Muhammad bin Zakaria Razi, Tabibu na Mkemia wa Rei
https://parstoday.ir/sw/radio/uncategorised-i14128-muhammad_bin_zakaria_razi_tabibu_na_mkemia_wa_rei
Tarehe 5 Shahrivar inayosadifiana na 26 Agosti ni siku aliyozaliwa Muhammad bin Zakaria Razi, msomi, tabibu na mkemia mkubwa wa Kiislamu na Kiirani katika karne ya tatu Hijria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 28, 2016 07:58 UTC
  • Muhammad bin Zakaria Razi, Tabibu na Mkemia wa Rei

Tarehe 5 Shahrivar inayosadifiana na 26 Agosti ni siku aliyozaliwa Muhammad bin Zakaria Razi, msomi, tabibu na mkemia mkubwa wa Kiislamu na Kiirani katika karne ya tatu Hijria.

Razi alizaliwa katika mji wa Rei nchini Iran mwaka 251 Hijria sawa na mwaka 865 Miladia katika zama za utawala wa Wasamani na kipindi cha karne za kati barani Ulaya. Mji wa Rei una historia ya miaka mingi na ulikuwa na wakazi katika kipindi cha zaidi ya miaka elfu tatu kabla ya kuzaliwa Nabii Isa Masiih (as). Baba wa historia ya elimu, George Sarton, anasema: Muhammad Zakaria Razi alikuwa daktari mkubwa zaidi wa Kiislamu katika karne za kati. Naye mtaalamu wa historia ya elimu, Julius Ruska amesema: Razi ndiye baba wa elimu ya kemia na mwasisi wa mfumo mpya wa sayansi. 

Muhammad bin Zakaria Razi

Zakaria Razi alisifika sana kwa uhodari na uwezo wake mkubwa wa kihifadhi na kushika mambo mengi kichwani mwake. Ameandika katika kitabu chake alichokipa jina la "Shaka Kuhusu Galinos" (Doubts About Galen) akisema: "Katika ujana wangu nilikuwa na hamu kubwa ya kufanya majaribio ya vitu mbalimbali". Ni hamu hii kubwa ya Razi ndiyo iliyomuelekeza katika elimu ya kemia na kugundua mada iliyobadili chuma cha kawaida na kukifanya chuma chenye thamani kubwa hususan dhahabu. Hata hivyo wakati anafanya kazi na majaribio ya mada za kemikali na karibu na moto, macho ya Razi yalipatwa na madhara. Hivyo aliamua kwenda kwa daktari kutibu macho yake. Gharama ya matibu yake wakati huo ilikuwa karibu dinari mia tano, ambazo zilikuwa fedha nyingi sana kipindi hicho. Wakati alipokuwa akilipa gharama za matibabu, Zakaria Razi alijisemeza mwenyewe kwamba: "Hii ndiyo kemia na si kazi unayoifanya wewe kwa sasa ewe Razi"!

Tangu wakati huo Muhammad Zakaria Razi aliacha elimu ya kemia na kuanza kusoma elimu ya utabibu. Alifanya jitihada kubwa kwa ajili ya kufikia muradi wake. Mtu mmoja aliyeishi na Razi mjini Rei anasema: "Siku zote alitembea na kalamu na karatasi na daima alionekana akiandika". 

Razi aliamua kuelekea Baghdad nchini Iraq kwa ajili ya kupata elimu zaidi. Zama hizo mji wa Baghdad ulikuwa na hospitali nyingi, na wanafunzi wa tiba walipata fursa ya kutekeleza kivitendo waliyoyasoma darasani. Katika upande mwingine, utawala wa Baghdad ulitenga kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya madaktari na wasaidizi wao na vilevile kwa ajili ya kutengeneza dawa. 

Razi alikuwa msomi hodari na mwenye bidii. Ameandika katika kitabu chake cha Mwenendo wa Falsafa kwamba: "Nilitumia miaka 15 ya umri wangu kuandika tabu kubwa la  al-Hawi fi al-Tibb hadi nikapatwa na udhaifu katika macho yangu na mshipa wa mkono wangu ukashindwa kufanya kazi na hatimaye nikashindwa kuandika. Hata hivyo sikuacha kufanya jitihada kubwa za kutafuta elimu na niliendelea kusoma na kuandika kwa msaada wa huyu na yule".

Razi alipata umashuhuri mkubwa wa kimataifa katika kipindi kifupi kwa kadiri kwamba watawala na wafalme wa zama hizo walianza kumwita na kumwalika. Alikubali wito wao na wakati mwingine kuandikia vitabu kwa majina yao. Miongoni mwa vitabu alivyowaandikia watawala wa zamani hizo ni kile cha  Kitab al-Mansuri fi al-Tibb (Liber Almansoris au Liber Medicinalis) aliporejea Rei kwa wito wa Abu Saleh bin Mansur bin Is'haq wa utawala wa Wasamani na kukubali kuwa mkuu wa hospitali ya mji huo. Kitabu hicho ni miongoni mwa vitabu mashuhuri zaidi vya Razi barani Ulaya.    

Licha ya uhusiano wake wa karibu na watu wakubwa na watawala wa zama hizo, Muhammad bin Zakaria Razi alikuwa mtu wa watu wa kawaida na alikuwa mwema na mwenye huruma sana kwa watu maskini na wasiojiweza. Mwanahistoria Ibn Nadiim ameandika katika kitabu chake mashuhuri cha al-Fihrist kwamba: "Razi alikuwa mwema na mpole kwa watu wote hususan maskini na wagonjwa wake. Alikuwa akiwatembelea na kuwajulia hali wagonjwa wake wasiojiweza na kuwatengea kiwango kikubwa cha fedha", mwisho wa kunukuu.

Alkemi

Zakaria Razi ameandika katika kitabu chake cha "Sifa za Hospitali" kwamba: Si kila mtu ana sifa za kuwa tabibu na daktari, na tabibu anapaswa kuwa na sifa makhsusi. Aliwapinga sana watu wenye elimu ndogo waliojiita madaktari na kupiga vita israfu katika utumiaji wa dawa. Alijiepusha sana kumpa dawa mgonjwa kadiri inavyowezekana. Pale ilipolazimu kutoa dawa kwa mgonjwa, tabibu Razi alianza kumpa dawa ya kawaida, na kama haikumfaa mgonjwa alimwandikia na kumpa dawa mchanganyiko. Msomi Razi alikuwa akiamini kwamba: "Tabibu anayeweza kutibu mgonjwa wake kwa kutumia chakula huwa amepata saada na ufanisi".

Muhammad Zakaria Razi alikuwa daktari mvumbuzi na kamwe hakufuata kibubusa matabibu wenzake. Daima alikuwa akitafuta mbinu mpya kwa ajili ya kufaidika zaidi na elimu ya tiba. Katika hospitali yake, tabibu Razi alikuwa amezungukwa na wanafunzi wa wanafunzi wake na wanafunzi wake mwenyewe. Kila mgonjwa aliyekwenda hospitalini hapo kupata matibabu kwanza alipelekwa kwa wanafunzi wa wanafunzi wake. Pale wanafunzi wa wanafunzi wake waliposhindwa kumtibu au kuainisha matatizo yake, mgonjwa alipelekwa kwa wanafunzi wake asili na wakuu. Wanafunzi wakuu wa Razi walimshughulikia mgonjwa na pale waliposhindwa kujua ugonjwa wake, mgonjwa alipelekwa kwa mwalimu, yaani Zakaria Razi. Utaratibu huu ni miongoni mwa kumbukumbu zilizobakishwa na tabibu Razi na zingali zinatumika hadi hii leo katika hospitali nyingi za mafunzo duniani.  

Katika kipindi chake, suala la upasuaji wa mwili wa mwanadamu halikuwa maarufu na kimsingi suala hilo lilitambuliwa kuwa ni kinyume na maadili na mafundisho ya dini. Hata hivyo katika vitabu vyake kama kile cha Liber Almansoris, Zakaria Razi alibainisha na kuweka wazi suala la upasuaji wa mifupa, mishipa, ubongo, jicho, sikio, mapafu, moyo, utumbo na kadhalika na kueleza picha ya uti wa mgongo, matundu yake, uboho na kadhalika. Razi alikuwa tabibu wa kwanza aliyetambua baadhi ya mishipa katika kichwa na shingo ya mwanadamu na kutoa maelezo na ufafanuzi kuhusu viungo hivyo.

Tabibu Razi pia alikuwa miongoni mwa watu wachache sana ambao katika zama hizo walisisitiza umuhimu na nafasi ya elimu ya lishe na chakula na mchango wake katika afya ya mwanadamu. Katika uwanja huo Razi ameandika kitabu alichokipa jina la "Manufaa ya Vyakula na Madhara Yake" ambacho kimekusanya mambo yote ya tiba ya afya ya chakula. Kitabu hicho kina faslu na milango kadhaa. Ndani yake, tabibu Razi ameeleza sifa za vyakula mbalimbali, sababu za kuwa na hamu ya chakula na kinyume chake, mmengenyo wa chakula, mazoezi ya viungo, na kadhalika. 

Razi alikuwa mtu wa kwanza aliyeanza mchakato wa kubadili Alkemi (Alchemy) kwa maana ya kemia ya karne za kati iliyokusudia kugeuza metali ya kawaida kuwa dhahabu, na kuifanya elimu ya kemia. Kutokana na mbinu zilizotumiwa na msomi huyo Mwislamu wa Iran, tunaweza kusema kuwa, Razi alikuwa miongoni mwa waasisi wa elimu ya kemia. 

Mkemia wa Kijerumani Dakta Julius Ruska ambaye amefanya uhakiki kuhusu vitabu na maandiko ya msomi huyo wa Kiislamu ameandika kuwa: Kwa mara ya kwanza kabisa, Razi alianzisha mfumo mpya katika elimu ya kemia ambao tunaweza kuupa jina la mfumo wa elimu ya vitendo na nadharia ya kemia. Miongoni mwa matunda muhimu ya tabibu Razi ni ugunduzi wa asidi sulfuriki na alikoli.

Razi alitabahari sana katika elimu nyingi za sayansi asilia (bayolojia, kemia na fizikia), na vilevile katika metafizikia, yaani falsafa ya kuchunguza chanzo cha uhai na maarifa, na ameandika vitabu vingi katika elimu hizo. Faharasa ya kwanza kabisa ya vitabu vya Zakaria Razi iliandikwa na yeye mwenyewe na inapatikana katika kitabu cha al Fihrist kilichoandikwa na mtaalamu maarufu wa vitabu katika karne ya nne Hijria, Ibn Nadeem.

Faharasa hiyo inaonesha kuwa, Razi aliandika vitabu 184 katika maudhui mbalimbali kama tiba, mantiki, hisabati, falaki, falsafa na sayansi asilia.

Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Razi ni Kitab al-Hawi fi al-Tibb (Liber Continens) ambacho kinahesabiwa kuwa tabu kubwa (encyclopedia) la maarifa ya tiba. Ndani ya kitabu hicho pia kuna nadharia za madaktari na matabibu wa kabla ya Zakaria Razi. Kitabu hicho kilitarjumiwa kwa lugha ya  kilatini mwaka 1297 Miladia. Kitabu kingine cha msomi huyo Mwislamu ni Tiba ya Mansuri (Liber Almansoris). Kitabu hiki ndicho cha pili kwa umuhimu sana kati ya vitabu vya msomi huyo baada ya kile cha al Hawi. Katika kitabu hiki, Razi ameeleza elimu msingi ya masuala ya udaktari katika makala kumi. Makala ya tisa ya kitabu hicho ina kichwa cha maneno: Tiba ya maradhi yote kuanzia utosini hadi kidole gumba. Makala hii imechapishwa Ulaya katika kitabu kinachojitegemea na hadi mwishoni mwa karne ya 15 kilikuwa sehemu ya ratiba ya masomo ya tiba barani Ulaya. 

Muhammad bin Zakaria Razi alipitisha kipindi cha mwishoni mwa umri wake katika mji wa Rei ambako alifundisha na kulea wanafunzi wengi waliotokea kuwa mabingwa katika elimu ya udaktari. Kipindi hicho macho ya Razi yaliingiwa na mtoto wa jicho na mmoja wa wanafunzi wake kutoka Tabaristan alikwenda Rei kwa ajili ya kumtibu mwalimu wake. Razi alimwambia mwanafunzi kwamba, kazi hiyo itamzidishia mashaka na maumivu na kwamba anahisi kifo chake kilikuwa kimekaribia; hivyo hakuna haja ya kujitia mashakani kwa ajili ya kurejesha uwezo wake wa kuona.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa na mwaka 312 Hijria Muhammad bin Zakaria Razi aliaga dunia katika mji alikozaliwa wa Rei nchini Iran.