Apr 27, 2024 13:51 UTC
  • Oparesheni Ahadi ya Kweli katika Vyombo vya Habari

Mashambulio ya ndege zisizo na rubani (droni) na makombora ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni wiki iliyopita yaliakisiwa na vyombo vya habari vya nchi ajinabi tangu dakika za mwanzo baada ya kutekelezwa. Katika kipindi hiki, tunatupia jicho radiamali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusua mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel.

Siku kadhaa zilizopita vyombo vya habari vya kikanda na kimataifa viliakisi sana oparesheni ya kulipiza kisasi ya droni na makombora ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) lilianza kutekeleza oparesheni dhidi ya utawala wa Israel usiku wa Jumamosi Aprili 13. IRGC ilitekeleza oparesheni hiyo ya "Ahadi ya Kweli" ikijibu shambulio la kigaidi la utawala huo katika ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus, mji mkuu wa Syria. Oparesheni hiyo iliwafanya Wazayuni wakabiliwe na usiku wa aina yake kuwahi kushuhudia tangu kuasisiwa kwa utawala huo bandia. Tukio hilo muhimu na la aina yake liliakisiwa na kuzungumziwa kwa mapana na vyombo mbalimbali vya habari duniani tangu mwanzo kabisa lilipoanza; ambapo hadi sasa marefu, na vyombo hivyo vya habari vinaendelea kuzungumzia oparesheni hiyo ya IRGC. 

Makombora ya balistiki ya IRGC 

Televisheni ya NBC News ya Marekani ulitangaza habari kuhusu mashambulizi ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni chini ya anwani "Ulipizaji kisasi wa Iran" na kuandika: Shambulio la Iran lilikuwa ni la kwanza kuwahi kutekelezwa  moja kwa moja dhidi ya Israel. Shambulio hilo limetekelezwa wiki chache baada ya hujuma ya Israel kwenye jengo la ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus ambalo lililouwa wawakilishi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC), na Tehran iliahidi tangu awali kuwa italipiza kisasi."  

Jarida la Economist, sawa na vyombo vingine vya habari, lilizungumzia ukubwa wa mashambulizi ya Iran na kuandika katika tovuti yake kuwa: Waisraili wameonja tajiriba ya usiku wa hofu na wahka. Hata kama shambulio la Iran lisingesababisha vifo vingi na hasara kubwa, lakini taathira zake ni kubwa sana." 

Wakati huo huo shirika la habari la Associated Press liliashiria katika ripoti yake kuhusu hatua ya Iran ya kutishia kulipiza kisasi hujuma ya kigaidi ya Israel na kusema linaitambua hatua hiyo ya Iran kama jibu la kawaida na kusistiza kuwa Iran ilianza kutekeleza mashambulizidi dhidi ya Israel kwa kurusha droni zaidi ya 100 na kisha ikaendeleza mashambulizi kwa kutumia makombora yenye uharibifu ya balistiki. 

Katika upande mwingine, vyombo vya habari vya Kiarabu vilikuwa na maoni tofauti kuhusu tukio hilo. Kwa mfano, televisheni ya al  Jazeera ya Qatar ilimnukuu mwandishi wake wa Tehran na kuripoti kuwa kumefanyika mashambulizi mseto dhidi ya utawala wa Israel na kwamba Iran imekanyaga na kupuuza mistari myekundu ya Wazayuni. 

Ripota wa al Jazeera pia alisema: Kinachotokea sasa si "hatua ya kupita" na kwamba hatua ya Tehran ya kutoa jibu la wazi kwa Israel kutoka katika ardhi ya Iran inaweza kufuatiwa na changamoto; Lakini Tehran inasema imejiandaa kwa changamoto hizo."

Televisheni ya Al Arabiyya ya Saudi Arabia pia ni kati ya vyombo vya habari vilivyozungumzia tukio hilo. Televisheni hiyo iliashiria onyo la jeshi la Iran kwa nchi za eneo la Magharibi mwa Asia iwapo zitausaidia utawala wa Israel na kuwanukuu maafisa wa jeshi la Iran wakisema: "Tutaishambulia nchi yoyote itakayowapatia Wazayuni anga na ardhi yake kuishambulia Iran." 

Nalo Shirika la habari la Baratha la Iraq lilimnukuu mtaalamu wa masuala ya kistratijia, Nasim Abdullah, na kuandika kuwa, malengo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamefikiwa kupitia operesheni yake yya kijeshi dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.

Hii ni katika hali ambayo vyombo vya habari vya nje ya nchi vya lugha ya Kifarsi vilijaribu kueneza hofu kuhusu jibu la Iran kwa mashambulizi ya Wazayuni katika ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus na kutoa uchambuzi na tathmini zisizo na mashiko. 

Shambulio la kigaidi la Israel katika ubalozi mdogo wa Iran, Damascus 

Vyombo hivyo vya habari vya lugha ya Kifarsi vyenye makao yake mjini London, viliakisi pakubwa habari zinazohusiana na matamshi ya uungaji mkono wa maafisa wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni, na kujaribu kuidhihirisha Iran kuwa dhaifu. 

Kwa mfano, Radio Farda inayomilikiwa na serikali ya Marekani na kutangaza kwa lugha ya Kifarsi iligusia kutoridhishwa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) na eti kutojulishwa viongozi wa Washington kabla yya shambulio la utawala wa Kizayuni dhid ya ubalozi mdogo wa Iran kuripoti kuwa: Licha ya kutoridhishwa huko, Rais na viongozi wengine wa Marekani wamesisitiza kuwa nchi hiyo itaihami na kuilinda Israel mbele ya shambulio lolote la Iran. Iliripoti kuwa: Kufuatia matukio ya karibuni, inaonekana kuwa viongozi wa kijeshi na usalama wa pande hizo mbili wanashirikiana kwa karibu ili kujibu mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran. 

Hapana shaka kwamba kuingia ndege zisizo na rubani na makombora ya Iran ndani kabisa ya ardhi zilizokaliwa kwa mabavu za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel mbali na kufichua ngano ya kutoshindwa mfumo wa kujikinga na makombora wa Iron Dome ilikuwa vilevile ilikuwa adhabu kwa Tel Aviv. Suala hili liko wazi kiasi kwamba baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi vilishindwa kulipuuza na kulifumbia macho. Alon Ben David, mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa gazeti la Maariv la Israel amesema: "Iran imeingia katika hatua nyingine katika vita dhidi ya Israel, na ni lazima tukubali dhana kwamba Iran iko tayari kufanya mashambulizi makubwa zaidi. Wakati wa shambulio la Iran, hofu na wasiwasi vilitawala katika kambi za anga ambazo zililengwa na makombora. Maelfu ya askari walijificha kwenye mahandaki, wakijiuliza iwapo sakafu ya zege za mahandaki hayo zinaweza kustahamili makombora mazito ya Iran".  

 

Tags