May 24, 2023 14:39 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 904 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 57 na 58 za sura hiyo ambazo zinasema:

وَلَمَّا ضُرِبَ ابْنُ مَرْيَمَ مَثَلًا إِذَا قَوْمُكَ مِنْهُ يَصِدُّونَ

Na alipo pigiwa mfano Mwana wa Maryam, watu wako waliupiga ukelele.

وَقَالُوا أَآلِهَتُنَا خَيْرٌ أَمْ هُوَ ۚ مَا ضَرَبُوهُ لَكَ إِلَّا جَدَلًا ۚ بَلْ هُمْ قَوْمٌ خَصِمُونَ

Wakasema: Miungu yetu ni bora au yeye? Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi!

Kwa mujibu wa mapokezi ya historia, washirikina wa Makka walipotaka kutafuta kisingizio cha kuhalalisha na kutetea shirki yao ya kuabudu masanamu, walitoa hoja ya kufananisha upotofu wao huo na matendo ya Wakristo; na wakawa wanamwambia Bwana Mtume SAW ya kwamba: Wakristo pia walikuwa wakimwabudu Masih, ambaye amezaliwa na mwanamke aitwaye Maryam. Kwa hivyo kama sisi tunafanya makosa, na wao pia wanakosea; na ikiwa kama usemavyo wewe, sisi na tunavyoviabudu tutatiwa motoni, basi Masih pia itapasa akatiwe motoni, kwa sababu yeye pia amekuwa mwabudiwa. Ulinganishaji huo usio na uhusiano wa kuyafananisha masanamu na Nabii Isa Masih (as), na ambao ubatili wake uko wazi kabisa, ulifanywa na washirikina kwa ajili ya kufanya ubishani tu na kutaka kumpinga Bwana Mtume SAW. Badala ya kuacha mwenendo na matendo yao ya upotofu, waliyatafutia kisingizio cha kuyahalalisha na kuyatetea, kwa kuyalinganisha na mwenendo potofu wa watu wengine, fikra batili ambayo, leo hii pia hutumiwa na watu wengi ili kutetea mwenendo na matendo yao potofu. Tukumbushe na kubainisha hapa kwamba, kwa upande wa wanadamu, waabudiwa watakaoingia motoni, ni wale watu ambao walitaka wao wenyewe wafanywe hivyo; kama Firauni, ambaye aliwataka watu wamtii na kumwabudu yeye. Lakini Nabii Isa Masih (as), yeye katu hakuwa tayari kuwa mwabudiwa na alikuwa akilichukia mno jambo hilo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tuzipinge na kuzikosoa kwa hoja na mantiki itikadi zisizo sahihi za watu wengine, badala ya kuzifanyia shere na stihzai. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kufanya mdahalo, mazungumzo na majadiliano kwa ajili ya kuijua haki na ukweli ni jambo linaloshauriwa na kuusiwa na Qur'ani. Lakini mtu kuanzisha mjadala kwa lengo la kutetea mwenendo na matendo yake yasiyo sahihi, na kutaka kutetana na kupingana tu na wenzake, hilo ni jambo lisilofaa.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 59 na 60 ambazo zinasema:

إِنْ هُوَ إِلَّا عَبْدٌ أَنْعَمْنَا عَلَيْهِ وَجَعَلْنَاهُ مَثَلًا لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ

Hakuwa yeye (Isa) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili. 

وَلَوْ نَشَاءُ لَجَعَلْنَا مِنكُم مَّلَائِكَةً فِي الْأَرْضِ يَخْلُفُونَ

Na tungeli penda tungeli wafanya badala yenu Malaika katika ardhi kuwa makhalifa.

Katika aya zilizotangulia tulieleza kuhusu mtazamo potofu wa washirikina wa Makka wa kuyalinganisha masanamu yao na Nabii Isa (as). Aya hizi zinamtetea Mtume huyo mteule kwa kusema: yeye Masih, alikuwa akijitambua kuwa ni mja wa Mwenyezi Mungu; na hakuridhia katu kuabudiwa na Wakristo na akikabiliana vikali na jambo hilo. Nabii Isa (as) alikuwa mwanadamu, ambaye Allah SWT alimtunukia neema teule ya Utume ili awe Nabii wa kaumu ya Bani Israil; na kutokana na kuwa kwake ruwaza na kigezo kilichokamilika cha mja mteule, awe sababu ya wao kuutambua na kuufuata uongofu. Kusema kweli, kila moja ya miujiza aliyokuja nayo Nabii huyo ilikuwa alama ya wazi kabisa ya adhama ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na Utume wake yeye Isa (as). Kwa muda wote alioishi na watu, Nabii Isa aliungama kuhusu kuwa kwake yeye mja wa Mwenyezi Mungu na akawalingania watu wote kumwamini na kumwabudu Mola pekee wa haki. Lakini kwa masikitiko, badala ya Wakristo kumwabudu Mwenyezi Mungu, walimpa utakatifu na kumwabudu yeye Isa Masih (as). Kisha aya zinaendelea kuwahutubu washirikina ya kwamba, ikiwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanakulinganieni kufuata njia sahihi iliyonyooka, si kwa maana kwamba Yeye Allah ni mhitaji wa kuamini na kuabudu kwenu. Kwa sababu ikiwa atataka, anaweza akawaweka ardhini malaika badala yenu; malaika ambao daima na muda wote wanatii na kutekeleza amri za Allah SWT na kumsabihi na kumwabudu Yeye Mola. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kudhihirisha uja na kumwabudu Mwenyezi Mungu ndio njia ya kumtukuza mwanadamu na kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiutu; na Mitume, ndio watu waliofikia daraja ya juu kabisa ya kuwa waja halisi na wa kweli wa Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, japokuwa katika kipindi chote cha historia, Mayahudi wamekuwa wakimpinga Nabii Isa (as) lakini Mtume huyo alitokana na kaumu ya Bani Israil; na kitendo cha Mayahudi cha kumpinga na kumkataa, kilitokana na inadi na ukaidi tu wa watu hao. Halikadhalika, aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, Mwenyezi Mungu ametaka mwanadamu aamini na kuikubali haki kwa hiari na kwa uelewa; vyenginevyo angeweza kuwaleta malaika ardhini, ambao hajawapa hiari ya kuchagua, wakawa muda wote wanamtii na kumwabudu Yeye Mola.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 61 na 62 ambazo zinasema:

وَإِنَّهُ لَعِلْمٌ لِّلسَّاعَةِ فَلَا تَمْتَرُنَّ بِهَا وَاتَّبِعُونِ ۚ هَٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ

 Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. 

وَلَا يَصُدَّنَّكُمُ الشَّيْطَانُ ۖ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ

Wala asikuzuilieni Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu wa dhaahiri.

Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizopita kwa kuashiria sifa nyingine maalumu ya Nabii Isa na kueleza kwamba, yeye mwenyewe Masih (as) ni moja ya alama na ishara za Kiyama. Kwa sababu kuzaliwa kwake na mama pasi na kuwa na baba, ni alama ya uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kuja kuwaumba tena wanadamu Siku ya Kiyama. Muujiza mwingine wa Nabii Isa (as) ulikuwa ni kuwafufua wafu papa hapa duniani. Lakini mbali na hayo, kwa mujibu wa Hadithi za Kiislamu zenye itibari na hata kwa itikadi waliyonayo Wakristo, Nabii Isa atateremka kutoka mbinguni katika Aakhiru-Zaman, ambapo hiyo yenyewe itakuwa ishara ya kukaribia mwisho wa dunia na kujiri kwa Kiyama. Kisha aya zinatilia mkazo uhakika usio na chembe ya shaka wa kutokea kwa Kiyama na kueleza kwamba, katu msiwe na shaka juu ya hilo, kwa sababu kughafilika na Kiyama humfanya mtu atumbukie kwenye lindi la anuai za maasi na upotofu na mwishowe kuishia kwenye adhabu ya Moto. Kwa hivyo shikamaneni na njia ya Mwenyezi Mungu iliyonyooka, njia ambayo imebainishwa na Mitume na ndiyo itakayomuokoa mwanadamu na hatari chungu nzima zinazomnyemelea; na hivyo kupata saada na fanaka ya duniani na akhera. Tab'an mkabala na njia ya Mwenyezi Mungu, kuna njia ya shetani, ambaye anataka kutumia wasiwasi na udanganyifu ili akuzuilieni kufuata njia ya Allah SWT na kufikiria hatima yenu huko akhera ili mpate kuharibikiwa hapa duniani na akhera mnakoelekea. Chimbuko la vitimbi hivyo vya shetani ni chuki na uadui wake wa tokea tangu na tangu alionao dhidi yenu, wa pale alipobaidishwa na kuwekwa mbali na rehma za Mwenyezi Mungu alipokataa kumsujudia baba yenu Adam. Ni hapo ndipo alipoapa kuwa hadi mwisho wa dunia, atafanya kila hila na vitimbi ili awapotoshe wana wa Adam (as). Sasa inakuwaje mnakaa vivi hivi tu mbele ya adui huyo aliyekukamieni, na kumwacha akutieni wasiwasi kila mara ili kukuzuilieni kufuata njia ya haki? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwepo kwa mawalii wa Mwenyezi Mungu pamoja na kauli na matendo yao vinatanabahisha na kumkumbusha mtu juu ya Kiyama na Kufufuliwa viumbe. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mwanadamu anahitaji kigezo na mfano wa kuiga kwa ajili ya kupiga hatua katika njia iliyonyooka. Kwa hivyo inapasa afuate mafunzo na miongozo ya waja safi na wateule wa Mwenyezi Mungu, yaani Mitume, ili aweze kuifahamu na kuishika njia hiyo iliyonyooka. Vyenginevyo, ataishia kutekwa na hawaa na matamanio ya nafsi yake na kuzongwa na ghilba na wasiwasi wa shetani, huku akidhani kwamba yuko kwenye njia iliyonyooka. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, shetani huwa muda wote anamnyemelea na kumvizia mwanadamu, ili kwa kutumia kila njia na mbinu, ajipenyeze ndani ya moyo na nafsi yake na kumzuilia kufuata njia ya haki na iliyonyooka. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 904 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah, azifanye thabiti imani zetu kwa kutulinda na shari ya wasiwasi wa shetani na kutuwafikisha kuishika njia ya haki iliyonyooka, hadi mwisho wa uhai wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/