Sura ya Muhammad, aya ya 15-17 (Darsa ya 930)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 930 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 47 ya Muhammad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 15 ya sura hiyo ambayo inasema:
مَّثَلُ الْجَنَّةِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ ۖ فِيهَا أَنْهَارٌ مِّن مَّاءٍ غَيْرِ آسِنٍ وَأَنْهَارٌ مِّن لَّبَنٍ لَّمْ يَتَغَيَّرْ طَعْمُهُ وَأَنْهَارٌ مِّنْ خَمْرٍ لَّذَّةٍ لِّلشَّارِبِينَ وَأَنْهَارٌ مِّنْ عَسَلٍ مُّصَفًّى ۖ وَلَهُمْ فِيهَا مِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ وَمَغْفِرَةٌ مِّن رَّبِّهِمْ ۖ كَمَنْ هُوَ خَالِدٌ فِي النَّارِ وَسُقُوا مَاءً حَمِيمًا فَقَطَّعَ أَمْعَاءَهُمْ
Mfano wa Pepo waliyo ahidiwa wachamngu ina mito ya maji yasiyo vunda, na mito ya maziwa isiyo haribika ladha yake, na mito ya mvinyo wenye ladha kwa wanywao, na mito ya asali iliyo safishwa. Na wao humo watakuwa na kila namna ya matunda, na maghfira kutoka kwa Mola wao Mlezi. Basi je, hao ni kama watakao dumu Motoni na wakinyweshwa maji yanayo chemka yatakayokata chango zao?
Katika aya tulizosoma katika darsa iliyopita ilielezwa ni vipi itakavyokuwa hatima ya waumini na makafiri. Aya hii tuliyosoma inaendeleza maudhui hiyo kwa kuashiria hali za makundi hayo mawili Peponi na Motoni na kutaja baadhi ya sifa maalumu za sehemu hizo mbili. Katika hali maalumu za kimwili alizonazo mwanadamu hapa duniani, na ambayo itakuwepo pia huko akhera ni kuona kiu, ambayo kuiondoa kwake kunahitaji maji salama ya kunywa. Aya hii inasema: kwa ajili ya kukidhi haja hiyo, Mwenyezi Mungu SWT amewaandalia aina mbalimbali za vinywaji vitamu na vya kuburudisha watu wa peponi, kuanzia maji na maziwa mpaka mvinyo na asali. Lakini kwa upande wa watu wa motoni hawatopewa kinywaji chochote isipokuwa maji moto yenye kuunguza, licha ya kwamba kwa kuweko kwao motoni uhitaji wao wa maji baridi utakuwa mkubwa zaidi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, mapambo na raha za kidunia zisituteke na kutuelekeza kwenye madhambi, kwani Yeye Allah SWT amewaandalia watu wa peponi huko akhera raha na starehe za kiwango cha juu kabisa na zisizo na mfano. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, watu wanaomcha Mwenyezi Mungu na wakaamua kujiepusha na raha, starehe na burudani zilizo haramu na za kupita, watakwenda kupata raha na starehe za milele huko akhera. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, rehema na maghufira makhsusi ya Mola, mbali na neema za kimaada na kimwili zitawapa watu wa peponi utulivu wa kipekee wa kiroho na kiakili. Wa aidha tunajifunza kutokana na aya hii kuwa, mbali na anuai za vinywaji, watu wa peponi watakirimiwa pia kwa namna mbalimbali za vilaji na matunda. Na pia aya hii inatuelimisha kwamba, neema za peponi haziharibiki, haziwi na kasoro wala nuksani na wala hazimaliziki.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 16 ambayo inasema:
وَمِنْهُم مَّن يَسْتَمِعُ إِلَيْكَ حَتَّىٰ إِذَا خَرَجُوا مِنْ عِندِكَ قَالُوا لِلَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ مَاذَا قَالَ آنِفًا ۚ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ طَبَعَ اللَّهُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ وَاتَّبَعُوا أَهْوَاءَهُمْ
Na wapo miongoni mwao wanao kusikiliza, mpaka wakiondoka kwako huwauliza walio pewa ilimu: Amesema nini sasa hivi? Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao, na wakafuata matamanio ya nafsi zao.
Aya hii inazungumzia kundi moja la watu wenye imani dhaifu na nyoyo zenye maradhi ya nafsi, ambao walikuwa wakiishi katika jamii ya Kiislamu lakini hawakuwa wakiyaamini maneno ya Bwana Mtume SAW na Wahyi aliokuwa akiteremshiwa na Allah SWT. Walikuwa wakiyasikia maneno ya Mwenyezi Mungu kutoka kwenye kinywa cha Mtume, lakini wakawa wanasema: hatuelewi wala hatufahamu chochote; na wakati walipokuwa wakikutana na waumini wajuzi na waelewa, wakawa wanawauliza kwa kejeli na stihzai: Hivi nyinyi mmeyafahamu maneno ya Mtume? Sisi wenzenu hatujafahamu chochote! Aya hii inatoa jibu kwa mwenendo huo usio sahihi wa watu hao na kusema: maneno ya Mtume yako wazi na wadhiha kabisa. Lakini kwa vile mnachotaka nyinyi ni kukidhi hawaa na matamanio ya nafsi zenu na si kufuata haki, ndio maana mmeshindwa kuelewa na kufahamu haki na ukweli. Kwa maneno mengine ni kuwa, tatizo haliko kwa Bwana Mtume; tatizo ni nyinyi wenyewe ambao hamuikubali haki. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hii ni kwamba, kutii hawaa na kufuata matamanio haramu ya nafsi husababisha mtu kupoteza uwezo wa kupambanua haki na batili na kumfanya ashindwe kufahamu ukweli. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, tujihadhari na watu wenye maradhi ya nyoyo, ambao dhamira yao ni kutia shaka juu ya ukweli wa wahyi na maneno ya Mtume na kudhoofisha imani za watu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa, kusoma na kusikiliza tu maneno ya Mwenyezi Mungu hakutoshi; ni muhimu pia kuyafahmu na kuyaelewa mafunzo, mafundisho, maamrisho na makatazo yake na kuyafanyia kazi. Watu wangapi na wangapi walikuwa wakiyasikia maneno fasaha na wadhiha ya Bwana Mtume SAW, lakini kwa vile walijali kwanza hawaa na matamanio ya nafsi zao, hawakuwa tayari kuikubali haki.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 17 ya sura yetu ya Muhammad ambayo inasema:
وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ
Na wale wanaokubali kuongoka anawazidishia uongofu na anawapa (jaza ya) uchamngu wao.
Mkabala wa watu wenye maradhi ya nyoyo, ambao hawaukubali na wanautilia shaka wito wa uongofu wa Mtume, katika aya hii, Qur'ani tukufu inaahidi kwamba kila atakayeukubali wito wa awali wa uongofu wa Mitume, Mwenyezi Mungu atamtunuku neema mbili zenye thamani aali: ya kwanza ni kupata na kubainikiwa na uongofu katika njia ya maisha iliyojaa kila aina ya misukosuko. Na ya pili, ni kuwa na uzima, usafi na utoharifu wa roho. Hapana shaka mwanadamu kila mara huwa hatarini kuteleza na kukosea. Na si jambo rahisi kwake kutambua njia sahihi ya kufuata katika masuala mbalimbali kama ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kifamilia n.k. Mwanadamu anahitaji mwongozo wa dini katika vipindi vyote vya maisha yake. Na ndio maana Allah SWT ameahidi kwamba, kama mtu ataukubali uongofu wa awali wa dini, Yeye Mola atamsaidia kutambua njia sahihi ya kufuata ya maisha. Na bila shaka mbali na mwongozo huo, unahitajika pia usafi na utoharifu wa nafsi na wa batini ili mtu asiathirike na hisia potofu kutokana chuki, husda, ubakhili au sifa nyingine chafu za kiakhlaqi na kuikengeuka njia ya haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuukubali mwongozo na uongofu wa awali wa Allah, humwandalia mtu mazingira ya kuongezewa uongofu na Allah SWT. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuwa na utayarifu wa kufuata uongofu huijenga na kuiimarisha nafsi ya mtu kimaanawi. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa, kuufikia utoharifu wa moyo na irfani halisi ya kumtambua vilivyo Allah kinafsi kunapatikana kwa kufuata mwongozo na uongofu wa Mwenyezi Mungu tu; na si kwa kufuata njia na fikra zilizobuniwa na wanadamu kama Ubudha, Uhindu na mfano wa hizo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 930 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/