May 27, 2023 00:01 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 925 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 46 ya al Ah'qaaf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 19 ya sura hiyo ambayo inasema:

وَلِكُلٍّ دَرَجَاتٌ مِّمَّا عَمِلُوا ۖ وَلِيُوَفِّيَهُمْ أَعْمَالَهُمْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ

Na wote watakuwa na daraja zao mbali mbali kwa waliyo yatenda, na ili awalipe kwa vitendo vyao, na wala hawatadhulumiwa.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia makundi mawili ya watu. La kwanza ni la wanaomwamini Allah na kuwafanyia wema na ihsani wazazi wao; na la pili ni la wanaokanusha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na kutojali kuchunga haki za wazazi. Aya hii tuliyosoma inasema: Siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu Mtukufu atawalipa watu wa kila moja kati ya makundi hayo mawili malipo ya thawabu au adhabu kulingana na amali zao; na daraja za malipo hayo zitatafautiana kwa kuzingatia nia na utendaji wao. Kisha aya inaendelea kutilia mkazo uadilifu wa Allah SWT katika mfumo wa utoaji malipo kwa waja na kueleza kwamba, kila mtu atapata malipo kamili ya amali zake na hakuna atakayedhulumiwa kwa kunyimwa hata chembe ya haki yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, majaaliwa na hatima ya kila mtu hapa duniani na huko akhera iko mikononi mwa mtu mwenyewe; na nafasi atakayokuwa nayo mtu Siku ya Kiyama itatokana na nia na amali zake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kupita kwa muda na zama hakutayafanya matendo na amali za mtu zifutike na kutoweka; kwani asili ya kila amali na athari zake zimehifadhiwa kwenye daftari la amali za mja; na Siku ya Kiyama itadhihirika hakika yake kwa ukamilifu. Na ndio utakuwa msingi wa malipo ya thawabu au adhabu atakayolipwa mtu siku hiyo.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 20 ambayo inasema:

وَيَوْمَ يُعْرَضُ الَّذِينَ كَفَرُوا عَلَى النَّارِ أَذْهَبْتُمْ طَيِّبَاتِكُمْ فِي حَيَاتِكُمُ الدُّنْيَا وَاسْتَمْتَعْتُم بِهَا فَالْيَوْمَ تُجْزَوْنَ عَذَابَ الْهُونِ بِمَا كُنتُمْ تَسْتَكْبِرُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَبِمَا كُنتُمْ تَفْسُقُونَ

Na siku watakapowekwa mbele ya Moto waliokufuru (waambiwe): Nyinyi mlitwaa vitu vyenu vizuri katika uhai wa duniani, na mkastareheshwa navyo. Basi leo ndio mnalipwa adhabu ya fedheha kwa mlivyo kuwa mkitakabari katika ardhi bila ya haki, na kwa sababu mlikuwa mkifanya ufuska. 

Rehma, ukarimu na uraufu wa Allah SWT kwa waja wake hapa duniani unajumuisha makundi yote mawili ya watu, yaani waumini na makafiri; na Yeye Mola hawanyimi neema zake za kimaada na za vitu vya dunia hata wanaomkufuru na wanaomshirikisha pia. Aya tuliyosoma inasema: makafiri na wafanya maovu walijistarehesha kiasi cha kutosha kwa neema za Mwenyezi Mungu na raha za kimaada hapa duniani na hawakunyimwa chochote walichotaka kufanya; lakini Siku ya Kiyama, ambayo ni siku ya malipo, rehma zisizo na ukomo za Allah SWT zitawahusu waja safi na wema peke yao. Ni jambo la yakini kwamba, wale ambao hapa duniani walisimama kuipiga vita haki na hawakuwa tayari kuikubali na kuifuata kutokana na inadi, ukaidi na kiburi, watafikwa na adhabu kali. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kunufaika na neema za Mwenyezi Mungu hapa duniani hakushurutishwi na kumwamini Yeye Mola. Riziki ni kitu ambacho Allah SWT amewakadiria viumbe wake wote wakiwemo wanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kujigamba na kutakabari kunamuelekeza mtu kwenye ufasiki na uovu na kumkengeusha na njia ya haki. Halikadhalika aya hii inatuelimisha kwamba, udhalili na unyonge Siku ya Kiyama, ni adhabu itakayowafika watu waliokuwa wakitakabari hapa duniani kwa kujiona wana nguvu, utukufu na hadhi ya juu kuliko wenzao.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 21, 22 na 23 za sura yetu ya al Ah'qaaf ambazo zinasema:

وَاذْكُرْ أَخَا عَادٍ إِذْ أَنذَرَ قَوْمَهُ بِالْأَحْقَافِ وَقَدْ خَلَتِ النُّذُرُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّهَ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ

Na mtaje ndugu wa kina A'di, alipo waonya watu wake kwenye vilima vya mchanga. Na kwa yakini waonyaji wengi walitokea kabla yake na baada yake kuwaambia: Msimuabudu isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi nakukhofieni adhabu ya siku iliyo kuu. 

قَالُوا أَجِئْتَنَا لِتَأْفِكَنَا عَنْ آلِهَتِنَا فَأْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ

Wakasema: Oh! Umetujia ili ututenge mbali na miungu yetu? Basi tuletee hayo unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

قَالَ إِنَّمَا الْعِلْمُ عِندَ اللَّهِ وَأُبَلِّغُكُم مَّا أُرْسِلْتُ بِهِ وَلَٰكِنِّي أَرَاكُمْ قَوْمًا تَجْهَلُونَ

Akasema: Hakika ujuzi uko kwa Mwenyezi Mungu tu. Mimi nakufikishieni niliyo tumwa. Lakini nakuoneni kuwa nyinyi ni watu mnaofanya ujinga.

Aya hizi zinazungumzia kisa cha Nabii Hud na kaumu yake ya Adi na kueleza kwamba Hud (AS), kama walivyokuwa Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu aliwaonya na kuwatahadharisha watu wake na shirki, kuabudu masanamu na kufanya mambo maovu na machafu. Lakini badala ya watu wake kutafakari na kuyatia akilini maneno yake kwa kuacha kuabudu miungu bandia na mienendo yao miovu, walimtaka Mtume wao huyo awateremshie papa hapa duniani adhabu anayowaahidi kuwa itawafika kwa kuikataa haki. Walitoa dai hilo kwa Nabii Hud, ilhali utoaji adhabu uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu; na Mitume hawana mamlaka wala nafasi yoyote katika uteremshaji na utoaji adhabu; iwe hapa duniani au huko akhera. Kwa sababu hiyo, Nabii Hud aliwajibu watu wake kwa kuwaambia: hilo mnalotaka nikufanyieni haliko kwenye mamlaka yangu. Allah SWT ndiye mwenye ujuzi wa hilo. Mimi nina jukumu la kufikisha wito wa maamrisho ya Mwenyezi Mungu tu na kukulinganieni tauhidi, yaani kumwabudu Yeye Mola pekee wa haki. Mimi siwezi kukulazimisheni muyakubali maneno yangu, wala sina uwezo wa kumpa adhabu mtu yeyote. Chanzo cha huu ukaidi wenu na kuikataa haki ni ujinga na ujahili, ambao ndio unaokufanyeni msiifahamu na kuiamini. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, jukumu la kwanza ambalo walikuwa nalo Mitume kwa kaumu zao za watu washirikina na waovu lilikuwa ni kuwapa maonyo ili wazinduke na kuelewa hatari ya wanayoyafanya. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, lengo na mwongozo mkuu wa Mitume wote katika kila zama za historia ulikuwa mmoja, nao ni Laa ilaaha illa Allah, yaani kumwabudu Mola pekee wa haki na kujiepusha na kila aina ya shirki na ukafiri. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, ikiwa mtu atakuwa na imani ya kujiri kwa Kiyama, atarekebisha mwenendo na matendo yake hapa duniani. Wa aidha aya hizi zinatubainishia kuwa, jukumu la Mitume lilikuwa ni kufikisha risala na ujumbe wa Mwenyezi Mungu si kuwalazimisha watu waabudu kwa nguvu. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, taasubu na ukereketwa usio na msingi juu ya mila, desturi na imani za kikaumu na kikabila ni ishara ya ujinga alionao mtu, ambao humfanya aselelee kwenye hali hiyo na kushindwa kuitambua haki na ukweli. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 925 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/