وَإِنَاثًا ۖ وَيَجْعَلُ مَن يَشَاءُ عَقِيمًا ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ قَدِيرٌ

 Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza.

Aya iliyotangulia imeashiria kuwa, neema na rehma yoyote ile ipatikanayo katika ulimwengu huu basi inatoka kwa Mwenyezi Mungu. Kisha aya tulizosoma zinaendeleza nukta hiyo kwa kueleza kwamba, uendeshaji wa mbingu na ardhi uko kwa Mwenyezi Mungu na Yeye huumba chochote kile atakacho. Daima Mwenyezi Mungu yuko katika uumbaji, na si kwamba alishaumba ulimwengu huko nyuma na uumbaji huo umeshakamilika na kumalizika. Kisha aya zinaashiria moja ya neema muhimu zaidi za Allah kwa waja wake, ambayo ni neema ya mtoto. Ni hakika kabisa kwamba baba na mama, sio waumbaji wa mtoto, bali ni wasita na kiunganishi cha uumbaji wa Allah; na ni Yeye Mola ndiye anayemuumba mtoto, awe wa kike au wa kiume. Kwa mujibu wa aya hizi, watoto wote, wa kike na wa kiume ni hidaya ya Mwenyezi Mungu; na kwa mtazamo wa Qur'ani, si sahihi kutafautisha baina yao. Na bila shaka kwa mtu aliye tasa, huyo pia amekuwa hivyo kwa irada ya Mwenyezi Mungu, ambaye amemkadiria hilo kulingana na hekima yake. Na Yeye Allah ana ilimu na ujuzi kamili wa uendeshaji masuala ya ulimwengu na wanadamu; na ni Mweza pia wa kufanya lolote lile atakalo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mtoto, awe wa kike au wa kiume, ni hidaya ya Mwenyezi Mungu kwa wazazi; na haifai kutafautisha baina yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Mwenyezi Mungu daima yuko katika uumbaji, na kila kitoto kichanga kizaliwacho katika pembe yoyote ile ya dunia ni mfano mmojawapo wa uumbaji wake. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, kama tunaiamini ilimu, ujuzi, uwezo na qudra ya Mwenyezi Mungu, basi tuwe na imani na Yeye Mola kwa atakavyotukadiria, kama tuwe na mtoto au la; na kama mtoto huyo atakayezaliwa, awe ni mwanamme au mwanamke.

Ifuatayo sasa ni aya ya 51 ya sura yetu hii ya Ash-Shuura, ambayo inasema:

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ عَلِيٌّ حَكِيمٌ

Na haikuwa kwa mwanaadamu kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa Wahyi (Ufunuo), au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye humfunulia ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hikima.

Sura hii ya Ash-Shuura ilianza na maudhui ya wahyi walioteremshiwa Mitume na inahitimishwa pia na maudhui hiyohiyo. Kwa kuanzia aya inasema: mwanadamu hawezi kusemezwa moja kwa moja na Mwenyezi Mungu, kwa sababu Allah SWT si mwepo wa kiwiliwili, hata aseme na kuongea kwa mdomo na ulimi; na watu wayasikie kwa masikio yao yale ayasemayo. Lakini ilivyo ni kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu anawasiliana na Mitume wake kwa njia tatu, moja kati ya hizo ikiwa ni ya Mtume kupewa ilhamu ndani ya moyo wake, kuyajua yale apaswayo kuyajua na kisha kuyalingania na kuwafikishia watu. Katika njia ya pili, Mwenyezi Mungu huweka mawimbi ya sauti ambayo humfikia akayasikia Mtume wake bila kushuhudiwa na mtu mwengine yeyote, kama ilivyotokea kwa Nabii Musa AS. Na katika njia ya tatu, humtuma Malaika wake wa wahyi Jibril kwa Mtume, na yeye Mtume akapokea wahyi huo wa Allah kupitia Malaika huyo mteule. Alaa kulli haal, wahyi ulikuwa ukiteremshwa kwa namna ambayo, Mtume ikimthibitikia kwa uhakika kwamba, maneno hayo yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Na watu kwa upande wao, walipata hakikisho kupitia miujiza aliyofanya Mtume, kwamba mja huyo mteule anayedai kuwa anapokea wahyi, ni kweli ana mawasiliano na Mwenyezi Mungu, na mambo ayafanyayo, yako nje ya uwezo wa mwanadamu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Mwenyezi Mungu amewasiliana nao na kuwafikishia maneno yake wajumbe wake kwa njia tofauti, ili waufikishe ujumbe wake kwa watu na kuwaongoza katika njia ya haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, suala kwamba ni nani miongoni mwa wanadamu, awe msemezwa wa Allah SWT, hilo liko kwenye hiari yake Mola, ambaye huamua kwa ujuzi na hekima yake, kumchagua mja huyo na kumteremshia wahyi wake.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 52 na 53 ambazo zinasema:

وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ رُوحًا مِّنْ أَمْرِنَا ۚ مَا كُنتَ تَدْرِي مَا الْكِتَابُ وَلَا الْإِيمَانُ وَلَٰكِن جَعَلْنَاهُ نُورًا نَّهْدِي بِهِ مَن نَّشَاءُ مِنْ عِبَادِنَا ۚ وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

Na namna hivi tumekufunulia wahyi roho kwa amri yetu. Ulikuwa hujui Kitabu ni nini, wala Imani. Lakini tumeifanya kuwa ni Nuru ambayo kwayo tunammwongoza tumtakaye katika waja wetu. Na hakika wewe unaongoza kwenye Njia Iliyo Nyooka.

صِرَاطِ اللَّهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِلَى اللَّهِ تَصِيرُ الْأُمُورُ

Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye tu viliomo mbinguni na ardhini. Jueni kuwa mambo yote yanarudi kwa Mwenyezi Mungu.

Aya hizi ambazo ni za mwisho za sura hii ya Ash-Shuura zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya iliyotangulia kuhusu aina ya njia za uteremshwaji wahyi na kumhutubu Bwana Mtume SAW ya kwamba: kama tulivyowateremshia wahyi Mitume wengine waliotangulia, ndivyo na wewe pia tumekushushia hii Qur'ani inayowapa uhai wanadamu; na kama ilivyo roho kwa kiwiliwili cha mtu, nayo pia inakivaa na kukipa uhai kiwiliwili cha jamii ya wanadamu. Ni kama inavyoeleza Qur'ani yenyewe katika aya ya 24 ya Suratul-Anfal ya kwamba:  Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba, kuteremshwa wahyi ni rehma ya Allah, ambayo kwanza ilimfikia Mtume wake kwa kuteremshiwa aya za Mola wake. Yeye Bwana Mtume aliyaamini kikamilifu yaliyomo ndani yake; na kisha rehma hiyo ikawajumuisha wanadamu wote, ambao waliutambua ukweli na hakika ya Uislamu kupitia Bwana Mtume na nuru ya aya za Qur'ani alizowasomea. Kuhusiana na nukta hiyo, aya zinamhutubu Bwana Mtume SAW kwa kumwambia: Qur'ani si nuru kwako wewe tu, bali ni nuru ya wote na wenzo wa uongofu kwa walimwengu wote wa kuwaelekeza kwenye njia iliyonyooka; na wewe unawaongoza watu katika njia sahihi ya maisha. Katika kuielezea Njia Iliyonyooka aya zinasema: Hiyo ni njia ya Mwenyezi Mungu ambaye, vyote vilivyomo mbinguni na ardhini ni vyake Yeye. Na naam, njia hiyo inaishia kwa Mwenyezi Mungu. Njia iliyonyooka, ndio njia pekee inayoelekea kwa Allah SWT; na je kuna njia iliyonyooka zaidi na iliyo safi na ing'aayo zaidi kuliko ile imfikishayo mwanadamu kwa Muumba wa ulimwengu, Mtawala na Mwendeshaji wake? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mitume hawana uongofu utokanao na wao wenyewe; bali wao pia wanahitaji uongofu wa Mwenyezi Mungu, ili nao waweze kuwa walezi na waongozaji wa wanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mafundisho ya Qur'ani, ni chemchemi ya uongofu wa watu na uhai wa jamii yao, tab'an kwa sharti kwamba, wayakubali na kuyatekeleza, na si kuzisoma tu aya za kitabu hicho pasi na kuzitafakari na kuzifanyia kazi. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, Qur'ani peke yake haitoshi, bali inahitaji mwalimu na mwongozaji ili mafundisho yake yajengayo na kuyapa uhai maisha ya watu yaweze kutekelezwa katika jamii na kuwa kigezo cha kivitendo cha njia iliyonyooka. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 895 ya Qur'ani imefikia tamati na ndiyo inayotuhitimishia tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 42 ya Ash-Shuura. Inshaallah tuwe tumeaidhika, tumeelimika na kunufaika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/