Sura ya Az-Zukhruf, aya ya 29-35 (Darsa ya 900)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 900 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 29 na 30 za sura hiyo ambazo zinasema:
بَلْ مَتَّعْتُ هَٰؤُلَاءِ وَآبَاءَهُمْ حَتَّىٰ جَاءَهُمُ الْحَقُّ وَرَسُولٌ مُّبِينٌ
Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ikawafikia Haki na Mtume anaye bainisha.
وَلَمَّا جَاءَهُمُ الْحَقُّ قَالُوا هَٰذَا سِحْرٌ وَإِنَّا بِهِ كَافِرُونَ
Na ilipo wafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na sisi hakika tunaukataa.
Utaratibu wa Allah katika kuamiliana na waja wake ni kutimiza kwanza dhima aliyojiwekea juu yao. Bila ya watu kufikiwa kwanza na wito wa haki, Mwenyezi Mungu hawasaili na kuwaadhibu. Washirikina wa Makka, nao pia hawakutafautishwa na watu wengine katika hilo. Kwa hiyo Allah SWT alimteua Mtume katika umma huo wa Waarabu ili waweze kuyafahamu kwa uwazi kabisa maneno yake na kuuelewa sawasawa wito wa haki. Lakini kama zilivyokuwa umma nyingine nyingi, wakati walipofikishiwa wito wa haki, akthari yao walisimama kuupinga; na badala ya kuikubali haki, wakaamua kumtuhumu mlinganiaji wa haki kwamba ni mchawi na hawakuwa tayari kusilimu na kumwamini. Lakini pamoja na hayo, Mwenyezi Mungu hakuacha kuwateremshia neema za kimaada watu hao na kuwapa muhula wa kuutumia ili kujirekebisha makosa yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, yote yaliyoteremshwa na Allah ni haki tupu; na kama mwanadamu ataweka kanuni za kukabiliana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu, kanuni hizo ni batili hata kama zitafuatwa na akthari ya watu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, watu kuwa katika uneemevu wa mali na utajiri si hoja ya kuonyesha kwamba wako kwenye haki; bali si hasha ukawa ni muhula na fursa ya kuwatahini waliyopewa na Allah. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, wakati mtu anapofikia hatua ya kuifahamu haki, huwa ameshatimiziwa dhima na Mola; hivyo kisingizio chochote atakachotoa ili kuipa mgongo haki kitakuwa ni ishara ya ukafiri na kuipiga vita haki.
Tunaendeleza darsa yetu kwa aya ya 31 na 32 za sura yetu ya Az-Zukhruf zisemazo:
وَقَالُوا لَوْلَا نُزِّلَ هَٰذَا الْقُرْآنُ عَلَىٰ رَجُلٍ مِّنَ الْقَرْيَتَيْنِ عَظِيمٍ
Na walisema: Kwa nini Qur'ani hii haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii?
أَهُمْ يَقْسِمُونَ رَحْمَتَ رَبِّكَ ۚ نَحْنُ قَسَمْنَا بَيْنَهُم مَّعِيشَتَهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۚ وَرَفَعْنَا بَعْضَهُمْ فَوْقَ بَعْضٍ دَرَجَاتٍ لِّيَتَّخِذَ بَعْضُهُم بَعْضًا سُخْرِيًّا ۗ وَرَحْمَتُ رَبِّكَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ
Kwani wao ndio wanao gawa rehema za Mola wako Mlezi? Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wenginewe wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya.
Aya hizi zinaashiria kisingizio kingine walichokuwa wakitoa washirikina waliposema: kama ingekuwa achaguliwe Mtume miongoni mwetu, basi ingepasa awe ni mmoja wa watu wakubwa wa mji huu wa Makka au T'aif; si mtu ambaye utotoni mwake alikuwa yatima na mtu aliyemlea ni babu yake na hana utajiri wala umakinikaji wa maisha ya kidunia. Wao wakidhani kwamba Mtume, kama walivyo wakuu wa makabila, inapasa naye pia awe mtu maarufu mwenye mamlaka, utajiri na hadhi ya kijamii; ambaye watu wote wa kabila lake wanamtii na kumfuata yeye. Hali ya kuwa, mtu anayestahiki kubeba jukumu la Utume ni yule aliyefikia ukamilifu wa kiutu, mwenye mwenendo safi, matendo mema na mkweli wa kauli; ni mtu ambaye amepambika pia kwa sifa maalumu kama urazini na uelewa, ukarimu na ushujaa na mwenye kuyafahamu mateso na machungu ya wanyonge na wanaodhulumiwa. Katika zama zote za historia, hivi ndivyo walivyokuwa Mitume wote wa Mwenyezi Mungu. Kisha aya zinaendelea kueleza kwa kuhoji: kwani mamlaka ya kuamua nani awe Mtume, yako mikononi mwa watu, kwamba Mwenyezi Mungu ampe Utume yeyote yule wanayemtaka wao; na yeyote wasiyemtaka, Mwenyezi Mungu asimpe jukumu na masuulia hayo? Yeye Allah SWT ni Mwelewa wa batini za waja wake, na Mjuzi zaidi kuliko mtu yeyote, wa kutambua ni nani anafaa na kustahiki kubeba jukumu hilo na nani hana ustahiki na hafai kwa kazi hiyo. Katika masuala ya kidunia pia, tofauti mbalimbali zionekanazo kwa watu zinatokana na hekima ya Allah. Ukweli ni kwamba, laiti kama watu wote wangekuwa na kiwango sawa cha uhodari, kipaji na uwezo wa kimwili na kiakili, mfumo wa masuala ya jamii ungeporomoka. Mwenyezi Mungu amewaumba watu wakiwa wanatafuatiana kwa uwezo wa kiakili na kimwili ili kila mmoja awe na hamu na uwezo wa kufanya jambo fulani; na kwa kupitia jambo hilo, atoe mchango wa huduma kwa watu. Na mkabala wake, watu wengine pia wachangie mambo mengine kukidhi mahitaji yake yeye. Na sababu ni kwamba, uendeshaji maisha unawezekana tu kwa njia ya kusaidiana na kila mmoja kutoa huduma fulani kwa mwenzake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mbele ya macho ya watu wengi, ukubwa, huwa unatokana na utajiri, madaraka na umarufu; lakini mbele ya Allah SWT vigezo hivyo havina thamani yoyote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, neema za kimaada na kimaanawi ni ishara ya rehma za Mwenyezi Mungu kwa watu; na yote mawili ni at'iya na majaaliwa ya Mola. Sasa kama maisha yao watu na riziki zao zinagawanywa baina yao kulingana na hikma ya Mwenyezi Mungu, vipi wao wanatarajia Utume, ambalo ni suala la kimaanawi liwe kwenye mamlaka yao? Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kubaki kwa jamii na kuwa na uhai wa kweli, kunategemea mashirikiano ya pande mbili ya watu wake na kutumiwa vipaji, ustadi na uwezo wa aina tofauti wa kimwili na kiakili wa watu hao wa jamii husika. Na kwa hivyo tofauti za kimwili na kiakili za watu wa jamii zimewekwa, ili kujenga moyo wa kusaidiana, na kila mmoja kukidhi mahitaji ya mwingine; si kwa watu kujivuna na kujiona, wakawadharau na kuwadunisha wenzao.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 33 hadi ya 35 ambazo zinasema:
وَلَوْلَا أَن يَكُونَ النَّاسُ أُمَّةً وَاحِدَةً لَّجَعَلْنَا لِمَن يَكْفُرُ بِالرَّحْمَٰنِ لِبُيُوتِهِمْ سُقُفًا مِّن فِضَّةٍ وَمَعَارِجَ عَلَيْهَا يَظْهَرُونَ
Na lau isinge kuwa watu watakuwa kundi moja tungeli wajaalia wanao mkufuru Mwingi wa rehma wana nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao pia wanazo pandia,
وَلِبُيُوتِهِمْ أَبْوَابًا وَسُرُرًا عَلَيْهَا يَتَّكِئُونَ
Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyo egemea juu yake,
وَزُخْرُفًا ۚ وَإِن كُلُّ ذَٰلِكَ لَمَّا مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۚ وَالْآخِرَةُ عِندَ رَبِّكَ لِلْمُتَّقِينَ
Na mapambo. Lakini hayo si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia tu, na Akhera iliyoko kwa Mola wako Mlezi ni ya wenye kumchamngu.
Katika aya zilizopita yaliashiriwa maneno waliyosema washirikina kwamba, kwa nini Qur'ani haikuteremshwa kwa mtu mwenye mali, hadhi na mamlaka? Aya tulizosoma zinasema: kwa Mwenyezi Mungu, mambo hayo hayana hadhi wala thamani yoyote, hata hilo lifanywe kwa kufuata msingi huo. Mbele ya Allah SWT usafi wa batini na uchaMungu ndio mambo yenye thamani; na Yeye Mola anawapima waja wake na matendo yao kwa kutumia vigezo hivyo. Dhahabu, fedha na aina nyinginezo za vito na vitu vya mapambo vinavyoteka macho ya watu na kuwafanya wavipaparikie, havina thamani mbele ya Mwenyezi Mungu. Kama kufaidika makafiri na neema hizo za kimaada kusingehofiwa kuwa kutawafanya watu wenye imani nyepesi na wapenda dunia wapoteze imani zao na kumkufuru Mola wao, basi Yeye Mwenyezi Mungu angelizifanya nyumba za makafiri na vitu vyao viwe vya dhahabu na fedha. Wangekuwa na nyumba za ghorofa kadhaa zenye dari za fedha na ngazi za kupandia kwendea juu; si hayo tu, wangekuwa na makasri ya fahari, yenye milango kadhaa wa kadhaa pamoja na vitanda vya kuegemea wakiwa ndani yake. Mwenyezi Mungu angewaandalia pia anuai za mapambo yenye nakshi za kuvutia ili kuhakikisha maisha yao ya raha na starehe za kimaada yamekamilika kwa kila namna na hali. Hata hivyo, kama Allah SWT angelifanya hayo, ingekuwa ni kwa ajili ya kuwaacha washughulishwe na kujiburudisha na mambo hayo duni ya kimaada, ili kuhitimisha maisha yao ya dunia; na ili watu wote watambue kwamba, kipimo cha thamani na shakhsia ya mtu si vito na mapambo ya kimaisha. Na kwa kumalizia, aya zinasema: lakini vyote hivyo ni starehe tu za kupita za maisha ya kimaada ya dunia; na akhera na malipo yake ya milele ni kwa ajili ya wale waliomcha Mola wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, watu wengi akili zao zinaishia kwenye macho yao. Wanapowaona makafiri wanaishi maisha ya raha, starehe na uneemevu, hudhani kwamba njia ya maisha wanayofuata watu hao ndiyo sahihi na wanaishia kuwafuata wao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, thamani ya mtu inatokana na nafsi yake mwenyewe alivyo, si nyumba na gari yake, wala vitu vyake vingine vyovyote vya mapambo na fahari. Kwa maneno mengine ni kwamba, thamani ya kila mtu inategemea vile nafsi na batini yake ilivyopambika kwa ukamilifu wa kiakhlaqi na kiutu; si kwa vitu anavyomiliki nje katika dhahiri yake. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, ikiwa hapa duniani tutamcha Mwenyezi Mungu na kufuata njia yake iliyonyooka, Siku ya Kiyama, Yeye Mola atakwenda kutupa na kutuneemesha kwa yaliyo bora kuliko walivyo navyo matajiri hapa duniani, ambayo hayawezi kulinganishwa na chochote kile cha dunia hii ya kupita. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 900 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe utajiri wa nyoyo wa kukinai na kutosheka kwa aliyotukadiria na kutouza utu na imani zetu kwa sababu ya neema za kimaada za dunia. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/