Jumamosi, 17 Juni, 2023
Leo ni Jumamosi tarehe 28 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1444 Hijria sawa na tarehe 17 Juni 2023 Milaadia.
Tarehe 28 Dhilqaada miaka 1084 iliyopita mwanazuoni wa Kiislamu, Abul Qasim Tabarani, alifariki dunia katika mji wa kihistoria wa Isfahan nchini Iran. Tabarani alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Hadithi wa karne ya nne Hijria na alifanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kukusanya Hadithi za Mtume Muuhammad (saw). Alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi baada ya utafiti na uchunguzi wa miaka 33. Tabarani ameandika vitabu vikubwa vitatu vya Hadithi kwa majina ya Al Muujamul Kabiir", al Muujamul Wasiit na al Muujamus Swaghir. ***

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita sawa na tarehe 17 Juni 1925, ulitiwa saini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za vijidudu na kemikali mjini Geneva Uswisi. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utumiaji vitani wa aina yoyote ya silaha za vijidudu, gesi zinazoua, sumu za kemikali na nyinginezo kama hizo ulipigwa marufuku. Licha ya kufikiwa makubaliano hayo, lakini baadhi ya nchi bado ziliendelea kutumia silaha hizo zilizopigwa marufuku duniani. Ujerumani ilitumia silaha za kemikali katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Marekani katika vita vya Vietnam na utawala wa zamani wa Iraq kutumia silaha hizo wakati wa vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran. ***

Katika siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, wakazi wa kisiwa cha Iceland walifanikiwa kupata uhuru wao kutoka mikononi mwa Denmark. Kisiwa cha Iceland kiligunduliwa tarehe 10 Julai 874 Miladia na kuanzia wakati huo, ndipo wahajiri wa Norway, Scotland na Ireland wakaanza kuishi katika kisiwa hicho. Hadi kufikia karne ya 13 Miladia ilikuwa ni nchi huru hata hivyo muda baadaye iliunganishwa na Norway na kisha Denmark. Mwaka 1874 Denmark iliruhusu kuundwa baraza la watunga sheria (yaani bunge) katika kisiwa hicho cha Iceland. Aidha serikali ya ndani ya kisiwa hicho iliendelea kufuatilia haki zake zaidi ingawa bado kiliendelea kutambuliwa kuwa sehemu ya Denmark, hadi tarehe 17 Juni 1944 ambapo kulitangazwa kuvunjwa muungano huo baada ya kurejelewa maoni ya wakazi wa Iceland. Kuanzia wakati huo, wakakazi wa Iceland wanaitambua siku kama ya leo kuwa siku ya kitaifa. ***
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, yaani tarehe 27 Khordad kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia, Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuasisiwa taasisi ya Jihadi ya Ujenzi kwa ajili ya kulinda uhuru wa Iran, kujitegemea na kumaliza umaskini hususan katika maeneo ya vijijini. Kufuatia kutolewa amri hiyo, wananchi wa matabaka mbalimbali hasa wanafunzi na wanachuo, vijana wenye ghera na imani na wasomi walijitolea kwenda kufanya kazi za ujenzi za kuwasaidia watu maskini katika pembe mbalimbali za Iran. Taasisi ya Jihadi ya Ujenzi imezaliwa kutoka ndani ya Mapinduzi ya Kiislamu na hadi sasa inafanya kazi kubwa za ujenzi na kusaidia watu maskini na wenye haja. Taasisi hiyo inajihusisha na mambo mengi yakiwemo masuala ya viwanda, kazi za vijijini, kilimo, ufugaji, ujenzi wa mabwawa, kulinda mazingira na makumi ya kazi nyingine za kujenga taifa. Mwaka 1362 Hijria Shamsia Taasisi ya Jihadi ya Ujenzi ya Iran ilibadilishwa na kuwa Wizara, na mwaka 1379 Hijria Shamsia iliingizwa kwenye Wizara ya Kilimo ya Iran. ***