Sura ya Az-Zukhruf, aya ya 36-42 (Darsa ya 901)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 901 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 36 na 37 za sura hiyo ambazo zinasema:
وَمَن يَعْشُ عَن ذِكْرِ الرَّحْمَٰنِ نُقَيِّضْ لَهُ شَيْطَانًا فَهُوَ لَهُ قَرِينٌ
Anayeifanyia upofu dhikri ya Mwingi wa rehema tutamwekea Shet'ani kuwa ndiye rafiki yake.
وَإِنَّهُمْ لَيَصُدُّونَهُمْ عَنِ السَّبِيلِ وَيَحْسَبُونَ أَنَّهُم مُّهْتَدُونَ
Na hakika wao wanawazuilia Njia, na wenyewe wanadhani kuwa wameongoka.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia watu wanaopima kila kitu kwa mtazamo wa kimaada, wakapaparikia mali na utajiri na kushughulishwa na anasa na starehe za dunia; wakati waumini wa kweli, huwa wanafikiria akhera na wala nafsi zao hazishughulishwi na starehe na mapambo ya dunia. Aya tulizosoma zinasema: katika athari zenye madhara na hasara ya kughiriki kwenye mambo ya kimaada na kuikumbatia sana dunia ni mtu kughafilika na kumsahau Mwenyezi Mungu. Na kutokana na kughafilika huko, mwanadamu hutawaliwa na shetani, akamburuza na kumuelekeza kokote atakako. Hayo ndiyo matokeo ya kutarajia, pale mtu asipomtaja wala kukumbuka Mwenyezi Mungu. Kwa maneno mengine ni kwamba, moyo wa mwanadamu, ima ni faragha ya Allah SWT au faragha ya shetani. Mtu asipomkumbuka Mwenyezi Mungu, akatekwa na anasa na mapambo ya dunia na kutumbukia kwenye dimbwi la madhambi, ndipo hutawaliwa na kudhibitiwa na shetani. Hapo tena shetani huwa ndiye mwenza wake; na Mwenyezi Mungu hawi na nafasi tena. Shetani na fikra za kishetani huwazungukia kila upande watu wenye sifa hiyo na kuwafanya washindwe kuifuata njia ya Mwenyezi Mungu. Na hata pale watu hao wanapotaka kurejea kwenye njia ya haki, mashetani huwawekea vizuizi ili wasirudi katika njia iliyonyooka. Huwapambia njia ya upotofu, mpaka ikafika hadi macho, masikio na nyoyo zao zikaingia upofu na uziwi wa kutoisikia na kuiona haki na ukweli; wakadhani kwamba hivyo walivyo, ndio wako kwenye uongofu na yote wayafanyayo ni sahihi na ya sawa. Watu wa aina hii huwadhani na kuwafikiria wenzao wasiokuwa wao kuwa wakosa na wapotofu. Ni wazi kwamba, wakati mtu anapofikia hatua hiyo, huwa hawezi kuona kosa katika ayafanyayo, hata limfanye afikirie kujirekebisha na kurudi kwenye mstari wa njia iliyonyooka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, yeyote anayejitenga na Mwenyezi Mungu hata akiwa ni Muislamu, lakini akawa hasali wala haijali Qur'ani, huwa kwa hakika amejiweka mbali na utajo wa Allah na kujiandalia mazingira ya kutawaliwa na kuhodhiwa na shetani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, moyo wa mwanadamu haubakii mtupu; ima utakuwa faragha ya Mola Rahmani au ya shetani. Asipokuwepo Mwenyezi Mungu, nafasi yake huchukuliwa na shetani. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, lililo baya zaidi ya kufanya kosa, ni mtu kutoliona kosa lake na kudhani kwamba njia anayofuata ndiyo sahihi.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 38 na 39 ambazo zinasema:
حَتَّىٰ إِذَا جَاءَنَا قَالَ يَا لَيْتَ بَيْنِي وَبَيْنَكَ بُعْدَ الْمَشْرِقَيْنِ فَبِئْسَ الْقَرِينُ
Hata atakapo tujia atasema: Laiti ungeli kuwako baina yangu na wewe umbali baina ya mashariki na magharibi. Rafiki mwovu ulioje wewe!
وَلَن يَنفَعَكُمُ الْيَوْمَ إِذ ظَّلَمْتُمْ أَنَّكُمْ فِي الْعَذَابِ مُشْتَرِكُونَ
Na kwa kuwa mlidhulumu, haitakufaeni kitu leo kwamba nyinyi mnashirikiana katika adhabu.
Aya hizi zinaashiria hatima inayowapata wale wanaoghafilika na kumsahau Mwenyezi Mungu hapa duniani na kueleza kwamba: kujiweka mbali huko na Mwenyezi Mungu huendelea mpaka mtu anafumba jicho na kwenda kuhudhurishwa kwenye uwanja wa hukumu Siku ya Kiyama. Huko macho yatafungukiwa na hakika ya mambo na mtu kubaini balaa alilosababishiwa na shetani. Hapo atatamani alipokuwa duniani asingeukubali urafiki wa shetani na kuwa na usuhuba naye. Atasema wakati huo: Ya laiti kungekuwepo na masafa baina yangu na yako umbali wa mashariki na magharibi! Ulikuwa mwenza na rafiki mbaya uliyoje! Wewe uliyafanya mabaya na maovu yaonekane mema na mazuri; na njia ya upotofu ionekane ya uongofu na kunifanya niikingeuke njia ya haki. Ni wazi kwamba kutamani kwao huko juu ya kutengana na kubaidiana moja kwa moja na shetani kutageuka majuto; na majuto ni mjukuu, kwani wakati huo hayatakuwa na faida yoyote. Mwisho wa watu kama hao ni kuchanganywa na kuwa pamoja na shetani kwenye adhabu motoni, kama walivyokuwa wameridhia kusuhubiana naye na kumtii hapa duniani. Naam, hivyo ndivyo itakavyokuwa. Kiyama ni mithili ya kioo kinachoakisi yaleyale ya duniani. Waliokuwa marafiki wa lolote duniani, watakuwa pamoja pia akhera. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tujihadhari na tuwe makini hapa duniani katika kuchagua mtu wa kumfanya rafiki yetu ili huko akhera tusije kuishia kujilaumu na kubaki na majuto. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, adhabu ya moto wamewekewa wote wawili, watu na mashetani; hivyo watu wa motoni watakuwa na makazi mamoja na mashetani. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, dhulma, haifanyi mtu kuwafanyia wenzake tu, bali kujiweka mbali na Mwenyezi Mungu ni dhulma kubwa kabisa anayoifanyia mtu nafsi yake mwenyewe, kwa sababu humtumbukiza kwenye dhalala na upotofu hapa duniani na kuishia kwenye adhabu kali ya moto huko akhera.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 40 hadi 42 ambazo zinasema:
أَفَأَنتَ تُسْمِعُ الصُّمَّ أَوْ تَهْدِي الْعُمْيَ وَمَن كَانَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ
Je! Unaweza kumsikilizisha kiziwi, au kumuongoa kipofu na aliyemo katika upotofu ulio wazi?
فَإِمَّا نَذْهَبَنَّ بِكَ فَإِنَّا مِنْهُم مُّنتَقِمُونَ
Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi kwao.
أَوْ نُرِيَنَّكَ الَّذِي وَعَدْنَاهُمْ فَإِنَّا عَلَيْهِم مُّقْتَدِرُونَ
Au tutakuonyesha tuliyo waahidi. Nasi bila ya shaka tuna uweza juu yao.
Aya hizi zinamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba, wale ambao hawako tayari kuiona na kuisikiliza haki, japokuwa macho na masikio yao ya kimaumbile ni mazima, lakini uono na usikivu wao wa batini umefungika. Kwa hivyo huwezi kuwasikilizisha maneno yako, kuwafanya wauone ukweli kwa kuwatoa kwenye upotofu na kuwaelekeza kwenye njia ya uongofu. Kuna tofauti baina ya mtu aliyelala na ajifanyaye amelala. Wa mwanzo ukimwamsha mara kadhaa huamka, lakini wa pili, hata umpigie kelele mara ngapi hatotikisika wala kukuitika. Baadhi ya watu huwa wameghiriki na kuzama kwenye madhambi, mpaka wanafika hadi ya kuchukia hata kusikia jina la Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wanaposikia mafundisho ya dini na ujumbe wa masuala ya kiroho na kimaanawi, hali zao hutibuka na kutafirika. Ni wazi kwamba watu wa aina hii hawajibakishii tena fursa yoyote ya kutubia na kurejea kwenye njia ya uongofu, hata kama atakayewaongoza na kuwaonyesha uongofu huo atakuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ambaye ni mlinganiaji bora kabisa; na matendo yake ni ushahidi wa kuthibitisha ukweli wa Utume wake. Inadi, ubishi na ukaidi wa aina hiyo dhidi ya haki hautakuwa na tija na matokeo mengine ghairi ya kughadhibikiwa na kufikwa na adhabu ya Allah hapa duniani na akhera, iwe ni katika zama za uhai wa Mtume mwenyewe au baada ya kutawafu kwake. Vyovyote iwavyo, watu hao hawana pa kukimbilia. Kwa sababu Mwenyezi Mungu SWT ameuhodhi ulimwengu mzima na hakuna yeyote awezaye kutoka nje ya mamlaka yake yasiyo na mpaka wala kikomo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ikiwa mtu hatokuwa na utayarifu wa kuikubali haki, maneno na wito atakaolinganiwa hata na waja safi na wateule wa Allah, ambao ni Mitume wake hautakuwa na taathira kwake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kama shetani atamtawala mtu; moyo na roho ya mtu huyo huingia upofu na uziwi zikashindwa kuiona na kuisikia haki. Vilevile inatubainikia kutokana na aya hizi kwamba washirikina wasidhani kuwa madamu Mtume yuko duniani wao hawataadhibiwa, au kama atakuwa hayuko tena, amesharejea kwa Mola hakutakuwa na adhabu tena. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 901 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/