May 24, 2023 08:18 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 898 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 16 hadi ya 18 ya sura hiyo ambazo zinasema:

أَمِ اتَّخَذَ مِمَّا يَخْلُقُ بَنَاتٍ وَأَصْفَاكُم بِالْبَنِينَ

Au amejichukulia watoto wa kike katika vile alivyo viumba, na akakuchagulieni nyinyi watoto wa kiume?

وَإِذَا بُشِّرَ أَحَدُهُم بِمَا ضَرَبَ لِلرَّحْمَٰنِ مَثَلًا ظَلَّ وَجْهُهُ مُسْوَدًّا وَهُوَ كَظِيمٌ

Na anapo bashiriwa mmoja wao kwa yale aliyo mpigia mfano Mwenyezi Mungu, uso wake husawijika na hujaa hasira. 

أَوَمَن يُنَشَّأُ فِي الْحِلْيَةِ وَهُوَ فِي الْخِصَامِ غَيْرُ مُبِينٍ

Ati aliye lelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi kusema kwa bayana...?

Aya hizi zinaashiria moja ya imani potofu na ya khurafa iliyoenea katika zama zote za historia katika kaumu nyingi za watu na kueleza kwamba, imani hiyo ni kufadhilisha jinsia ya kiume kuliko ya kike; na kimsingi hasa ni kumchukulia mtoto wa kike kuwa ni nuhsi. Kwa hivyo aya zinasema: Vipi nyinyi mnawaona watoto wa kiume wana ubora kuliko wa kike, mpaka ikawa azaliwapo mtoto wa kiume mnafurahi, lakini anapozaliwa mtoto wa kike nyuso zenu zinasawijika na kujawa na ghadhabu? Baya zaidi ni kwamba, mnawanasabisha watoto wa kiume na nyinyi wenyewe na mnajifakharisha nao, lakini mnawanasibisha mabanati na Mwenyezi Mungu, kwamba Yeye amewaumba, lakini sio takwa lenu. Mvulana, ambaye ni msaidizi wenu katika kazi za biashara na uzalishaji na ambaye wakati wa vita ni askari mpiganaji, huyo mnamtambua kuwa anatokana na nyinyi; lakini msichana, ambaye anakulia kwenye mazingira ya nyumbani ya kushughilikia utanashati na mapambano bila kushirikishwa kwenye mambo mengine ya nje; na kwa sababu hana nguvu na sauti kwenye mitifuano na majadiliano, yeye ndio mnamnasibisha na Mwenyezi Mungu!? Inajulikana wazi kuwa mwanamke na mwanamme, wote wawili ni viumbe wa Mwenyezi Mungu; na uwepo wa wote wawili unahitajika ili kizazi cha mwanadamu kiendelee kubaki. Mbele ya Allah SWT hakuna yeyote baina ya wawili hao aliye mbora zaidi ya mwenzake, ijapokuwa kwa kuzingatia nafasi ya kila mmoja katika maisha, mwanamke na mwanamme wana baadhi ya mambo wanayotafautiana kinafsi na kimwili.  Moja ya tofauti hizo ni wanawake kutawaliwa zaidi na hisia za kiroho katika maneno na vitendo vyao. Ukweli ni kwamba, kwa sababu ya nafasi kuu ya wanawake katika maisha, ambayo ni ya umama, Mwenyezi Mungu Mtukufu amewajaalia kuwa na sifa maalumu, ambazo zimewafanya wasameheke kushirikishwa kwenye mambo ya vita na mapigano. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwatafautisha watoto wa kike na wa kiume, chimbuko lake ni imani potofu na za kikhurafa, ambazo Qur’ani inazipinga vikali. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kupenda urembo na mapambo kwa mabanati na wanawake ni jambo la kimaumbile na linalokubalika. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mazingira ya vita na mitifuano si ya kushirikishwa wanawake, kwa sababu hayaendani na maumbile yao.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 19 na 20 ambazo zinasema:

وَجَعَلُوا الْمَلَائِكَةَ الَّذِينَ هُمْ عِبَادُ الرَّحْمَٰنِ إِنَاثًا ۚ أَشَهِدُوا خَلْقَهُمْ ۚ سَتُكْتَبُ شَهَادَتُهُمْ وَيُسْأَلُونَ

Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wao wataulizwa!

وَقَالُوا لَوْ شَاءَ الرَّحْمَٰنُ مَا عَبَدْنَاهُم ۗ مَّا لَهُم بِذَٰلِكَ مِنْ عِلْمٍ ۖ إِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ

Nao husema: Angeli penda Mwingi wa Rehema tusingeli waabudu sisi. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu! 

Moja ya imani potofu ambayo walikuwa nayo washirikina ni kuwaitakidi malaika kuwa ni mabinti wa Mwenyezi Mungu; na waliikazania na kuing’ang’ania imani hiyo ya uzushi, utadhani, nastaghfirullah, wao walishuhudia na kumwona Mwenyezi Mungu akiwazaa viumbe hao! Baya zaidi ni kwamba, wakiwaabudu malaika na kuamini kuwa kwa namna fulani, wana nafasi na ushiriki katika uendeshaji wa mambo ya ulimwengu. Hali ya kuwa imani hizo zilitokana na dhana zisizo na msingi wowote na wala hazikuwa na uthibitisho wowote wa kielimu. Na ndipo Qur’ani ikasema: Dai lao hilo potofu litakuja kuulizwa Siku ya Kiyama; na wao hawatakuwa na jawabu ya kutoa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni haya yafuatayo: Mosi, malaika ni viumbe wa Mwenyezi Mungu, si watoto wake. Na kinyume na wanadamu, wao hawako katika jinsia ya kike au ya kiume. Pili, kumwabudu kiumbe yeyote wa Allah, awe ni malaika au mwanadamu kama Nabii Isa AS, kutaulizwa na kusailiwa Siku ya Kiyama. Tatu, tusidhani tuyasemayo na yatokayo vinywani mwetu yanafutika na kutoweka. Hasha wa kalla. Chochote tunachokisema kinahifadhiwa katika mfumo wa ulimwengu na iko siku itatupasa tuje kuwajibika na kujieleza kwa tuliyodai na tuliyoyasema. Na nne ni kwamba, tusihalalishe na kutetea jambo potofu kwa kulinasibisha na Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Yeye Allah SWT, ambaye ameteremsha Kitabu na ametuma Mtume na mwongozo kwa ajili ya mwanadamu, hajawahi katu kututaka tufuate njia ya dhalala na upotofu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 21 na 22 ambazo zinasema:

أَمْ آتَيْنَاهُمْ كِتَابًا مِّن قَبْلِهِ فَهُم بِهِ مُسْتَمْسِكُونَ

Kwani tuliwapa Kitabu kabla ya hichi, na ikawa wao wanakishikilia hicho?

بَلْ قَالُوا إِنَّا وَجَدْنَا آبَاءَنَا عَلَىٰ أُمَّةٍ وَإِنَّا عَلَىٰ آثَارِهِم مُّهْتَدُونَ

Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, basi na sisi tunaongoza nyayo zao.

Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kuhusu imani potofu na za khurafa walizokuwa nazo washirikiana na kuzungumzia chimbuko lake kwa kusema: si kwamba wao wana ushahidi kutoka kwenye mafundisho ya Mitume na Vitabu vya mbinguni walivyoteremshiwa, wa kuteteta na kuhalalisha uzushi na khurafa zao; kwa sababu hakuna Mtume yeyote aliyewafunza watu khurafa na upotofu huo. Lakini ukweli ni kwamba watu hao walizikubali imani na itikadi hizo kwa kufuata yale yaliyofanywa na mababu na wazee wao waliotangulia. Wazee ambao, wao wenyewe walikuwa katika ujinga na ujahili, pasi na kuwa na elimu na ujuzi wowote; na wakamnasibishia Mwenyezi Mungu mambo mbali mbali kutokana na makisio na dhana batili. Kwa maneno mengine ni kwamba, imani hizo potofu na za uzushi hazina mashiko wala msingi wa kielimu na kiakili au ushahidi wa maandishi kutoka kwenye vitabu vya mbinguni walivyoteremshiwa Mitume waliopita. Ni ufuataji na uigaji kibubusa wa yale yaliyokuwa yakifanywa na mababa na mababu zao waliotangulia, ndio uliopelekea kukubaliwa mambo hayo na watu. Hali ya kuwa hakuna mtu yeyote muelewa na mwenye akili timamu anayefanya uigaji kuwa ndio msingi wa kufuata katika mambo yanayohusu fikra, imani na itikadi zake; na tena uigaji wenyewe ni wa yeye mtu mjinga wa jambo kumfuata mtu mwingine aliye mjinga kama yeye. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, fikra na itikadi zinatakiwa zisimame juu ya msingi wa akili au wahyi. Kitu kisichokubaliana na akili na wahyi ni shirki na uzushi, hata kama kitajulikana kama mila, desturi na utamaduni wa jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tujihadhari na kutetea, kutangaza na kueneza mila na desturi potofu katika jamii kwa kisingizio cha kutunza na kuendeleza turathi za kale na athari za waliotangulia. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kwa mtazamo wa Qur’ani taasubi na ukereketwa wowote ule juu ya kabila, taifa, asili au lugha unaopelekea kuiga mambo kibubusa na kufanya vitu visivyo na mantiki na visivyoingia akilini, haukubaliki hata kidogo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 898 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/