Jumamosi, 24 Juni, 2023
Leo ni Jumamosi tarehe 5 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1444 Hijria mwafaka na tarehe 24 Juni 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 211 iliyopita, Napoleone Bonaparte mtawala wa Ufaransa akiwa na kikosi cha askari 350,000 alianza kufanya mashambulio dhidi ya utawala wa Russia wa Tsar. Miaka mitano kabla ya tukio hilo, nchi mbili hizo zilikuwa zimetiliana saini mkataba wa kutoshambuliana kijeshi. Hata hivyo taratibu uhusiano baina ya tawala mbili hizo ulianza kuharibika, na hivyo kumfanya Bonaparte afikie hatua ya kuandaa jeshi kubwa na kuishambulia Russia na kisha kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Moscow. Hata hivyo hali mbaya ya hewa yaani baridi kali na kutowafikia wanajeshi wa Kifaransa vifaa muhimu na suhula za kivita, kuliwafanya askari hao wakabaliwe na hali ngumu katika medani ya vita. Hali hiyo ilimlazimisha Bonaparte atoe amri ya kurejea nyuma vikosi vyake. Wakati wa kujiri zoezi hilo, askari jeshi wapatao 30,000 wa Kirusi waliwashambulia askari wa Bonaparte na kuwaua wengi miongoni mwao. Akiwa amebakiwa na askari 30,000 tu, Bonaparte aliikimbia Russia na kufanikiwa kuwasili Paris Ufaransa Desemba mwaka 1812. ***
Katika siku kama ya leo miaka 180 iliyopita, tanuu za feleji maarufu kwa jina la tanuu za Bessemer zilivumbuliwa. Mvumbuzi wa tanuu hizo alikuwa Mwingereza Henry Bessemer. Tanuu hizo zilitumika huko Uingereza kwa mara ya kwanza na leo hii zinatumika katika masuala mbalimbali viwandani. ***
Miaka 109 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Sheikh Muhammad al-Ghazali, msomi, mwandishin na alimu mkubwa wa Kimisri. Muhammad al-Ghazali alizaliwa na kukulia katika familia iliyokuwa imeshikmana na dini. Kutokana na hima na idili kuubwa aliyokuwa katika masomo, Muhammad al-Ghazali alifanikiwa kuhitimuu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar akiwa na umri wa miaka 26 sambamba na kupata idhini ya kufundisha chuo hapo. Muhammad al-Ghazali ameandika vitabu visivyopungua 94. Msomii huyu alifanya hima na juhudi kubwa pia za kupigania umoja katika jami ya Kiislamu. Muhammad al-Ghazali aliaga dunia 20 Mfunguo Mosi Shawwal 1416 Hijria. ***

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, alifariki dunia huko Najaf, Iraq Allamah Muhammad Hussein Kampani, mwanafalsafa, faqihi na mwanairfani mkubwa. Alizaliwa mwaka 1296 Hijria mjini Kadhimain nchini Iraq. Msomi huyo mkubwa alitabahari katika elimu za falsafa, tiba, irfan, historia, jiografia, mashairi na fasihi. Mbali na hayo Allamah Hussein Kampani alikuwa na fikra pevu na uwezo mkubwa wa kubainisha mambo. Msomi huyo ameandika vitabu kadhaa katika nyanja mbalimbali ikiwemo diwani ya mashairi akisifu viongozi wa Uislamu. ***