May 24, 2023 08:08 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 897 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 11 na 12 ya sura hiyo ambazo zinasema:

وَالَّذِي نَزَّلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً بِقَدَرٍ فَأَنشَرْنَا بِهِ بَلْدَةً مَّيْتًا ۚ كَذَٰلِكَ تُخْرَجُونَ

Na ambaye ameteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na kwa hayo tukaifufua nchi iliyo kufa. Na namna hivi ndivyo mtakavyo tolewa.

وَالَّذِي خَلَقَ الْأَزْوَاجَ كُلَّهَا وَجَعَلَ لَكُم مِّنَ الْفُلْكِ وَالْأَنْعَامِ مَا تَرْكَبُونَ

Na ambaye ameumba katika kila kitu jike na dume, na akakufanyieni marikebu na wanyamahowa mnao wapanda. 

Aya za mwisho tulizosoma katika darsa iliyopita zilizungumzia tauhidi katika ulimwengu wa maumbile. Aya hizi tulizosoma zinaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: uhai wa ardhi na mimea na uhai wenu nyinyi wanadamu unategemea kuteremshwa kwa mvua; na ikiwa itatokea sehemu yoyote ya ardhi ikakosa mvua, hukumbwa na ukame na baa la njaa na wanadamu hupoteza maisha kwa njaa na kiu. Suali la kujiuliza ni je, joto la jua linalopiga baharini na maji hayo kugeuka mvuke, kunatokana na uwezo wa mwanadamu; na je yeye mwanadamu ana mchango wowote katika mwenendo wa unyeshaji mvua? Tujiulize pia, je kufanyika kwa mawingu na kuvuma kwa upepo unaosukuma mawingu hayo kuelekea ardhi kavu na yabisi, kunatokana na nguvu za mwanadamu? Ardhi kavu na yabisi zilizoficha ndani yake mbegu za mimea, wakati inaponyesha mvua huanza kuhuika na kuchipua aina mbalimbali za mimea. Kuchipua na kukua mimea na kuchanua maua ya rangi tofauti pamoja na mashamba yanayootesha miti ya kila aina ya matunda, vyote hivyo vinatokana na baraka ya mvua. Na kama ambavyo ardhi yabisi iliyokufa huhuika kwa kunyeshewa na mvua, na nyinyi wanadamu pia ndivyo mtakavyofufuka baada ya kufa na kuzikwa. Kuteremshwa kwa mvua na kuhuika ardhi kavu iliyokufa, kunadhihirisha ujuzi na uwezo usio na mpaka wa Allah SWT; na hivyo kutobakisha hata chembe ya shaka kwamba Kiyama kitasimama na ni jambo linaloyumkinika kwa wafu kufufuliwa na kupewa uhai tena. Kusema kweli huo ni mfano mmojawapo wa kufufuliwa wanadamu, ambao umeashiriwa katika aya nyingi za Qur'ani. Kisha aya zinaendelea kuashiria suala la kuwepo jozi katika uumbaji na kubainisha kuwa, uumbwaji wa viumbe mbalimbali vilivyo hai, ambao wote unafuata kanuni ya jozi ya jike na dume na ambavyo kuendelea uhai na kuwepo kwao kunategemea hali hiyo, kusingeyumkinika isipokuwa kwa irada ya Allah SWT. Katika aya hizi zimeashiriwa pia merikebu na vipando vinginevyo ambavyo Mwenyezi Mungu amewawekea wanadamu kwa ajili ya kukata masafa katika njia za baharini na nchi kavu, ambazo kwa hakika ni miongoni mwa rehma na ukarimu wa Mola Mrehemevu kwa waja wake. Tangu enzi na enzi, imezoeleka kutumia merikebu na majahazi katika safari za baharini kwa ajili ya kusafirisha watu na bidhaa kutoka sehemu moja hadi nyingine. Ajabu ni kwamba, kutokana na kanuni maalumu za fizikia, mameli makubwa makubwa na licha ya kubeba shehena nzito za mizigo, yanapasua mawimbi bila kuzama majini. Hakuna yeyote aliyeziweka kanuni hizo katika ulimwengu ghairi ya Allah SWT. Katika zama hizi pia, kuna aina mbalimbali za vipando na vyombo vya usafiri zikiwemo gari, treni ziendazo kwa kasi pamoja na ndege, ambavyo vyote hivyo vimepanua wigo wa shughuli na harakati za wanadamu na kubadilisha sura ya maisha yao. Yote hayo yanatokana na rehma za Mwenyezi Mungu, kwa sababu vyombo hivyo vya usafiri vinavyotembea kwa kasi, navyo pia vinafanya hivyo kwa kutumia kanuni mbalimbali ambazo Yeye Mola ameziweka katika ulimwengu wa uumbaji. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mfumo wa ulimwengu unafuata kanuni maalumu ambazo Allah SWT ameipangia na kuikadiria kila sehemu ya mfumo huo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Mwenyezi Mungu ameweka utaratibu wa kila jambo kufanyika kupitia sababu na visababishi; na ndio maana mvua imefanywa kuwa sababu ya kupatikana uhai kwa ardhi na viumbe viishio ardhini. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, uundaji na utengenezaji wa vitu vya aina mbalimbali umefanywa na wanadamu kwa kutumia kanuni alizoweka Mwenyezi Mungu katika ulimwengu wa maumbile; walichofanya wanadamu ni kugundua tu kanuni hizo na kuzitumia.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 13 na 14 ambazo zinasema:

لِتَسْتَوُوا عَلَىٰ ظُهُورِهِ ثُمَّ تَذْكُرُوا نِعْمَةَ رَبِّكُمْ إِذَا اسْتَوَيْتُمْ عَلَيْهِ وَتَقُولُوا سُبْحَانَ الَّذِي سَخَّرَ لَنَا هَٰذَا وَمَا كُنَّا لَهُ مُقْرِنِينَ

Ili mkae vizuri migongoni mwao, kisha mkumbuke neema za Mola wenu Mlezi mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Ametakasika aliye mfanya huyu atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe. 

وَإِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا لَمُنقَلِبُونَ

Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi. 

Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kuhusu nafasi na mchango wa marikebu na nyamahowa, yaani wanyama wa miguu minne katika maisha ya wanadamu na kueleza kwamba, kila mpandapo kipando, kiwe kilichoundwa na mwanadamu kama meli, ndege, gari na treni; au vipando vya jadi kama farasi, ngamia na nyumbu msisahau kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliyekutiishieni wanyama na vipando hivyo. Nyinyi wanadamu mmegundua tu sifa mbalimbali alizojaalia Mwenyezi Mungu katika vitu na mada za aina kwa aina; na kwa kuzitumia sifa na hali za vitu na mada hizo mmeweza kuunda vyombo vya uchukuzi na usafiri kama meli, ndege na treni na kuvitiisha mmpendavyo. Mwenyezi Mungu amejaalia na kuwafanya baadhi ya wanyama wapole na maridhia, kwenu nyinyi wanadamu, japokuwa wanyama hao wana nguvu nyingi zaidi kimaumbile kulinganisha na nyinyi na kwa hivyo isingetarajiwa wawe maridhia na watiifu kwenu. Kama si rehma na uraufu wa Allah, msingekuwa na uwezo wa kuwatiisha wanyama hao. Kwa hivyo inapasa sisi wanadamu tumtakase, kumhimidi na kumshukuru Yeye Mola, ambaye amevifanya vipando na vyombo vyote hivyo viwe maridhia na vitiifu kwa mwanadamu. Kwa kumalizia, aya zimegusia suala la mwanadamu kurejea kwa Mola wake. Na sababu ni kwamba wakati anapopanda vipando, hasa vyombo hivyo vyenye kukata masafa makubwa na kwa kasi, asije mtu akaingiwa na ghururi na majivuno kutokana na neema hizo za kidunia. Vyovyote iwavyo, muikumbuke akhera, kwa sababu kuna watu wengi wanaotumia vipando na vyombo vyao hivyo kujikweza, kujivuna na kujifakharisha navyo mbele ya wenzao. Lakini jengine ni kwamba, kupanda vipando hivyo na kuweza kuhama kutoka mahali pamoja hadi pengine kutuzindue na kutukumbusha pia kuhusu kuhama kwetu kutoka dunia hii kuelekea ulimwengu mwingine. Kwani vyovyote itakavyokuwa, mwishowe tutaelekea kwa Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tusimsahau Allah SWT tunapozitumia neema za kimaada; na tumshukuru kwa kutuneemesha neema hizo. Inafaa ushukurivu huo tuukamilishe kwa kumsabihi na kumtakasa Yeye Mola Muumba. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tuonyeshe kwa dhati mbele ya Allah kwamba sisi si waweza, wala si lolote si chochote mbele yake Yeye. Huo wenyewe ni mfano mmojawapo wa ushukurivu; na si kujikweza, kujivuna na kuwa na ghururi kutokana na tuyafanyayo. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, tunapokuwa kwenye safari za duniani, tuikumbuke pia safari ya akhera, ambayo huanza kwa kifo.

Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 15 ambayo inasema:

وَجَعَلُوا لَهُ مِنْ عِبَادِهِ جُزْءًا ۚ إِنَّ الْإِنسَانَ لَكَفُورٌ مُّبِينٌ

Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanaadamu ni mwenye kukufuru waziwazi. 

Baada ya aya zilizotangulia kutaja mifano kadhaa ya tauhidi katika uumbaji na uleaji wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake, aya hii inazungumzia shirki inayofanywa na baadhi ya watu kwa kusema, inakuwaje baadhi ya washirikina wanawadhania malaika kuwa ni wana wa Mwenyezi Mungu na kuwachukulia kuwa ni sehemu na wanatokana na wazazi wawili kama walivyo watoto wengine? Mwenyezi Mungu hana umbo, hata awe na sehemu, au iyumkinike kupatikana sehemu ya kitu kinachotokana na Yeye. Malaika, wao pia kama walivyo viumbe wengine, wameumbwa na Allah SWT. Wao ni watendaji wanaohudumu katika mfumo wa ulimwengu, na si sehemu ya Mwenyezi Mungu, wala si wana wa Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, katika zama zote za historia, zimekuwepo khurafa na imani nyingi potofu na za uzushi kuhusu Mwenyezi Mungu na uhusiano wake na viumbe vyake. Yote hayo yametokana na ujinga wa watu au kuacha kwao kufuata mafundisho ya uongofu yaliyoletwa na Mitume. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, malaika wameumbwa na Allah na wanatii na kutekeleza amri za Mola; si wana wa Mungu hata wawe na hali ya Kiungu. Vilevile aya hii inatutaka tuelewe kwamba, imani za khurafa na shirki humfanya mtu awe mbali na Mwenyezi Mungu, aikengeuke njia iliyonyooka na kuzikufuru neema za Mola. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 897 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa washukurivu wa neema zake, kubwa na ndogo, tuzijuwazo na tusizozijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/