May 24, 2023 08:26 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 899 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 23 ya sura hiyo ambayo inasema:

وَكَذَٰلِكَ مَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ فِي قَرْيَةٍ مِّن نَّذِيرٍ إِلَّا قَالَ مُتْرَفُوهَا إِنَّا وَجَدْنَا آبَاءَنَا عَلَىٰ أُمَّةٍ وَإِنَّا عَلَىٰ آثَارِهِم مُّقْتَدُونَ

Na kadhaalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila watu wake wapenda anasa na starehe walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, na sisi tunafuata nyayo zao. 

Katika darsa iliyopita tulieleza kwamba, washirikina wa Makka walikuwa wakisema, sababu ya wao kufanya shirki na kuabudu masanamu ilikuwa ni kuiga na kufuata yaliyokuwa yakifanywa na wazee wao waliopita. Aya hii inamhutubu Bwana Mtume SAW ya kwamba: wanayosema washirikina hayakuanzia kwao wao tu, kwani hata Mitume wa kabla yako, nao pia walikumbana na watu ambao walipokuwa wakiwaonya na kuwatahadharisha na ubaya wa shirki na kuabudu masanamu, badala ya kuyapima na kuyatafakari maneno ya Mitume wao, walikuwa wakiwajibu kwamba: sisi tunataka kufuata njia ya mababa na mababu zetu na wala hatutaacha waliyokuwa wakifanya wao. Nukta muhimu ambayo inaashiriwa na aya hii ni jinsi wakuu wa kaumu mbalimbali na matajiri wa kaumu hizo waliotiwa ghururi na kuleweshwa na utajiri wao, walivyochangia sana katika kuwapinga Mitume. Aghalabu ya vinara wa wapinzani wa Mitume walikuwa matajiri na watu wenye madaraka wenye ubinafsi na wenye kutakabari, ambao walijijengea hadhi kubwa kwa watu kutokana na madaraka, mali na umaarufu wao; na watu wakawa wanawaridhia na kuwatii kwa sababu ya woga au tamaa. Wakuu na matajiri hao walikuwa wakijua kwamba, baada ya kudhihiri Mitume na kuaminiwa wito wao na watu, wanyonge watakomboka; na enzi zao za ubwana, dhulma na uonevu zitafikia tamati. Leo hii pia, tunashuhudia duniani kote jinsi wenye nguvu za utajiri na madaraka wanavyotumia nyenzo za vyombo vya habari na propaganda vilivyo kwenye mamlaka yao, kuwaghilibu, kuwadanganya na kuwapumbaza watu, ilhali akthari ya ufisadi na maovu yaliyotapakaa duniani yanatokana na madhalimu na mafisadi hao. Na kama atatokea mtu atakayetaka kuchukua hatua dhidi ya maslahi yao, humwandama wakamkandamiza na kumzima ili asije akahatarisha maslahi yao na kuwavurugia mipango yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, itikadi za jadi na athari za kifikra na kistaarabu zilizoachwa na waliotangulia zisiwe kizuizi cha kukifungia njia kizazi cha sasa ya kufikiri, kutafakari na kutumia akili; bali inapasa ziangaliwe upya. Kwani si ajabu wao waliopita ikawa wamekosea katika njia waliyofuata; na kuwafuata wao kibubusa kukatupotosha. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, jamii inahitaji watu waelewa na wenye uchungu nayo, ambao watazielewa hatari zinazoikabili na kuzitolea indhari hata kama watu wengi hawatoyajali maonyo na indhari hizo na watawapinga waonyaji hao. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, kama utajiri na madaraka havitadhibitiwa vinaweza kumfanya mtu awe asi na muovu. Na hiyo ndio sababu ya kushuhudiwa katika historia wenye utajiri na madaraka na watu maarufu na wenye hadhi maalumu katika jamii, ndio mara nyingi wanaowapiga vita wafuasi wa kweli wa njia ya haki.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 24 na 25 ambazo zinasema:

قَالَ أَوَلَوْ جِئْتُكُم بِأَهْدَىٰ مِمَّا وَجَدتُّمْ عَلَيْهِ آبَاءَكُمْ ۖ قَالُوا إِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ كَافِرُونَ

Akasema (Mwonyaji): Hata nikikuleteeni yenye mwongozo bora kuliko mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa tu hayo mliyo tumwa nayo.

فَانتَقَمْنَا مِنْهُمْ ۖ فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ

Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa walio kadhibisha! 

 Aya hizi zimeanza kwa kuwajibu waliokuwa wakisema, sisi tunaendeleza mila za wazee wetu na tunawafuata wao tu, ambapo Mitume wao waliwaambia: hata kama tumekuleteeni yaliyo bora kuliko yale mliyowakuta nayo wazee wenu; na yatakufanyeni mpate saada na fanaka, bado mtaamua tu kuikataa dini tuliyokuleteeni? Kwani nyinyi hamtaki mpate saada na fanaka? Kama mnataka, basi ingefaa muikubali na kuifuata dini na njia ya uhakika zaidi itakayokufikisheni kwenye saada hiyo. Hata hivyo ujinga na ukaidi wa watu, na taasubi na ukereketwa wa kibubusa waliokuwa nao uliwafanya waamue kuendelea kunga'ng'ania yale waliyoyarithi kwa wazee wao pasi na kutafakari kwa namna yoyote ile pendekezo walilopewa na Mitume wao; na kwa hivyo wakawajibu wajumbe hao wa Mwenyezi Mungu ya kwamba: Kuweni na uhakika kwamba sisi hatutakuaminini, kwa hivyo msijisumbue bure na wala msitukere na kutuudhi kwa maneno yenu! Nukta yenye kutoa mguso hapa ni kwamba, ijapokuwa Mitume walikuwa na yakini kwamba dini waliyokuja nayo wao ni ya haki; na wanayofuata washirikina ni batili, lakini wakati wa kujadiliana nao hawakuwaambia: kwa nini mnafuata njia ya batili na hamuikubali njia yetu sisi ya haki. Lakini wakizungumza kwa namna ya kutoegemea upande wowote na kuwaambia: hebu linganisheni dini yetu na yenu, muone ni ipi kwa mtazamo wenu iko karibu zaidi na uongofu muichague na kuifuata. Mbinu hii ya kujadiliana inayotumiwa na Qur’ani, inatufunza kuchunga adabu na muruwa katika kujadiliana na kubadilishana mawazo na watu wakaidi na wenye ghururi; na kutuonyesha kuwa, wakati waumini wanapofanya mdahalo na wapinzani inatakiwa wazingatie adabu na insafu. Badala ya kuuelezea kimkato tu upande wa pili kuwa uko kwenye batili, inapasa wabainishe ukweli wa maneno yao kwa hoja na mantiki na kuwataka wapinzani watafakari na kuchagua kufuata yale wanayoyaona kuwa ni sahihi. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba, inadi na ukaidi huo wa kuipinga haki ulifika hadi ya watu wa kaumu hizo kuasi na kupindukia mipaka katika maovu na mwishowe wakateremshiwa adhabu na Mwenyezi Mungu. Tab’an katika aya mbalimbali, Qur’ani imeashiria hatima na adhabu tofauti zilizowafika watu wa kaumu zilizopita ikiwemo baadhi yao kuangamizwa kwa tufani kali, wengine kwa tetemeko la ardhi la kutisha na wengine kwa upepo mkali na umeme uliowawakia kutokea mbinguni. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, moja ya njia ya kuutangaza Uislamu na kuulingania kwa watu ni kuyalinganisha mafundisho yake na ya dini na fikra nyinginezo kwa kutumia akili na mantiki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, katika kuchagua njia ya maisha tufadhilishe kufuata njia inayotegemea akili na wahyi kuliko ya kuiga mila, desturi, itikadi na mizimu ya waliotutangulia. Vilevile aya hizi zinatufunza kwamba, taasubi na ukereketwa wowote ule usio na msingi unaochochea inadi na ukaidi humnyima mtu uwezo wa kufanya upambanuzi sahihi na hivyo kushindwa kuibaini haki na ukweli.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 26 hadi 28 ambazo zinasema:

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ إِنَّنِي بَرَاءٌ مِّمَّا تَعْبُدُونَ

Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Hakika mimi ninajitenga mbali na hayo mnayo yaabudu.

إِلَّا الَّذِي فَطَرَنِي فَإِنَّهُ سَيَهْدِينِ

Isipo kuwa yule aliye niumba, kwani Yeye ataniongoza. 

وَجَعَلَهَا كَلِمَةً بَاقِيَةً فِي عَقِبِهِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ

 Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake ili warejee.

Aya hizi zinagusia kwa muhtasari habari za maisha ya Nabii Ibrahim AS ili kuwafahamisha washirikina wa Makka ya kwamba, nyinyi ambao mnamtaja Ibrahim kuwa ni babu yenu mkuu, kama kweli mnataka kufuata dini za wazee wenu waliotangulia, kwa nini hamufuati mila na dini yake yeye, ambayo ilikuwa ni ya tauhidi na kumwabudu Mungu mmoja tu wa haki? Wakati Nabii Ibrahim alipomwona mlezi wake Aazar na kaumu yake wametopea kwenye shirki, alijitenga na imani yao na kuwatangazia kuwa, mimi ninamwabudu Muumba wangu tu, ambaye ni Mungu mmoja wa pekee. Namwomba aniongoze kwenye njia sahihi na ninajua hatoniacha mkono. Nabii Ibrahim AS alifanya kila aliloweza kuhakikisha kalima na neno la tauhidi linasimama na kubakia milele duniani. Kwa hivyo mapambano yake dhidi ya shirki na kuabudu masanamu na kulingania wito wa tauhidi na imani ya Mungu mmoja pekee wa haki ni suna na mwenendo unaotambulika kama kumbukumbu aliyoiacha Nabii huyo mteule, na Mitume waliofuatia baada yake nao pia waliiendeleza na kuidumisha. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mfungamano na uhusiano wa kikaumu, kikabila au hata kichama usiwe na taathira hasi kwetu katika kuchagua itikadi na njia ya maisha na kutufanya tushindwe kuitambua na kuifuata haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, akili inahukumu kwamba, Mola aliyemuumba mwanadamu hawezi kufanya hivyo kisha akamwacha kama alivyo pasi na kumwekea nyenzo na njia ya kuutambua uongofu kupitia akili yake mwenyewe na wahyi. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, inatupasa tujitahidi kuanzisha mwenendo na mafundisho mema katika familia na jamii ili kuifanya njia ya haki iendelee na kudumu baada yetu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 899 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuepushe na kila aina ya shirki, kubwa na ndogo, ya dhahiri na iliyojificha na atufishe katika njia na imani ya tauhidi. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/