Jun 12, 2023 06:29 UTC
  • Jumatatu, tarehe 12 Juni, 2023

Leo ni tarehe 23 Dhilqaada 1444 Hijria sawa na Juni 12 mwaka 2023.

Tarehe 12 Juni miaka 483 iliyopita nchi ya Chile iliyoko magharibi mwa Amerika ya Kusini ilitekwa na wakoloni wa Hispania. Kabla ya hapo Wahindi Wekundu wa Chile walikuwa wamevunja hujuma na mashambulio kadhaa ya Wahispania waliokusudia kuteka na kukalia kwa mabavu ardhi yao. Hata hivyo, hata baada ya kutekwa nchi yao, Wahindi Wekundu hao waliendeleza mapambano dhidi ya wakoloni hadi pale José Francisco de San Martín jenerali wa Argentina alipowasili mwaka 1817 na kuanzisha mashambulio ya kuzikomboa nchi zote zilizokuwa chini ya ukoloni wa Hispania Kusini mwa Amerika, ikiwemo Chile. Kwa msingi huo, Chile akakombolewa na kutangaza uhuru wake mwaka 1818.

Bendera ya Chile

Tarehe 12 Juni 1914, kwa mara ya kwanza kabisa yalifanyika majaribio ya kutumia nishati ya joto la jua pambizoni mwa Cairo mji mkuu wa Misri.

Mbunifu na mtekelezaji wa mpango huo alikuwa mwanafizikia wa Kijerumani, ambaye aliweza kukusanya miale ya jua na kufanikiwa kuwasha mashine ya mvuke yenye kutumia 'horse power' 50.

Siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 12 Juni 1964, Nelson Mandela kiongozi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa tuhuma za kufanya uhaini dhidi ya mfumo na utawala wa ubaguzi wa rangi, Apartheid. Mandela alihukumiwa adhabu hiyo pamoja na wenzake saba akiwemo Walter Sisulu aliyekuwa Katibu Mkuu wa zamani wa chama cha African National Congress kilichokuwa kimepigwa marufuku nchini Afrika Kusini. 

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Juni 1975, Indira Gandhi Waziri Mkuu wa wakati huo wa India alizuiwa kuendelea na wadhifa huo kwa miaka sita, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya udanganyifu katika uchaguzi. Hata hivyo Indira Gandhi alipinga miito iliyomtaka ajiuzulu na akatangaza shjeria za kijeshi kote nchini India baad aya maandamano makubwa ya wananchi yaliyotishia kuiondoa madarakani serikali yake.   *****

Na katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita inayosadifiana na 12 Juni 1991, ulifanyika uchaguzi wa kwanza wa Rais wa Shirikisho la Russia.

Baada ya kusambaratika Urusi ya zamani, Russia kama zilivyokuwa nchi nyingine zilizokuwa zikiunda Umoja wa Kisovieti zilijipatia uhuru wake. Boris Yeltsin aliiongoza nchi hiyo kwa vipindi viwili, hadi mwezi Disemba 1999, alipoamua kung'atuka madarakani.

 

Tags