Jumanne, 27 Juni, mwaka 2023
Leo ni Jumanne tarehe 8 Dhulhija 1444 Hijria sawa na tarehe 27 Juni mwaka 2023.
Leo tarehe 8 Dhulhija ni siku ya Tarwiya. Siku hii imepewa jina la siku ya Tarwiya kwa maana ya kijitosheleza kwa maji kwa sababu katika zama za Nabii Ibrahim (as) maji hayakuwa yakipatikana katika jangwa na Arafa na kwa msingi huo watu walikuwa wakipeleka maji eneo la Arafa kutoka Makka tarehe 8 Dhulhija wakijitayarisha kwa ajili ya mahitaji ya maji ya kesho yake yaani tarehe tisa Dhulhija.

Katika siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Imam Hussein bin Ali (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad SAW aliondoka Makka na kuelekea Kufa nchini Iraq baada ya kukataa kumbai na kutoa kiapo cha utiifu kwa Yazid bin Muawiya. Miezi minne kabla ya hapo, Imam Hussein alikuwa amewasili mjini Makka akiwa pamoja na familia yake na alikitumia kipindi cha kuweko waumini waliotoka pembe mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufanya ziara katika Nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu, kuwaamsha na kuwabainishia dhulma na ufisadi mkubwa uliokuwa ukifanywa wa utawala wa Yazid mwana wa Muawiya. Wakati huo huo kutokana na wito wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na njama za utawala wa Yazidi za kutaka kumuuwa, Imam Hussein aliondoka Makka na kueleka Kufa.

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita inayosadifiana na 27 Juni 1977, nchi ya Djibouti iliyoko karibu na eneo la Pembe ya Afrika ilipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa baada ya kupita miaka kadhaa ya harakati ya kupigania uhuru. Tokea mwaka 1896 nchi hiyo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Somalia Ufaransa na kuwa chini ya himaya ya Ufaransa, lakini baada ya kupita miongo minane, hatimaye nchi hiyo ilipata uhuru. Djibouti ilikuwa nchi ya mwisho kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na inahesabiwa kuwa nchi muhimu iliyoko katika eneo la kiistratijia kwa kuwa inapakana na Bahari Nyekundu na Bahari ya Hindi, kwenye eneo la lango bahari la 'Bab Mandab'.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, sawa na tarehe 6 Tir 1360 Hijria Shamsia, Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiwa mjumbe wa Imam Khomeini katika Baraza Kuu la Ulinzi na Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, alinusurika kifo baada ya kundi la kigaidi la MKO Munafikiin kumtegea bomu wakati alipokuwa akitoa hotuba katika mojawapo ya misikiti ya Tehran. Kwenye tukio hilo la kigaidi, Ayatullah Khamenei alijeruhiwa vibaya mkono wake wa kulia.
Tarehe 27 Juni 1993, Marekani ilirusha makombora 23 huko Baghdad mji mkuu wa Iraq na pambizoni mwa mji huo. Shambulio hilo lilifanyika kwa kisingizo kwamba viongozi wa utawala wa zamani wa Iraq walitaka kumuuwa George Bush 'baba', Rais wa zamani wa Marekani wakati alipokuwa safarini nchini Kuwait mwezi April mwaka huo huo. Shambulio hilo lilipelekea watu sita kuuawa na jengo la makao makuu ya Taasisi ya Usalama ya Iraq liliharibiwa kabisa. ***
Na siku kama ya leo miaka 28 iliyopita Sheikh Hamad bin Khalifa Aal Thani aliyekuwa mrithi wa Amir wa Qatar alifanya mapinduzi dhidi ya baba yake. Sheikh Hamad alimuondoa madarakani baba yake, Sheikh Khalifa bin Hamad Aal Thani wakati Amiri huyo wa zamani wa Qatar alipokuwa safarini nchini Uswisi. Sheikh Khalifa ambaye alikuwa kiongozi wa Qatar tangu mwaka 1972 alifanya jitihada kubwa za kurejea madarakani lakini hakufanikiwa. Nchi ndogo ya Qatar iko kusini mwa Ghuba ya Uajemi na inapakana na Saudi Arabia. Nchi hiyo ina utajiri mkubwa wa mafuta na gesi.