Jun 19, 2023 23:38 UTC
  • Jumanne tarehe 20 Juni 2023

Leo ni Jumanne tarehe Mosi Dhulhija 1444 Hijria sawa na tarehe 20 Juni 2023.

Siku kama ya leo miaka 1442 iliyopita Binti wa Mtume Muhammad (saw) Fatima al Zahraa (as) alifunga ndoa na Imam Ali bin Abi Twalib (as)

Bibi Fatima alikuwa mwanamke mwema aliyejipamba kwa sifa zote nzuri ambaye alichumbiwa na shakhsia wakubwa na watu mashuhuri wa zama hizo. Hata hivyo Mtume (saw) alikuwa akiwaambia wachumbiaji hao kwamba suala la kuolewa Fatima liko mikononi mwa Mwenyezi Mungu.

Hatimaye Imam Ali bin Abi Twalib alikwenda kwa Mtume na kumchumbia Bibi Fatima na baada ya kushauriana na bintiye, Mtume alikubaliana na ombi la Ali na kuwafungisha ndoa. Baada ya kufunga ndoa, watukufu hao wawili waliishi maisha ya watu wa kawaida lakini yaliyojaa upendo, masuala ya kiroho na maadili ya Kiislamu. Watukufu hao wawili waliipa jamii ya mwanaadamu watu adhimu na kamili kama Imam Hassan, Imam Hussein na Bibi Zainab (as). Ali na Fatima (as) walikuwa kigezo bora cha mwanaadamu kamili.

Siku kama ya leo miaka 148 iliyopita inayosadifiana na hii ya leo yaani tarehe 20 mwezi Juni mwaka 1875, kisiwa cha Okinawa kinachopatikana katika Bahari ya Pacific huko Japan kilidhibitiwa na jeshi la nchi hiyo.

Hata hivyo mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia kisiwa hicho cha kistratijia chenye ukubwa wa kilomita mraba 1250 kilikaliwa kwa mabavu na majeshi ya Marekani licha ya mapambano makali ya jeshi la Japan.

Jeshi la Marekani liliondoka Japan mwaka 1958 lakini kisiwa cha Okinawa kiliendelea kudhibitiwa na Wamarekani. Mwaka 1972 vikosi vya Marekani vilisitisha ukaliaji wa mabavu wa kisiwa hicho kufuatia mazungumzo marefu kati ya Washington na Tokyo. 

Okinawa, Japan

Miaka 111 iliyopita katika siku kama ya leo msomi wa Poland kwa jina la Casimir Funk kwa mara ya kwanza kabisa alifanikiwa kugundua vitamin au virutubisho.

Baada ya uhakiki mwingi Dakta Casimir Funk aligundua kwamba vyakula vinavyotumiwa na mwanadamu vina baadhi ya virutubisho (vitamins) ambavyo japokuwa ni vichache sana lakini vina udharura mkubwa katika ukuaji na usalama wa mwili na akaamua kuvipa jina la Vitamini.

Kuna aina mbalimbali za vitamin kama A, B, C, D na E, na kila moja ina sifa za kipekee na matumizi ya aina yake katika mwili. 

Casimir Funk

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita magaidi wa kundi la MKO walitenda jinai kubwa ya kutisha katika haram tukufu ya Imam Ridha (a.s) mjukuu wa Mtume Mtukufu (s.a.w) katika mji mtakatifu wa Mash'had.

Bomu liliripuka ndani ya haram tukufu ya Imam Ridha (a.s) alasiri ya siku ya Ashura mwaka huo wakati watu walipokuwa wakifanya ziara na marasimu ya kukumbuka mapambano ya kihistoria ya kuuawa shahidi Imam Hussein(a.s). Makumi ya waumini na wapenzi wa Ahlul Bait (a.s) waliuliwa shahidi au kujeruhiwa katika haram hiyo. Mlipuko huo ulisababisha hasara na maafa mengi katika haram hiyo tukufu. 

Haram tukufu ya Imam Ridha (a.s)

Na katika siku kama ya leo miaka 21 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia alifariki dunia Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, mlinganiaji mkubwa wa Uislamu katika kanda ya mashariki mwa Afrika.

Hujjatul Islam Walmuslimin Rizvi alizaliwa huko mashariki mwa India na baada ya kupata masomo ya awali kwa baba yake alijifunza masomo ya juu na lugha za Kingereza, Kifarsi na Urdu na kupata daraja ya Fakhrur Afadhil. Baada ya kulingania dini kwa miaka mingi nchini India, Sayyid Akhtar Rizvi alihisi wajibu wa kuelekea Tanzania, barani Afrika na kuanza kueneza maarifa ya dini na mafundisho ya Ahlubaiti wa Mtume (saw).

Allamah Rizvi ameandika na kufasiri vitabu vingi kwa lugha mbalimbali ikiwa ni pamoja na tafsiri ya Qur'ani ya al Miizan na kitabu cha Al Ghadir na kujenga makumi ya misikiti, madrasa, maktaba na zahanati. Alifariki dunia jijini Dar es Salaam katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 76.

Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi