May 27, 2023 00:07 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 926 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 46 ya al Ah'qaaf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 24 na 25 za sura hiyo ambazo zinasema:

فَلَمَّا رَأَوْهُ عَارِضًا مُّسْتَقْبِلَ أَوْدِيَتِهِمْ قَالُوا هَٰذَا عَارِضٌ مُّمْطِرُنَا ۚ بَلْ هُوَ مَا اسْتَعْجَلْتُم بِهِ ۖ رِيحٌ فِيهَا عَذَابٌ أَلِيمٌ

Basi walipo liona wingu likielekea kwenye mabonde yao, walisema: Wingu hili la kutunyeshea mvua! (Hud akasema), haya ni hayo mliyo yahimiza; ni upepo ambao ndani yake imo adhabu iumizayo!

تُدَمِّرُ كُلَّ شَيْءٍ بِأَمْرِ رَبِّهَا فَأَصْبَحُوا لَا يُرَىٰ إِلَّا مَسَاكِنُهُمْ ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْقَوْمَ الْمُجْرِمِينَ

Unaangamiza kila kitu kwa amri ya Mola wake Mlezi. Basi Wakawa hawaonekani ila nyumba zao tu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo watu waovu!

Katika darsa iliyopita tulisema, kaumu ya Adi waliukataa wito wa tauhidi aliowapelekea Mtume wao Hud AS; na kwa ufidhuli, inadi na ukaidi wakamwambia: sisi hatuachi njia yetu tunayofuata. Kama wewe unasema kweli, iteremshe hiyo adhabu unayotuahidi. Baada ya kutimia dhima juu yao na kwa kuwa wao wenyewe walitaka wateremshiwe adhabu, Allah SWT aliwapelekea upepo mkali ulioambatana na wingu. Wakati watu wa kaumu hiyo walipoona wingu jeusi limetanda angani kote, walifurahi wakidhani kwamba muda si muda watanyeshewa na mvua yenye baraka nyingi. Lakini sio tu haikunyesha mvua, bali upepo mkali wa baridi yenye kuunguza na kuteketeza uliwafikia na kuiangamiza kaumu hiyo ya mafasiki na wafanya madhambi. Hakusalia yeyote kati ya waovu hao isipokuwa nyumba na maskani zao tu. Kwa mujibu wa aya ya saba ya Suratul-Haaqah, upepo huo uliokuwa mkali sana na uvumao kwa nguvu, uliendelea kutikisa mtawalia kwa muda wa mikesha saba na michana minane mpaka ukawaangamiza watu wote wa kaumu ya Adi pasi na kubakia hai hata mtu mmoja miongoni mwao. Hili kwa hakika ni onyo na indhari wanayopewa waovu, wafanya madhambi na makafiri wote walio jeuri na wakaidi ya kwamba, ikiwa na nyinyi pia mtakuwa na mwenendo huo, hamtakuwa na hatima nyingine isiyokuwa sawa na ya watu hao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, matokeo ya kuifanyia haki na ukweli inadi na ukaidi ni kufikwa na adhabu kali. Historia za kaumu zilizopita zimeacha ibra na somo hilo la kuzingatiwa na watakaokuja baada ya kaumu hizo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, vitu na matukio ya kimaumbile yako kwenye mamlaka ya Allah SWT. Mawingu, upepo na vitu vingine vya maumbile vinaweza vikawa alama ya rehma na ukarimu wa Allah SWT na vinaweza pia vikawa kielelezo cha ghadhabu na adhabu yake Mola. Kuna wakati Mwenyezi Mungu Mtukufu huufanya upepo uvume ili uyasukume mawingu kwa ajili ya kuteremka rehma ya mvua, na kuna wakati huufanya upepo uvume ili kuwa sababu ya kutokea hilaki na maangamizi. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, kuangamizwa waovu duniani ni utaratibu aliouweka Allah; na athari zilizoachwa na watawala na kaumu zilizopita ni maonyesho makubwa yenye ibra na mazingatio.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 26 ambayo inasema:

وَلَقَدْ مَكَّنَّاهُمْ فِيمَا إِن مَّكَّنَّاكُمْ فِيهِ وَجَعَلْنَا لَهُمْ سَمْعًا وَأَبْصَارًا وَأَفْئِدَةً فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُمْ سَمْعُهُمْ وَلَا أَبْصَارُهُمْ وَلَا أَفْئِدَتُهُم مِّن شَيْءٍ إِذْ كَانُوا يَجْحَدُونَ بِآيَاتِ اللَّهِ وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ

Na hakika tuliwamakinisha, sio kama tulivyokumakinisheni nyinyi; na tuliwapa masikio, na macho, na nyoyo; na hayakuwafaa kitu masikio yao, wala macho yao, wala nyoyo zao kwa lolote. Kwani hao walikuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na yakawazunguka yale waliyo kuwa wakiyafanyia stihzai.

Watu wa kaumu ya Adi walikuwa wakiishi karibu na Bara Arabu; na mabaki ya nyumba zao yalikuwa kwenye njia waliyokuwa wakipita watu wa eneo hilo katika safari zao. Na ndiyo maana Qur'ani inawahutubu washirikina wa Makka, waliokuwa wakionyesha inadi na ukaidi kwa wito wa Bwana Mtume SAW ya kwamba, watu wa kaumu ya Adi walikuwa na nguvu zaidi kimwili, na uwezo mkubwa zaidi wa mali na utajiri kuliko nyinyi; lakini ilipoteremshwa adhabu ya Mwenyezi Mungu, nguvu na utajiri wao huo havikuweza kuwasaidia wala kuwaokoa na adhabu hiyo. Kitu ambacho kingeweza kuwaokoa ni kuitambua na kuikubali haki. Wao, kama walivyo wanadamu wengine, walikuwa na macho, masikio na akili, lakini hawakuvitumia hivyo kwa ajili ya kuitambua haki na ukweli. Waliyafumba macho na masikio yao mbele ya haki na wakadhani kwamba nguvu na utajiri wao pamoja na nyenzo na suhula zao vitawawezesha kukabiliana na Allah SWT. Kwa hiyo wakawa wanayafanyia shere na stihzai na kutoyajali maonyo na indhari alizokuwa akiwapa Mtume wao Hud AS kuhusu hatari ya kushukiwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuwa na nguvu na madaraka pamoja na mali na utajiri hakumpi hakikisho mtu la kuokoka Siku ya Kiyama. Kutumia kwa njia sahihi neema za macho, masikio na akili kwa ajili ya kuufahamu ukweli na kuufuata ndiko kutakomuokoa mtu na kumpatia saada ya duniani na akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kukanusha haki na ukweli ni sababu ya kuangamizwa mtu; na utajiri na suhula zake za kimaada vitamsukumiza na kumfikisha kwenye hilaki. Vilevile aya hii inatutaka tuelewe kwamba, kuzifanyia shere na stihzai aya za Mwenyezi Mungu pamoja na maonyo ya Mitume ni miongoni mwa sababu za kufikwa na adhabu hata hapa duniani.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 27 na 28 za sura yetu ya Ah'qaaf ambazo zinasema:

‏ وَلَقَدْ أَهْلَكْنَا مَا حَوْلَكُم مِّنَ الْقُرَىٰ وَصَرَّفْنَا الْآيَاتِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ

Na hakika tuliiangamiza miji ilio jirani zenu, na tulizibainisha Ishara ili wapate kurejea.

فَلَوْلَا نَصَرَهُمُ الَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّهِ قُرْبَانًا آلِهَةً ۖ بَلْ ضَلُّوا عَنْهُمْ ۚ وَذَٰلِكَ إِفْكُهُمْ وَمَا كَانُوا يَفْتَرُونَ

Basi mbona wale walio washika badala ya Mwenyezi Mungu, kuwa ati hao ndio wawakurubishe, hawakuwanusuru? Bali waliwapotea! Na huo ndio (mwisho wa) uwongo wao na waliyo kuwa wakiyazua.

Baada ya aya iliyotangulia, ambayo ilizungumzia kuangamizwa kaumu ya Adi, aya hizi tulizosoma zinaeleza kwamba, si kaumu ya Adi peke yake, bali kuna kaumu zingine pia zilizokuwa zikiishi kandokando yenu nyinyi watu wa Makka, ambazo nazo pia tuliziangamiza ziliposimama kuipinga na kuikadhibisha haki. Miongoni mwao ni kaumu ya Thamudi ya kaskazini ya Bara Arabu na kaumu ya Saba'a iliyokuwepo kusini ya eneo hilo. Tuliwapelekea watu wa kaumu hizo aya na ishara zetu kulingana na uelewa na ufahamu wa kila moja kati ya kaumu hizo ili kutimiza dhima kwao na ili wasipate udhuru na kisingizio cha kuwafanya wafuate shirki na ukafiri. Lakini wao waliamua kuwaendea waabudiwa bandia na wa kujitengenezea, wakidhani wataweza kuwaokoa na kuwapatia saada. Hali ya kuwa, wakati adhabu ilipowashukia, si yeyote kati ya waabudiwa na miungu hao bandia aliyeweza kuwasaidia, au hata yenyewe kuweza kujinusuru na adhabu ya Mwenyezi Mungu; kwa hivyo ikatoweka bila kubaki athari yao yoyote. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, moja ya mbinu za uelimishaji za Qur'ani Tukufu ni kuwahimiza watu watalii na kusoma historia za watu waliopita na kupata ibra na somo kutokana na hatima za watu hao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Mwenyezi Mungu amemtayarishia mwanadamu njia na nyenzo za kuufikia uongofu na kurejea kwenye fitra na maumbile aliyomjaalia Yeye Mola. Muhimu ni yeye mwanadamu mwenyewe kutaka na kuwa tayari kurudi kwenye fitra yake na kuiacha njia ya upotofu. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, fikra za khurafa, uzushi na udhanifu hupelekea watu kuvipa hadhi ya kuwakurubisha wao na Mwenyezi Mungu, vitu ambavyo haviwapatii wao faida yoyote, wala haviwi na taathira yoyote kwao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 926 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azipe akili zetu ufahamu wa kuitambua haki, ayape masikio yetu usikivu wa kuipokea, azipe nyoyo zetu ulainifu wa kuikubali na atupe sisi wenyewe taufiki ya kuifuata. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/