Mapinduzi ya Kiislamu na Maendeleo ya Kiuchumi
Kipindi chetu juma hili kinaangazia Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na maendeleo ya kiuchumi kwa mnasaba wa siku hizo za maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Moja ya sababu muhimu za kutokea Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni hali mbaya ya kiuchumi na dhulma kubwa iliyokuwa ikitawala jamii. Sehemu kubwa ya mapato mengi ya mafuta katika kipindi cha kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ilitumiwa kwa ajili ya anasa na kutajirisha familia ya kifalme na jamaa zake, na vilevile kununua zana za kijeshi kupita kiasi, huku sekta nyingine muhimu kama kilimo, elimu na afya zikiendelea kufifia na kudidimia.
Kwa upande mwingine, mfumuko wa bei na ughali wa maisha ulikuwa ukiongezeka, na ufukara na umaskini vilionekana waziwazi katika sehemu mbalimbali za nchi. Baada ya kupata ushindi, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalilipa kipaumbele suala la kuboresha hali ya uchumi na kufikisha ustawi na maendeleo kwa wananchi. Hata hivyo kazi hii ilikuwa ngumu sana, kwa sababu hakukuwa na miundombinu inayofaa ya kiuchumi, mapato ya serikali yalitegemea bidhaa ya mafuta tu, na umaskini hasa katika maeneo ya mbali na vijijini, uliwafanya watu wateseke na kuishi kwenye tabu.
Wakati huo huo, machafuko ya ndani na mashinikizo ya nje yalifanya iwe vigumu kutekeleza mipango inayofaa ya ustawi wa uchumi na vita dhidi ya umaskini. Hata hivyo, takriban mwaka mmoja na nusu baada ya ushindi wa Mapinduzi Kiislamu, Saddam Hussein, mtawala wa kidikteta na mbabe wa Iraq, alianzisha vita vikali dhidi ya Iran, ambavyo vilishughulisha suhula nyingi na nguvu kazi hai ya Iran kwa muda wa miaka minane na kusababisha uharibifu mkubwa kwa uchumi wa nchi. Vilevile Marekani na washirika wake ambao walipata kipigo kikubwa kutokana na harakati ya kupambana na dhulma ya wananchi wa Iran, waliiwekea Iran vikwazo vya pande zote tangu mwanzoni mwa ushindi wa harakati hiyo. Vikwazo hivyo viliongezwa kadiri muda ulivyopita na sasa Washington imeiwekea Iran vikwazo vikubwa na vikali zaidi.

Pamoja na hayo, utawala wa Kiislamu na wananchi wanamapinduzi wa Irani hawakusalimu amri, kwa kadiri kwamba, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Fedha la Kimataifa ya 2022, Iran ilishika nafasi ya 22 kama nguvu kubwa ya kiuchumi duniani kwa kuwa na pato ghafi la taifa la dola trilioni moja na bilioni 596 kwa mwaka huo. Pia, Benki ya Dunia imetangaza kuwa ustawi wa uchumi wa Iran mwaka 2023 iliimarika kwa asilimia 4.1. *****
Kwa ujumla, inaonekana kwamba viashiria vingi vya kiuchumi vya Iran vinakua na kuimarika. Serikali, sambamba na kujaribu kukabiliana na mfumuko wa bei, imeweka kipaumbele katika sera kuu mbili, ambazo ni kusaidia uzalishaji wa ndani na kuongeza mabadilishano ya kibiashara, hasa na nchi jirani. Wakati huo huo, ustawi wa bidhaa za makampuni yanayotegemea elimu na sayansi umekuwa kwa kiasi kikubwa, na katika suala hili, idadi ya makampuni hayo imeongezeka karibu mara mbili hadi kufikia mwaka jana. Kadhalika, kiwango cha mabadilishano ya kibiashara ya Iran na nchi nyingine kimeongezeka mara kadhaa ikilinganishwa na kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na mauzo ya mafuta nje ya nchi yamepungua; kinyume chake, usafirishaji wa bidhaa zinazotokana na mafuta na zisizo za mafuta umeongezeka sana. Kiwango cha mauzo na uagizaji wa bidhaa zisizo za mafuta ya Iran meongezeka kwa zaidi ya 11% na kufikia dola bilioni 112.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imepata maendeleo makubwa katika sekta ya viwanda na madini, ambayo hayawezi kulinganishwa na kipindi cha kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Maelfu ya viwanda vidogo na vikubwa vinajishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za aina mbalimbali, na ubora na wingi wa uzalishaji wao umeongezeka sana ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Vitengo vikubwa zaidi vya viwanda vya Iran vinafanya kazi katika kuzalisha mafuta na madini. Viwanda vikubwa vya petrokemikali vya Iran sasa vina uwezo wa kubeba takriban tani milioni 95, ambazo zitaongezeka maradufu kwa kuzinduliwa viwanda vipya. Mwaka jana, mapato ya mauzo ya nje ya bidhaa za petrokemikali yalikuwa dola bilioni 16, na maafisa wa sekta hiyo wanajaribu kupunguza utegemezi wa nchi kwa mafuta ghafi kwa kuongeza kasi katika uuzaji wa bidhaa zinazotokana na petroli nje ya nchi. Sera hii kwa upande mwingine, inaweza kupunguza athari mbaya za vikwazo haramu vya Marekani dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran.
Katika uwanja wa sekta ya madini, Iran imekua na kustawi kwa kiasi kikubwa. Kwa sasa, asilimia saba ya migodi ya madini duniani yenye thamani ya takriban dola bilioni 770 imegunduliwa nchini Iran. Uuzaji wa bidhaa za migodi hiyo mwaka jana uliingiza zaidi ya dola bilioni 12. Kwa kuzingatia thamani kubwa ya bidhaa za migodi ya Iran, maafisa wa sekta hiyo wametayarisha mipango mingi ya kukuza uzalisha katika tasnia hiyo. Kwa sasa Iran inashika nafasi ya tano katika uga wa uzalishaji wa shaba, na ni nchi ya kumi duniani kwa uzalishaji wa Madini ya chuma (iron ore). Vilevile, Iran inashika nafasi ya nane duniani kwa kuzalisha tani milioni 62 za saruji na inashika nafasi ya tano duniani katika uzalishaji wa kauri. ****
Moja ya maeneo mengine muhimu ya maendeleo ya Iran ni ujenzi wa mabwawa. Wakati utawala wa kifalme wa Pahlavi kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ulikuwa umejenga mabwawa 19 tu, tena kwa msaada wa wataalamu wa kigeni, sasa mabwawa mara kumi zaidi ya idadi hiyo yamejengwa hapa nchini kwa juhudi za wataalamu wa Iran na kwa teknolojia ya kisasa. Ujuzi wa wataalamu hao wa Iran ni mkubwa kiasi kwamba sasa wanajishughulisha na kusanifu na kusimamia ujenzi wa mabwawa katika nchi 16.
Mwaka 2022 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi tano zinazoongoza duniani katika uga wa teknolojia ya nano. Ustawi huo wa Iran ulithibitishwa katika utafiti wa kimataifa ambapo, orodha mpya iliyopewa jina la "Focus on Emerging Areas of Technology" ilibaini kuwa Iran ni ya tano duniani katika teknolojia ya nano. Mbali na Iran kuwa mojawapo ya nchi bora katika uzalishaji bidhaa nyingi zaidi za teknolojia ya nano, vilevile imehesabiwa kuwa ni miongoni mwa nchi bora kwa mtazamo wa viwango vya kisayansi katika sekta hiyo.
Ripoti ya Tume ya Kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Ajili ya Afrika ya Aprili 2020 ilitangaza kuwa Iran iko katika kundi moja na Marekani, China na Umoja wa Ulaya katika teknolojia ya nano. Ripoti hiyo ilisema, nchi za Afrika zinaweza kuiga Iran kwa kuweka miundo msingi ya utafiti katika sekta ya teknoljia ya nano.

Ripoti hiyo ilisema Iran iko pamoja na nchi zilizostawi ambazo ni Marekani, China, Uingereza, Russia pamoja na Umoja wa Ulaya katika kuweka viwango vya juu kabisa kitaifa katika uga wa teknolojia ya nano.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, nano ni teknolojia ya kisasa inayohusu matumizi ya vitu vidogo sana na miundo yake inapimwa kuwa kati ya nanomita 1-1000. Asili ya Nano ni nanomita ambayo ni kipimo cha sehemu ya bilioni moja ya mita. Hii ina maana ya vitu ambavyo ni vikubwa kuliko atomu na vidogo mara 1000 kuliko upana wa unywele. ****