Sura ya Az-Zukhruf, aya ya 43-48 (Darsa ya 902)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 902 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 43 na 44 za sura hiyo ambazo zinasema:
فَاسْتَمْسِكْ بِالَّذِي أُوحِيَ إِلَيْكَ ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ
Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika wewe uko kwenye Njia Iliyo Nyooka.
وَإِنَّهُ لَذِكْرٌ لَّكَ وَلِقَوْمِكَ ۖ وَسَوْفَ تُسْأَلُونَ
Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja ulizwa.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia inadi na ukaidi wa wapinzani wa haki na kukataa kwao maneno ya Bwana Mtume SAW. Aya hizi zinamhutubu mtukufu huyo ya kwamba: njia unayofuata wewe na yale unayoyalingania ni sahihi kabisa, wala hayana doa wala toa au lolote lile la walakini na upotofu; kwa hivyo kutokubali wapinzani si hoja ya kuutia ila ukweli wa Utume wako. Endelea kushika njia unayofuata kwa uzito kamili kulingana na anayokuamuru Mola wako na wahyi unaoshushiwa; na tambua kwamba uko kwenye njia iliyonyooka na hiyo ndio njia ya haki. Hakika lengo hasa la kuteremshwa Qur'ani ni kuwaamsha wanadamu na kuwatambulisha majukumu na masuulia yao. Kwa hivyo inapasa umati wako ushikamane na Qur'ani na kujitahidi kila wakati kuyakumbuka na kuyafuata mafundisho yake. Sababu ni kuwa, Kitabu hiki kinalingania mambo yanayoendana na akili, fitra na maumbile ya mwanadamu na kumwokoa kiumbe huyo na hatari ya kutumbukia kwenye lindi la mghafala na kujisahau. Moja ya mambo ambayo watu wengi tunaghafilika nayo ni mahakama ya Siku ya Kiyama. Katika mahakama hiyo, watu wote watahojiwa na kusailiwa na watapaswa kuwajibika kwa matendo na amali zao na pia juu ya namna walivyoijali Qur'ani na kutekeleza mafunzo na mafundisho yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, njia pekee ya uhakika na isiyo na shaka ni kushikamana na Qur'ani na mafundisho yake, kitabu ambacho Allah SWT ametupa dhamana na hakikisho la usahihi wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mbali na Qur'ani, Sunna na Sira ya Bwana Mtume Muhammad SAW navyo pia ni hoja na marejeo kwetu; na Mwenyezi Mungu ametilia mkazo kwamba njia ya Mtume wake huyo mteule ni ya kweli na ya haki. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Siku ya Kiyama, Waislamu wataulizwa na kusailiwa kuhusu Qur'ani na kwamba, kwa kiwango gani walishikamana nacho na kukifuata kitabu hicho kitukufu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 45 ambayo inasema:
وَاسْأَلْ مَنْ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رُّسُلِنَا أَجَعَلْنَا مِن دُونِ الرَّحْمَٰنِ آلِهَةً يُعْبَدُونَ
Na waulize Mitume wetu tulio watuma kabla yako: Je! Tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Mwingi wa rehema (Rah'mani)?
Washirikina wa Makka walikuwa wakijitambulisha kwamba, wao wanatokana na kizazi cha Nabii Ibrahim na Nabii Ismail (as). Wakawa kila mwaka wanatekeleza baadhi ya amali za kiibada kama Hija na kuipa heshima Nyumba Tukufu ya Allah ya Al Kaaba; lakini wakati huohuo waliendelea kuabudu masanamu. Kwa hivyo katika kuikana ibada ya kuabudu masanamu na kuonyesha kuwa itikadi hiyo ya Washirikina ni batili, aya tuliyosoma inamhutubu Bwana Mtume SAW ya kwamba: waulize wafuasi wa Mitume waliopita, je Mitume hao waliwaambia watu: viabuduni vitu vingine ghairi ya Mwenyezi Mungu, Ar-Rahman?! Aya hii inawaambia Waislamu wawaulize wafuasi wa Mitume waliotangulia kama Mwenyezi Mungu alitoa amri hiyo, kwamba tumwabudu asiyekuwa Yeye? Kama Mwenyezi Mungu ametoa amri hiyo, sisi hatuna upinzani. Kwa sababu sisi tunatii amri yake Yeye Allah SWT na lolote asemalo tunalitekeleza bila kuhoji hivi wala vile. Kwa kuibua suali hili, aya hii inakusudia kutilia mkazo nukta kwamba, Mitume wote wa Mwenyezi Mungu walilingania Tauhidi; na kila mmoja wao alikabiliana kwa uwezo wake wote na shirki na ibada ya kuabudu masanamu. Na kwa hivyo hatua ya Bwana Mtume SAW ya kupinga kuabudu masanamu na kulingania watu tauhidi si jambo jipya, bali amefufua na kuendeleza mwenendo wa kudumu ulioanzishwa na kufuatwa na Mitume waliomtangulia. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, mhimili wa dini za Mwenyezi Mungu na msingi wao wa pamoja ni Tauhidi; na hilo ni jambo ambalo Qur'ani na Bwana Mtume SAW wamelitilia mkazo pia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, haijuzu kuabudu kitu chochote au mtu yeyote badala ya Mwenyezi Mungu au pamoja na Yeye Mola. Wa kuabudiwa ni Yeye Allah SWT peke yake mwenye sifa ya Ar-Rahman.
Zifuatazo sasa ni aya za 46 na 47 ambazo zinasema:
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ بِآيَاتِنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ فَقَالَ إِنِّي رَسُولُ رَبِّ الْعَالَمِينَ
Na hakika tulimtuma Musa kwa Ishara zetu aende kwa Firauni na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote!
فَلَمَّا جَاءَهُم بِآيَاتِنَا إِذَا هُم مِّنْهَا يَضْحَكُونَ
Lakini alipo wajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka.
Aya hizi zinasimulia machache kuhusu Nabii Musa AS na kueleza kwamba, mbali na kaumu yake ya Bani Israil, jukumu jengine ambalo alipewa Mtume huyo, lilikuwa ni kumwendea Firauni na kumlingania wito wa Laa ilaha illaLlah. Na katika kufanya hivyo, alitakiwa aionyeshe mbele ya Firauni mwenyewe, maashrafu pamoja na washauri wake, miujiza aliyopewa na Mwenyezi Mungu ili iwe hoja na ushahidi wa kuthibitisha ukweli wa Utume wake. Utume ambao wito wake umetoka kwa Mola wa walimwengu wote, kinyume na Firauni aliyekuwa akijidai na kujinadi kwamba yeye ni 'mungu' anayewaendeshea watu mambo yao na kwa hivyo inapasa wote watii amri zake yeye. Wakati Nabii Musa alipokwenda kwenye kasri la utawala wa Firauni ili kumfikishia wito wa uongofu, alivaa mavazi ya kawaida kabisa ya sufu. Akamuelekea Firauni na wakuu wa kasri la utawala wake na kuwaeleza kwamba, yeye ametumwa na Mwenyezi Mungu awaongoze na kuwaelekeza kwenye njia ya uongofu. Lakini wao walimdhihaki na kumcheka kwa kejeli. Sababu ni kwamba, kama walivyokuwa watu wa Makka, wao pia walikuwa wakidhani, kama Mwenyezi Mungu anataka kumteua mtu awe Mtume wake, atamchagua mmoja wa vinara, matajiri na maashrafu wa kaumu ya watu, na si mtu asiye na umaarufu wowote na ambaye aliwahi kuwa mtoto wa kulea wa Firauni. Yaani iweje mtu kama huyo, leo aje kudai kwamba anataka kumwongoza na kumuonyesha uongofu Firauni na kaumu yake! Alaa kulli hal, huu ndio mwenendo wa wale wote wanaotakabari kwa nguvu za madaraka, wakati wanapofikiwa na viongozi wateule wa dini ya Allah, yaani kuufanyia wito wao kejeli na stihzai. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mbali na watu wa kawaida, Mitume walikuwa wakiwaendea pia watawala; kwa sababu bila kurekebishwa watawala, masuala ya kijamii hayawezi kurekebishika. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Mitume walikuwa na ukamilifu wa kinafsi na wa sifa aali na tukufu za kiakhlaqi; na walikuja pia na miujiza ili kuthibitisha ukweli wa Utume wao na kuwaondolea watu shaka ya aina yoyote ile. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mbinu ya wapinzani ni kudhihaki, kukejeli na kudhalilisha watu wa haki. Wao hawana mantiki wala hoja yoyote.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 48 ambayo inasema:
وَمَا نُرِيهِم مِّنْ آيَةٍ إِلَّا هِيَ أَكْبَرُ مِنْ أُخْتِهَا ۖ وَأَخَذْنَاهُم بِالْعَذَابِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ
Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko nyingineyo. Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee.
Aya hii inaeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizotangulia na kubainisha kwamba: ili kumfanya Firauni na watu wake wasiwe na kisingizio chochote cha kutoa, tuliwaonyesha miujiza kadha wa kadha, ambao kila mmoja ulikuwa na uzito mkubwa zaidi na ishara za wazi zaidi kuliko wa kabla yake, ili wajivue vazi la kiburi na ghururi walilokuwa wamejivika; na kama walikuwa kweli wanataka kuitambua haki, iwabainikie. Lakini kadri tulivyowaongezea miujiza, ndivyo inadi, ubishi na ukaidi wao ulivyoongezeka pia, mpaka tukaamua, mbali na miujiza hiyo tuwatahini kwa misukosuko na mabalaa ya kimaonyo, kama ukame, njaa na mengineyo, kwamba huenda asaa watazinduka na kuifuata njia ya haki. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, katika kutimiza dhima yake kwa watu kwa ajili ya kuwapa uthibitisho na ushahidi, Mwenyezi Mungu Mtukufu hatosheki na hoja na ushahidi mmoja tu, bali huwapelekea pia miujiza na mambo mbalimbali ya kuwatanabahisha. Hii yenyewe ni alama ya rehma na uraufu wa Allah kwa waja wake. Aidha aya hii inatutaka tujue kuwa, baada ya watu kutimiziwa dhima ya kuonyeshwa hoja na miujiza, kinachofuatia ni kutiwa adabu na kuonjeshwa adhabu ya duniani, kwamba huenda maonyo na idhari hizo zitawafanya wajirudi na kuacha njia ya upotofu wanayofuata. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 902 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/