Jun 25, 2023 02:38 UTC
  • Jumapili, 25 Juni, 2023

Leo ni Jumapili tarehe 6 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 144 Hijria sawa na tarehe 25 Juni 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1186 iliyopita, yaani tarehe 6 Dhul-Hijja mwaka 258 Hijria, alizaliwa Abu Ali Muhammad ibn Hammam, mmoja wa Maulamaa mashuhuri wa Iran. Ibn Hammam alikuwa akiishi mjini Baghdad, Iraq ambapo alifanikiwa kusoma elimu ya hadithi kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake. Aidha msomi huyo alikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao walijifunza toka kwake elimu ya hadithi na elimu nyingine za Kiislamu. Msomi huyo ameacha vitabu kadhaa katika uga wa hadithi. ***

Abu Ali Muhammad ibn Hammam

 

Miaka 201 iliyopita katika siku kama ya leo, kundi la watumwa wa Marekani wenye asili ya Afrika ambao waliachiwa huru na wamiliki wao wazungu wa nchi hiyo, walirejea Afrika na kuanzisha makazi katika ardhi ambayo leo hii inajulikana kama Liberia. Raia hao weusi wa Marekani walianzisha harakati ya ukombozi mwanzoni mwa karne ya 19 kwa lengo la kujiondoa utumwani na kuunda nchi yao. Kwa sababu hiyo kundi la Wamarekani weusi wenye asili ya Afrika lilihamia Magharibi mwa Afrika na kuasisi nchi ya Liberia kwa kusaidiwa na taasisi ya wahamiaji, baada ya kuwa utumwani kwa miaka mingi huko Marekani. Awali Liberia ilikuwa ikiendeshwa kama moja ya majimbo ya Marekani, lakini mwaka 1847 nchi hiyo iliasisi mfumo wa jamhuri na rais wake wa kwanza akawa Joseph Roberts, mtumwa kutoka jimbo la Virginia. ***

Bendera ya Liberiia

 

Tarehe 4 Tir miaka 60 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini alihamishiwa katika kambi ya kijeshi ya Eshtar-Abad baada ya kukamatwa na Shirika la Usalama Wa Taifa la Shah maarufu kwa jina la Savak. Siku 40 baada ya kushikiliwa katika kambi hiyo, Imam Khomeini kwanza alipelekwa uhamishoni nchini Uturuki na mwaka mmoja baadaye akapelekwa Iraq. Katika kipindi chote cha miaka 13 ya kubaidishiwa nje ya nchi, Imam aliongoza harakati zake za mapinduzi kupitia wanafunzi wake waliokuwa wakiwasilisha ujumbe zake kwa wananchi ndani ya Iran. Februari mwaka 1979 Imam Ruhullah Khomeini alirejea nchini na kupokewa na watu milioni tano. Siku 10 baadaye Imam alifanikiwa kuuangusha utawala wa kifalme ulioiongoza Iran kwa kipindi cha miaka 2500. ***

Imam Ruhullah Khomeini (ra)

 

Katika siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, yaani tarehe 25 Juni mwaka 1975, Msumbiji ilipata uhuru. Mwishoni mwa karne ya 15 kundi moja la mabaharia wa Kireno likiongozwa na mvumbuzi mashuhuri Vasco da Gama lilifika Msumbiji na kuanzia hapo mabaharia hao wakaanza kuikoloni nchi hiyo, ukoloni ambao uliendelea kwa karne tano. Wareno walianza kupora maliasili na utajiri wa Msumbiji na makumi ya maelfu ya wananchi wapigania ukombozi wa Msumbiji waliuawa wakitetea nchi yao. ***

 

Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, mamia ya mahujaji wa Iran na wengine kutoka nchi tofauti waliokuwa wameenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu mjini Makka na wakiwa katika hali ya kutekeleza ibada ya faradhi ya kujitenga na washirikina, waliuawa shahidi na askari wa utawala wa Saudi Arabia. Ni vyema kukumbusha kuwa, mahujaji wa Iran kwa miaka yote huwa wanatekeleza ibada hiyo kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo mbali na kuwasisitizia Waislamu kuungana, hutangaza kujitenga na maadui wa Uislamu hususan Marekani na utawala haramu wa Israel. Ibada hiyo ambayo hufanyika kwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, huwa na taathira kubwa katika msimu wa Hija. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akasisitiza sana umuhimu wa ibada ya kujitenga na mushrikina na maadui wa dini ya Kiislamu.  ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 35 iliyopita yaani tarehe 4 Tir 1367 Hijria Shamsia, ndege za utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq, kwa mara nyingine tena ziliwashambulia kwa mabomu ya kemikali wapiganaji wa Kiirani waliokuwa katika visiwa vya Majnun. Mamia ya wanajeshi wa Iran waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Saddam. Utawala wa zamani wa Iraq ulitumia silaha za maangamizi ya umati za kemikali tangu mwanzoni mwa vita vyake dhidi ya Iran mwaka 1359 Hijria Shamsiya, na kuzidisha matumizi ya silaha hizo sambamba na ushindi wa wapiganaji wa Iran. ***

Silaha za kemikali

 

Tags