Jumamosi, 08 Julai, 2023
Leo ni Jumamosi tarehe 19 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1444 Hijria, mwafaka na tarehe 8 Julai 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita aliaga dunia Pierre Paul Broca, msomi wa Kifaransa na mwanzilishi wa elimu ya kraniolojia (elimu ya fuu la kichwa). Broca alizaliwa Juni 28 mwaka 1824 huko Ufaransa na baada ya kukamilisha masomo ya msingi na sekondari alijiunga na Chuo Kikuu kwa ajili ya kusoma taaluma ya tiba na kuhitimi vyema katika fani hiyo. Baada ya kuhitimu masomo Broca alijishughulisha na kazi ya upasuaji akiwa daktai mahiri. Sambamba na kazi yake hiiyo aliendelea na utafiiti na uhakiki. Utafiti wake huo ulimfanya afikie ugunduzi muhimu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Muhammad Mahdi Rabbani Amlashi aalimu na mujahidi wa Kiirani. Ayatullah Amlashi alizaliwa mwaka 1313 Hijria Shamsiya katika familia ya kidini katika mji mtukufu wa Qum na kuanza masomo ya kidini katika mji huo. Mwanazuoni huyo alipambana vilivyo kwa miaka mingi katika njia ya kuutetea Uislamu na kulinda thamani zake. Kama walivyokuwa viongozi na wafuasi wengine wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Rabbani Amlashi katika uhai wake hakuacha kufanya juhudi za kupambana dhidi ya utawala wa Shah licha ya kufungwa na kubaidishwa. ***
Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Muhammad Nasih mwanafasihi na mshairi wa Kiirani. Muhammad Ali Nasih alizaliwa mjini Tehran ambapo mbali na kujifunza elimu mpya alijihusisha pia na kusoma elimu za kale. Nasih alikuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kifasihi ya Iran ambapo baadaye alikuwa kiongozi wa jumuiya hiyo hadi anaaga dunia. ***
Na siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, alifariki dunia Kim Il-sung aliyekuwa Kiongozi na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti wa Korea Kaskazini. Kim Il-sung alizaliwa mwaka 1912. Akiwa na cheo cha ukapteni jeshini alirejea kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 1945 akiandamana na jeshi. Alipanda ngazi ya uongozi haraka na akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha wakomunisti wa nchi hiyo. Mwaka 1948 wakati nchi hiyo ilipoasisiwa na kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, Kim Il-sung alifikia cheo cha uwaziri mkuu. Katika vita vya Korea, Kim Il-sung aliteuliwa kuwa kamanda mkuu wa majeshi ya nchi hiyo na mwaka 1972 akawa rais wa taifa hilo.