Jul 10, 2023 22:55 UTC
  • Jumanne, tarehe 11 Julai, 2023

Leo ni Jumanne tarehe 22 Dhulhija 1444 Hijria sawa na tarehe 11 Julai 2023.

Tarehe 11 Julai imepewa jina la Siku ya Kimataifa ya Jamii. Siku ya leo inakumbusha tukio la tarehe 11 Julai 1978 wakati idadi ya watu duniani ilipopindukia bilioni 5. Takribani miaka 40 iliyopita, Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza ulitoa mpango wa kupanga na kudhibiti idadi ya watu duniani. Hatua hiyo ilitokana na kuwa, ongezeko la watu linahitajia ustawi wa kudumu, upanuzi wa miji na kupatikana huduma muhimu kama za tiba. Kutokana na uhakika huo, kuna haja kwa mataifa yote ya dunia kuandaa mipango mizuri ili kuhakikisha watu wanaishi maisha salama, umasikini unapungua, kunakuweko na uwiano wa ukuaji na uongezekaji wa idadi ya watu, kuweko familia na jamii salama na ambazo zitaishi katika maisha mazuri na salama zaidi. Siku hii huadhimishwa kila mwaka kama Siku ya Idadi ya Watu Duniani.   

Katika siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Maytham al-Tammar mmoja wa Masahaba na wafuasi wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Awali Maytham al-Tammar alikuwa mtumwa na alinunuliwa na kuachiwa huru na Imam Ali bin Abi Talib (as). Imam Ali alikuwa akimpenda na kumthamini sana Maytham al-Tammar kama ambavyo Maytham pia alikuwa na mapenzi makubwa kwa Imam Ali. Hatimaye katika siku kama ya leo, sahaba huyo mwema wa Mtume (saw) aliuawa kinyama na watawala wa Bani Umayyah kwa kosa la kuwapenda na kuwaunga mkono Ahlul Bait (as). 

Mahali lilipo kaburi la Maytham al Tammar, Kufa, Iraq

Siku kama ya leo miaka 963 iliyopita alifariki dunia malenga na arif mkubwa wa Kiislamu na wa Iran wa karne ya tano Hijria Khaja Abdullah Ansari. Alizaliwa katika mji wa Herat ulioko Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mohabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."

Katika siku kama ya leo miaka 779 iliyopita, mji wa Baitul Muqaddas ulikombolewa na Waislamu wakati wa Vita vya Msalaba. Vita vya Msalaba vilianza mwishoni mwa karne ya 11 Miladia na watu wa Ulaya waliwatwisha Waislamu vita hivyo. Watu wa msalaba walianzisha vita hivyo kidhahiri wakiwa na lengo la kuteka Baitul Muqaddas, ingawa shabaha halisi ya wapiganaji hao ilikuwa ni kudhibiti ardhi kubwa za Waislamu na kuwanyonya na kuwakoloni wafuasi wa dini hiyo. Katika vita hivyo wafuasi wa kanisa walichora alama za msalaba kwenye mabega na mavazi yao, na kwa sababu hiyo vita hivyo vimekuwa maarufu kwa jina la Vita vya Msalaba. 

Miaka 466 iliyopita katika siku kama ya leo, Sebastian Cabot mvumbuzi na mwanabaharia wa Kiitalia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81. Tangu awali alikuwa akifanya safari na baba yake aliyekuwa mwanabaharia na kwa msingi huo akafanikiwa kujifunza mambo mengi yanayohusiana na ubaharia. 

Sebastian Cabot

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, nchi ya Mongolia ilijitangazia uhuru. Mongolia ina historia kongwe mno. Changiz Khan Moghol alianza kuziteka ardhi za nchi hiyo mwanzoni mwa karne ya 13 na kusonga mbele hadi Ulaya ya mashariki. Mongolia iligawanyika katika sehemu mbili yaani Mongolia ya nje na ya ndani baada kusambaratika utawala wa kifalme wa Wamogholi. Mongolia ya ndani iliijumuisha China, na Mongolia ya Nje ikawekwa chini ya udhibiti wa China mwishoni mwa karne ya 17.   

Bendera ya Mongolia