Alkhamisi, tarehe 6 Julai, 2022
Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Dhulhija 1444 Hijria sawa na Julai 6 mwaka 2023.
Katika siku kama ya leo miaka 169 iliyopita, alifariki dunia George Simon Ohm mwanahisabati na mwanafizikia wa Ujerumani akiwa na umri wa miaka 67. Simon Ohm alizaliwa mwaka 1789 na kuanza kupenda sana somo la fizikia na kufanikiwa kuvumbua kanuni katika uwanja wa umeme kutokana na utafiti mkubwa aliokuwa akiufanya katika uwanja huo. Alizipa kanuni hizo jina lake yaani "Ohm Laws". Kanuni ambazo zinatumiwa hadi leo hii.

Miaka 61 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia mwandishi wa Kimarekani, William Faulkner. William alizaliwa mwaka 1897. Baada ya kushiriki katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Faulkner alirejea tena nchini kwake. Alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake, Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili Wamarekani wenye asili ya Afrika. Hadithi za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa leo nchini Marekani.

Tarehe 6 Julai miaka 59 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Malawi ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kabla ya Malawi kupata uhuru, ilikuwa ikijulikana kwa jina la Nyasaland. Mwaka 1859, makundi ya Wamishonari kutoka Scotland wakiwa pamoja na mvumbuzi David Livingstone waliwasili Nyasaland na kufuatiwa na Uingereza. Uingereza iliunga mkono uvamizi wa Ujerumani na Ureno huko Nyasaland na hatimaye mwaka 1891 nchi hiyo ikawekwa chini ya mamlaka yake. Kwa utaratibu huo Nyasaland ambayo ni Malawi ya leo ikawa miongoni mwa makoloni ya Uingereza katika eneo la Mashariki mwa Afrika. Kijiografia Malawi iko kusini mashariki mwa Afrika ikipakana na nchi za Tanzania, Zambia na Msumbiji.

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, visiwa vya Comoro vilipata uhuru. Raia wengi wa visiwa vya Comoro walianza kuingia katika dini ya Kiislamu na kueneza utamaduni wa dini hiyo visiwani humo, baada ya wafanya biashara wa Kiislamu kuwasili visiwani humo katika karne ya 12 Miladia. Tangu karne ya 16 visiwa vya Comoro vilikuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno na baadaye Sultan wa Oman alifanikiwa kuhitimisha ukaliwaji mabavu wa visiwa hivyo. Hata hivyo mwaka 1842 sehemu kadhaa za visiwa hivyo ziliingia chini ya udhibiti wa Wafaransa na taratibu wakoloni hao wakaidhibiti ardhi yote ya nchi yote hiyo. Mapambano ya wananchi yalipelekea kutangazwa uhuru rasmi wa nchi ya Kiislamu ya Comoro mwaka 1975. Comoro ina ukubwa wa kilomita mraba 1862 na kijiografia inapatikana kusini mashariki mwa bara la Afrika katika bahari ya Hindi.

Na miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sayyid Javad Khamenei, baba wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Alizaliwa katika mji wa Khamenei karibu na Tabriz huko Azerbaijan Mashariki na akaondokea kuwa alimu na fakihi kupitia malezi ya baba yake. Akiwa katika rika la ujana, Sayyid Javad Khamenei alifanya safari katika maeneo matakatifu na akauchagua mji mtakatifu wa Mash’had kuwa makazi yake ya kudumu. Akiwa mjini Mash’had alisoma masomo ya Hawza kwa Ayatullah Aghazadeh Khorasani na al Haj Hussein Qumi na kukwea daraja za kielimu. Aidha akiwa na nia ya kujiendeza zaidi kielimu alifanya safari huko Najaf Iraq na kufanikiwa kusoma kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah Mirza Naini na Abul-Hassan Isfahani. Hatimaye Sayyid Javad Khamenei aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 91 na kuzikwa jirani na haram ya Imam Ridha AS.
