Jun 18, 2023 04:24 UTC
  • Jumapili, tarehe 18 Juni, 2023

Leo ni Jumapili tarehe 29 Dhulqaada 1444 Hijria sawa na tarehe 18 Juni 2023.

Siku kama ya leo miaka 208 iliyopita, vilianza vita vya kihistoria vya Waterloo, vita vya mwisho vya Napoleon Banaparte na madola ya Ulaya. Katika vita hivyo majeshi ya serikali za Prussia na Uingereza yalikutana uso kwa uso na majeshi ya Napoleon Banaparte katika eneo lililokuwa likiitwa kwa jina la Waterloo. Katika vita hivyo na kutokana na kunyesha mvua kali na kuharibika njia zilizokuwa zikitumiwa kwa usafirishaji, hivyo zana za kijeshi  zilichelewa kufika uwanja wa vita sambamba na kuchelewa kufika kikosi cha mstari wa mbele cha Wafaransa. Kufuatia hali hiyo, Napoleon Banaparte akawa ameshindwa vibaya katika vita hiyo na hivyo kumfanya akimbie kwa kutumia meli kuelekea kisiwa cha Saint Helena na kufariki dunia miaka kadhaa baadaye kwenye kisiwa hicho. 

Vita vya kihistoria vya Waterloo

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 68, Maxim Gorky, mwanafasihi na mwandishi mashuhuri wa nchini Russia. Alexei Maximovich Peshkov maarufu kwa jina la Gorky, alikuwa mandishi mkubwa aliyezaliwa tarehe 28 Machi 1868 katika mji wa Gorky nchini Russia. Alianza kusoma kwa bidii elimu ya fasihi hapo mwaka 1895 na kupewa lakabu ya Maxim Gorky ambayo ilikuja kutumika kama jina lake na baadaye kufikia kupata umashuhuri mkubwa katika fani hiyo. Kwa kuzingatia kuwa alitokana na familia masikini, hivyo uandishi wa Maxim Gorky ulijikita sana katika kupiga vita umasikini na ujinga. Ameacha athari mbalimbali kikiwemo kitabu cha Mijeledi Mitatu kinachozungumzia maisha yake.   

Maxim Gorky

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita inayosadifiana na tarehe 18 Juni 1953 utawala wa kifalme ulisambaratika nchini Misri na kukaasisiwa mfumo wa Jamhuri baada ya Mfalme Farouq wa nchi hiyo kupelekwa uhamishoni. Kufuatia kushindwa Misri katika vita na Israel mwaka 1948 wananchi wa Misri walipoteza imani yao kwa Mfalme Farouq na hivyo hali ya ndani ya Misri kuanza kuharibika. Mwishowe liliundwa shirika la siri ndani ya jeshi lililopinga utawala wa mfalme huyo. Mwaka 1952 shirika hilo lilimlazimisha Mfalme Farouq kujiuzulu kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Muhammad Najib na Jamal. Mwaka mmoja baada ya kutangazwa Jamhuri ya Misri, Jenerali Muhammad Najib aliapishwa kuwa rais wa kwanza wa Misri. Mwaka mmoja baadaye Jamal Abdul Nassir alimuuzulu Muhammad Najib. Abdul Nassir alipata umaarufu mkubwa nchini Misri na duniani kote kwa sababu ya kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.  

Mfalme Farouq

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, yalitiwa saini makubaliano ya pili ya kupunguza silaha yaliyojulikana kwa jina la Salt 2 kati ya Marais Leonid Brezhnev wa Urusi ya zamani na Jimmy Carter wa Marekani. Makubaliano hayo yalikuwa na lengo la kupunguza silaha za nyuklia duniani. 

Salt 2

Miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo, Necmettin Erbakan Waziri Mkuu aliyekuwa na misimamo ya Kiislamu wa Uturuki alilazimika kujiuzulu kutokana na mashinikizo ya wanajeshi wa nchi hiyo. Chama cha Erbakan kilipata kura nyingi katika uchaguzi wa Disemba mwaka 1994 na kuunda Baraza la Mawaziri. Lakini wasekulari na makamanda wa jeshi walizuia kutekelezwa malengo ya serikali ya Erbakan. Waziri Mkuu huyo alikuwa akiamini kwamba kuwakandamiza wanaharaki wa Kiislamu nchini Uturuki ni kinyume na demokrasia na alipinga kuimarishwa uhusiano wa nchi hiyo na utawala ghasibu wa Israel. Lakini Baraza la Usalama wa Taifa la Uturuki ambalo lilikuwa na ushawishi mkubwa wa wanajeshi Februari 1997 lilitoa amri ya kumlazimisha Erbakan akabiliane na wanaharakati wa Kiislamu. Miezi minne baadaye waziri mkuu huyo alishtakiwa mahakamani kutokana na misimamo yake ya Kiislamu na kuzuiwa kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa muda wa miaka mitano.

Necmettin Erbakan