Historia ya Maisha ya Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi
May 20, 2024 08:42 UTC
Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na viongozi kadhaa aliofuatana nao wamekufa shahidi katika ajali ya helikopta iliyotokea jana Jumapili katika eneo la Varzghan mkoani Azerbaijan Mashariki wakiwa katika kazi ya kuwahudumia na kuwatumikia wananchi.
Katika ajali hiyo ya ndege, Rais Sayyid Ebrahim Raisi na walioandamana naye, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian, Ayatullah Sayyid Mohammad Ali Al-Hashem, Imamu wa Ijumaa wa Tabriz, Malik Rahmati, Gavana wa Azerbaijan Mashariki, pamoja na timu ya walinzi wa rais, marubani na wafanyakazi wa helikopta wamekufa shahidi.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Sahab, Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alizaliwa Desemba 1960 katika ukoo wa Mashekhe katika mji wa Mashhad kwenye kitongoji cha Noghan.
Baba yake Hujjatul-Islam Sayyid Haj Raees Al-Sadati na pia mama yake Sayyidah Esmat Khodadad Hosseini wanatoka kwenye ukoo wa Masharifu wa Hosseini na nasaba yake kwa ubabani na umamani inafikia kwa Mtukufu Zayd bin Ali Ibnul-Hussain (AS).
Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi, ambaye aliishi maisha ya uyatima kwa kuondokewa na baba yake akiwa na umri wa miaka mitano, alipata elimu yake ya msingi katika Skuli ya Jawadiyyah na akaanza masomo yake ya kidini katika Madrasa ya Nawwab na baadaye katika Madrasa ya Ayatullah Mousavinejad.
Kwa ajili ya kuendelea na masomo, mnamo mwaka 1975, Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi alielekea Chuo cha Kidini, Hawza cha Qom na kuanza masomo katika Madrasa ya Ayatullah Boroujerdi; na kwa muda fulani alisoma pia katika Madrasa iliyokuwa ikiendeshwa na Ayatullah Pasandide chini ya usimamizi wa Imamu Khomeini (MA).
Kufuatia kitendo cha kuvunjiwa heshima Imam Khomeini (MA) kilichofanywa na toleo la Juni 7, 1978 la gazeti la Ettelaat na kuanza harakati kubwa ya wananchi, Sayyid Ebrahim Raisi alishiriki kwenye mikusanyiko na maandamano ambayo mengi yao yalianzia katika Madrasa ya Ayatullah Boroujerdi (Madrasa ya Khan), na kuendesha harakati kupitia vikundi vidogovidogo vya wanafunzi wanamapinduzi wa kidini.
Katika kipindi hicho, Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi aliendelea na harakati zake za mapambano kupitia mawasiliano aliyokuwa akifanya na maulamaa wanamapinduzi walioachiliwa huru kutoka jela au waliobaidishwa na kupelekwa uhamishoni, na akawa anashiriki pia katika mikusanyiko mbalimbali ikiwemo migomo ya kuketi iliyofanywa na maulamaa na wanafunzi wa kidini katika Chuo Kikuu cha Tehran.
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Sayyid Ebrahim Raisi alishiriki katika mafunzo maalumu yaliyoendeshwa na Marehemu Shahidi Beheshti kwa ajili ya kuandaa kada ya wafanyakazi wa kukidhi mahitaji ya uongozi na uendeshaji wa Mfumo wa Kiislamu; na kufuatia ghasia zilizoanzishwa na mrengo wa Umaksi na vitimbi mbalimbali ulivyoanzisha katika Msikiti wa Suleiman, yeye pamoja na kundi la wanafunzi wenzake wa kidini walielekea eneo hilo kuendesha harakati za kiutamaduni. Baada ya kurejea kutoka Msikiti wa Suleiman, alianzisha majimui ya kisiasa na kiitikadi ya kambi ya mafunzo iitwayo Safar-2 huko Shahrood na kuiendesha kwa kipindi kifupi.
Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi aliingia kwenye uga wa uongozi mwaka 1980 akiwa Mwendsha Mashtaka Msaidizi wa mji wa Karaj; na baada ya muda, akateuliwa na Shahidi Qoddusi kuwa Mwendesha Mashtaka wa mji huo.
Baada ya miaka miwili, mnamo mwaka 1982 Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi alihudumu pia wadhifa wa Mwendesha Mashtaka wa Hamedan akiwa pia Mwendesha Mashtaka wa mji wa Karaj na akatumikia nyadhifa hizo mbili hadi mwaka 1984.
Mnamo mwaka 1985, Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi aliteuliwa kuwa Naibu Mwendesha Mashtaka wa Mapinduzi wa Jiji la Tehran; na ndipo kilipoanzia kipindi cha uongozi wake katika Idara ya Mahakama.
Mwaka 1994, Sayyid Ebrahim Raisi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Shirika Kuu la Ukaguzi nchini na akaendelea kushika wadhifa huo kwa muda wa miaka 10.
Kipindi cha uongozi wa Sayyid Ebrahim Raisi katika Shirika Kuu la Ukaguzi nchini kilikuwa muhimu mno na cha mabadiliko makubwa katika maisha yake, ambapo kwa kutumia hazina ya tajiriba na uzoefu aliokuwa nao alileta mabadiliko makubwa na yenye nidhamu makini katika usimamizi wa vyombo vya kiidara.
Kuanzia mwaka 2004 hadi 2014, Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi alihudumu katika wadhifa wa Naibu Mkuu wa Kwanza wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuanzia mwaka 2014 hadi 2015 alishika wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa nchi.
Mwaka 2012 Sayyid Ebrahim Raisi aliteuliwa pia na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa Mwendesha Mashtaka Maalumu wa Mahakama za viongozi wa dini na kushikilia wadhifa huo hadi mwaka 2021.
Mnamo mwezi Machi 2016 Shahidi Raisi aliteuliwa na Ayatullahil-Udhma Khamenei kushika kwa muda miaka mitatu wadhifa wa kusimamia Taasisi ya Qods Razavi, ambapo katika kipindi hicho alichukua hatua athirifu za kuishughulikia Haram Tukufu ya Imam wa Nane, Mtukufu Ali Ibin Musa Ridha AS na kuanzisha mfumo na utaratibu mzuri sana wa utoaji huduma kwa wafanyaziara wa Haram hiyo takatifu iliyoko kwenye mji mkuu wa kidini wa Iran ya Kiislamu.
Mnamo Machi 7, 2019 Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi aliteuliwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi kuwa Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran; na utendaji wa Mahakama wakati wa uongozi wake, ulipelekea kwa sababu kadhaa kupanda kiwango cha utendaji katika mfumo wa uendeshaji nchi katika Jamhuri ya Kiislamu.
Kutokana na utaratibu wa Sayyid Ebrahim Raisi wa kushughuikia mambo mahala husika, kufuatilia kwa karibu shida na matatizo ya wananchi, kuwachukulia hatua kali na bila mzaha mafisadi wa kiuchumi, kuandaa na kukamilisha hati ya mabadiliko ya Idara ya Mahakama na kuasisi mfumo erevu katika Idara hiyo, hatua kubwa na za maana zilipigwa katika kuinua kiwango cha utekelezaji haki na uadilifu kwenye vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu, kiasi kwamba Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi alisifu mabadiliko hayo yaliyojenga matumaini ndani ya nyoyo za wananchi.
Mwaka 2021 Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi alishika wadhifa wa Urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kupata ushindi wa zaidi ya kura milioni 18 za wananchi katika uchaguzi wa 13 wa Rais uliofanyika tarehe 28 Juni.
Rekodi za kitaaluma za Sayyid Ebrahim Raisi ni hizi zifuatazo: Daraja ya nne ya Elimu katika Fiqhi na Usuli kutoka Chuo Kikuu cha Kidini cha Qom, Shahada ya Uzamivu ya Fiqhi na Misingi ya Sheria katika uga wa Sheria za Binafsi kutoka Chuo Kikuu cha Shahid Motahari, ufundishaji taaluma ya fiqhi na sheria katika ngazi ya juu, fiqhi ya mahakama na fiqhi ya kiuchumi katika Vyuo Vikuu vya Tehran na Vyuo Vikuu vingine nchini na kufundisha kwa muda wa miaka miwili katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Khorasan kozi za fiqhi ya kiwango cha juu kabisa katika maudhui za waqfu, nadhiri na kuamrisha mema na kukataza maovu.../