Jul 09, 2023 02:32 UTC
  • Leo Katika Historia

Leo ni Jumapili Mwezi 20 Mfunguo Tatu Dhul-Hijjah, 1444 Hijria, sawa na tarehe 9 Julai, 2023 Miladia.

Miaka 1316 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Imam Musa Kadhim AS, mmoja wa wajukuu vipenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Mpaka anatimiza umri wa miaka 20, mtukufu huyo alikuwa pamoja na baba yake mpenzi Imam Jaafar Sadiq AS akichota maalumati kwenye bahari yake ya elimu na maarifa. Baada ya kufa shahidi baba yake, Imam Musa Kadhim AS alibeba jukumu la Uimamu na uongozi wa Waislamu kwa muda wa miaka 35, ambapo katika kipindi chote hicho alihimili na kuvumilia tabu na misukosuko mingi. Miaka ya mwanzoni ya Uimamu wa Imam Musa Kadhim, ilisadifiana na kuporomoka kwa utawala wa Bani Umayyah na kushikwa hatamu za utawala na Bani Abbas. Hadi mwisho wa uhai wake akiwa na umri wa miaka 55, mtukufu huyo alishuhudia tawala za makhalifa watano wa Bani Abbas, ambao kila mmoja wao hakusita kuchukua kila hatua ya kuwapiga vita wapinzani wake na kuwakandamiza watetezi wa haki waliokuwa wafuasi wa watu wa Nyumba ya Bwana Mtume SAW. Imam Musa Kadhim AS alitumia sehemu kubwa ya maisha yake kuwasomesha na kuwalea watu kimaadili na kuwaelimisha juu ya utamaduni na mafundisho sahihi ya Uislamu. Lakini kutokana na kumhisi ni hatari kwake, utawala wa Bani Abbas ulimweka gerezani mtukufu huyo ili kuwafanya watu wakose nuru ya uongofu na elimu ya Imamu huyo mwema na kubaki kwenye giza la ujinga na ujahili. Imam Musa Kadhim AS alikuwa alimu mkubwa zaidi na mja mwema na mkarimu zaidi kuliko watu wote wa zama zake. Alipambika kwa khulka njema, huruma na ukarimu usio na kifani na alikuwa maarufu mbele ya watu wote kwa utukufu wa nafsi, ukarimu, moyo wa kutoa kwa siri na kwa dhahiri na kuwasamehe wanaomkosea. Mbali na kutoa mkono wa heri na baraka kwa mnasaba wa kuzaliwa Imamu huyu muadhamu, nakunukulieni maneno mazuri na ya hekima ya mtukufu huyo aliposema: “Njia bora inayomkurubisha mtu kwa Mwenyezi Mungu baada ya kumjua Yeye Mola ni Sala, kuwatendea wema wazazi na kuacha uhasidi na kujiona”.

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, tarehe 9 Julai mwaka 1948 vita kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel vilianza upya baada ya kusitishwa kwa mwezi mmoja. Vita hivyo vilianza mwezi Mei mwaka huo kufuatia kuasisiwa kinyume cha sheria utawala haramu wa Israel lakini vikasitishwa mwezi Juni kwa wito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Katika muda huo wa takribani mwezi mmoja, utawala wa Kizayuni ulipokea shehena nyingi za silaha kutoka kwa waungaji mkono wake wa Magharibi hususan Marekani na ukapata mafanikio makubwa vilipoanza vita tena katika siku kama ya leo. Magenge ya wabeba silaha wa Kizayuni hayakuukubali tena wito mwingine wa usitishaji vita uliotolewa na Baraza la Usalama mpaka yalipofikia malengo yao. Mkataba wa kuacha mapigano na vita ulikuja kusainiwa mwezi Januari 1949 wakati 78% ya ardhi ya Palestina ilikuwa tayari imeshavamiwa na kukaliwa na Wazayuni; na Wapalestina laki saba na nusu wakiwa wameshapoteza makazi yao na kugeuzwa wakimbizi.

Miaka 21 iliyopita katika siku kama ya leo, tarehe 9 Julai 2002, Umoja wa Afrika AU ulichukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika OAU baada ya uamuzi huo kupitishwa na viongozi wa nchi za bara hilo. OAU iliasisiwa mwaka 1962 kwa lengo la kusaidia harakati za kupigania uhuru wa nchi za Afrika na kutatua tofauti zinazozuka baina yao lakini baadaye ikahisika kuwa katika mazingira mapya ya dunia kuna udharura wa kuanzishwa jumuiya yenye ufanisi mkubwa zaidi na malengo mapya zaidi. Kwa mintaarafu hiyo, katika siku kama ya leo mnamo mwaka 2002 viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika walikutana mjini Durban Afrika Kusini na kuasisi Umoja wa Afrika. Ndani ya umoja huo zimeanzishwa taasisi kadhaa ikiwa ni pamoja na Bunge, Kamisheni ya Utekelezaji, Benki Kuu, Mfuko wa Fedha pamoja na Mahakama kwa ajili ya kuratibu na kusaidia ustawi wa kiuchumi wa nchi za Kiafrika. Kuna pia Baraza la Amani na Usalama la AU ambalo hali inapofikia pabaya huwa na uwezo wa kuingilia baadhi ya masuala muhimu ya ndani ya nchi wanachama. Makao Makuu ya Umoja wa Afrika yako mjini Addis Ababa, Ethiopia na mkutano wa wakuu wa wanachama hufanyika huko mara moja kila mwaka.

Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo, njama ya mapinduzi ya kijeshi ya Nouzhe ilifichuliwa.  Njama ya mapinduzi ya kijeshi ya Nouzhe (Kizoro) ilipangwa muda mfupi tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979. Njama hiyo iliyoaandaliwa na shirika la ujasusi la Marekani CIA ilipangwa kutekelezwa na maafisa kadhaa wa jeshi la uliokuwa utawala wa Kifalme wa Shah wa Iran kwa kuhusisha zaidi makamanda wa jeshi la anga na kwa lengo la kumuua Imamu Khomeini (MA) na kuupindua Mfumo mchanga wa Jamhuri ya Kiislamu. Jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi lilipangwa lianzie kwenye kituo cha jeshi la anga cha Shahidi Nouzhe mjini Hamedan, na ndio maana baada ya kufichuliwa na kuzimwa likawa marufu kwa jina hilo la "Mapinduzi ya kijeshi ya Nouzhe". Jaribio hilo la mapinduzi lilipewa jina la Operesheni ya Kizoro, na hatua ya kwanza ya mapinduzi ilikuwa ni kufanya shambulio la anga dhidi ya makazi ya Imamu Khomeini mjini Tehran na kisha kisha kushambulia maeneo na vituo nyeti na hasasi ukiwemo uwanja wa ndege wa Mehrabad mjini Tehran. Hata hivyo jaribio hilo la mapinduzi lilifichuka na waliohusika walikamatwa na kuadhibiwa kwa uhaini wao huo.

Kituo cha anga cha Shahidi Nouzhe, Hamedan

Na Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita tarehe 18 ya mwezi wa nne wa Tir mwaka 1381 kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia ya Iran, Ayatullah Sayyid Kadhim Ikhwan Mar'ashi, mmoja wa wahadhiri wabobezi wa Chuo cha Kidini Hawza cha mjini Mashhad aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 83. Akiwa na umri wa miaka mitano, alifiwa na baba yake aliyekuwa alimu mkubwa, lakini tukio hilo chungu halikuathiri hima na bidii yake kujifunza elimu za dini. Alipotimiza umri wa miaka 32 na baada ya kuishi mjini Qum kwa muda wa miaka 17, Sayyid Ikhwan Mar'ashi alielekea Najaf, ambapo mbali na kuendelea na masomo na kuchota elimu kwa Ayatullah Sayyid Abdulhadi Shirazi, alifanya kazi pia ya kusomesha wanafunzi wa Hawza wa masomo ya ngazi ya juu. Ayatullah Sayyid Kadhim Ikhwan Mar'ashi alitoa mchango mkubwa zaidi wakati vuguvugu la Kiislamu la watu wa Mashhad dhidi ya utawala wa Pahlavi lilipokuwa limepamba moto na nyumba yake ikawa ndio kitovu cha mashauriano na uchukuaji maamuzi. Baadhi ya athari za alimu huyo mwanamapambano ni: Amali za Hija, Muhtasari wa Al-U'rwatul-Wuthqa, Sherhe ya Al-U'rwatul-Wuthqa na uchambuzi wa darsa za Fiqhi za Ayatullah Bourjerdi.

Ayatullah Sayyid Kadhim Ikhwan Mar'ashi