Apr 12, 2024 12:12 UTC
  • Netanyahu anataka kubadilisha uwanja wa mchezo

Hamjambo na karibuni katiika kipindi chetu cha wiki hii cha Makala ya Wiki kinachobeba anwani: Netanyahu anataka kubadilisha uwanja wa mchezo.

Shambulio la kigaidi lililofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus siku ya Jumatatu, Aprili 1, na kuuawa shahidi washauri kadhaa wa kijeshi wa Iran, limekabiliwa na upinzani mkali wa kimataifa katika ngazi za kieneo na dunia. Nchi mbalimbali zimelaani shambulizi hilo zikisisitiza kwamba vituo vya kidiplomasia havipaswi kulengwa kwa mashambulizi, na kwamba kitendo hicho cha Israel kimekiuka sheria za kimataifa. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia Jumanne wiki iliyopita lilifanya mkutano wa dharura kuchunguza uhalifu huo. Mkutano huo uliitishwa baada ya kuwasilishwa malalamiko ya Iran katika Baraza la Usalama la UN kwa sababu ya kukiukwa Mkataba wa Vienna wa 1961. Kulingana na mkataba wa 1961, majengo ya ubalozi ni miongoni mwa vituo vyenye kinga ya kidiplomasia.

Shambulio la anga la utawala wa Kizayuni katika ubalozi mdogo wa Iran, Syria 

Baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na kuvunjwa mwavuli wa kiusalama, kijeshi na kijasusi wa utawala haramu wa Israel, utawala wa Kizayuni umefanya jinai zote zinazowezekana ili kufidia kushindwa huko kwa kuvamia eneo la Ukanda wa Gaza. Hata hivyo, kadiri Wazayuni wanavyoendelea na jinai zao huko Gaza, ndivyo sura yao halisi ya ulaghai na utenda jinai inavyodhihirika katika uga wa kimataifa na maoni ya umma. Uvamizi wa utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza umefungua nyanja mpya za mapambano dhidi ya utawala huo. Hizbullah kutoka kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Muqawama wa Kiislamu wa Iraq na Yemen unalenga vituo vya kijeshi na kiuchumi vya Israel kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu; na Mlango Bahari wa Bab al-Mandab sio salama tena kwa meli zinazokwenda kwenye bandari za utawala huo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio kitovu cha Muqawama wa Kiislamu na harakati za ukombozi katika kanda hii ya Magharibi mwa Asia. Katika miongo mitatu iliyopita Muqawama wa Kiislamu umebadilisha milingano wa nguvu katika eneo la Mashariki ya Kati. Muqawama huo ndio ulioiwezesha Hizbullah kuwafurusha wanajeshi wa Israel kusini mwa Lebanon mwaka  2000, na Ukanda wa Gaza mwaka 2005. Mnamo mwaka 2006, Hizbullah ya Lebanon ilipata ushindi mnono na usio na kifani katika historia ya kuwepo utawala huo bandia katika vita vya siku 33. Katika vita vya sasa vya Gaza pia Muqawama wa Kiislamu umetoa kipigo kikubwa kwa jeshi la Israel ambacho hakina kifani katika historia ya utawala huo bandia ulioishia kuua wanawake, watoto wadogo na raia wa kawaida kwa ujumla. 

Hizbullah ya Lebanon 

Uwezo huo mkubwa wa makundi ya Muqawama ni matokeo ya ujasiri wa vikosi vya muqawama na msaada na himaya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sasa Wazayuni wanajua kwamba Iran iko katikati ya mhimili wa Muqawama. Wakati huo huo, kila moja ya pande zinazounda mhimili huo inautandika na kutoa vipigo murua kwa utawala wa Kizayuni katika mahali na wakati mwafaka. Licha ya misaada ya pande zote ya Marekani na nchi nyingine za Magharibi kama Uingereza na Ujerumani, Israel inakabiliwa na mashinikizo kutoka kila upande, na ili kujiondoa katika mashinikizo hayo, inahitaji kupanua vita na kugeuza uvamizi wa Gaza na mauaji ya Wapalestina kuwa vita vya kieneo. Kwa msingi huo baada ya kunasa kwa miezi kadhaa huko Gaza, Netanyahu na genge lake la kibaguzi wamekuwa wakijaribu kufungua uwanja mpya wa vita bila mafanikio. Utawala wa Netanyahu, ambao unakabiliwa na migogoro ya ndani na maandamano ya kila siku, umechagua mkakati wa mauaji ya kigaidi na upanuzi wa vita ili kujinasua katika kinamasi cha Gaza. Katika muktadha huo, katika miezi michache iliyopita, idadi ya washauri wa kijeshi wa Iran wameuawa shahidi huko Syria na Lebanon kwa kutumia ndege za kisasa za kivita na makombora ya kutoka Marekani.

Maandamano dhidi ya Netanyahu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu 

Wazayuni wanadhani kuwa, mchezo huo unaweza kuipa Israel ushindi maradufu. Kwani wakati huu ambapo maoni ya umma ya walimwengu yanaendelea kusikitishwa na mauaji na mateso ya Wapalestina na kusimama kidete wapiganaji shupavu wa Muqawama kukabiliana na mauaji ya halaiki ya Israel, utawala wa Kizayuni unajaribu kuuhamisha mtizamo huo wa walimwengu kutoka Gaza na kuuelekeza kwingine; na hivyo kulipa jeshi lake lililochoka nafasi ya kupumua. 

Israel imekwama huko Gaza, kama ilivyotabiriwa hapo awali, Netanyahu yuko chini ya shinikizo la ndani na nje, na mwisho wa vita vya Gaza bila kuangamizwa harakati ya Hamas, kama alivyoahidi, ni kielelezo cha kifo chake cha kisiasa. Hapa ndipo inaposadiki kauli tulioyosema mwanzoni mwa kipindi hiki, kwamba Netanyahu anajaribu kubadilisha na kupanua uwanja wa vita na kisha kubadilisha pande za vita vivyo kutoka Palestina-Israel hadi Iran-Marekani! Shambulizi dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus linaweza kuwa kiashiria kuwa Netanyahu amefikia mwisho.

Alaa kulli hal, kubadilisha milingano ya kisiasa na kiusalama  kutokana na nguvu ya Muqawama katika eneo la Mashariki ya Kati, kumewafanya Wazayuni na waungaji mkono wao wa Marekani na Ulaya washindwe kutimiza malengo ya utawala ghasibu wa Israel. Azma ya nchi kadhaa za Ulaya ya kulitambua rasmi taifa la Palestina ni matokeo ya ukweli huo. Muqawama na mapambano ya Kiislamu ya Palestina hauwezi kuangamizwa wala kupuuzwa. Vilevile jaribio la Netanyahu la kupanua vita kwa kutumia sera ya mauaji ya kigaidi dhidi ya washauri wa kijeshi wa Iran na viongozi wa Muqawama huko Syria na Lebanon hayatazaa matunda yanayotarajiwa. 

Tags