Oct 15, 2018 11:30 UTC

Katika siku za mwanzoni mwa mwezi Muharram Waislamu hususan wafuasi na wapenzi wa Watu wa Nyumba tukufu ya Mtume wetu Muhammad (saw) katika maeneo mbalimbali ya dunia huwa katika siku za majonzi na huzuni ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa mtukufu huyo, Imam Hussein bin Ali (as) ndugu, watoto na masahaba zake huko Karbala.

Shughuli hiyo inayofuatana na majonzi, maombolezo na alama za huzuni huandamana na Waislamu kulia kutokana na kukumbuka masaibu na mashaka makubwa yasiyo na kifani yaliyomsibu Hussein na watu wa familia ya Mtume katika siku hiyo.  

Wako baadhi ya watu ambao ama kutokana na uadui wao au ujinga na kutojua vyema mafundisho ya Kiislamu wamekuwa wakihoji ni kwa nini Waislamu wa madhehebu ya Shia na wafuasi wa Ahlubaiti wa Mtume (saw) huomboleza na kumlilia Bwana wa Vijana wa Peponi? Kundi hilo linadai kwamba, kitendo hicho kinapingana na mafundisho ya Uislamu.

Marejeo bora zaidi na ya kuaminika ya dini ya Uislamu ni kitabu cha Mwenyezi Mungu SW, Qur'ani tukufu. Mwenyezi Mungu Jalla Jalaluhu anasema katika aya ya 32 ya Suratul Hajj kwamba:

Ndivyo hivyo, na anayezitukuza nembo za Mwenyezi Mungu basi hiyo ni katika alama za taqwa na uchamungu wa nyoyo. Wafasiri wa Qur'ani tukufu wanasema kuwa, maana ya nembo za Mwenyezi Mungu katika aya hii si vitu kama Swafa na Marwa pekee vilivyokuwa vikizungumziwa kabla ya aya hiyo, bali ni kila kitu kinachomkumbusha na kumuelekeza mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu Muumba. Mfasiri mkubwa wa Qur'ani wa zama hizi, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai anasema "sha'air" au nembo zinazotajwa katika aya hiyo zina maana ya alama na nembo za adhama ya Mwenyezi Mungu Muumba na ni alama ya taqwa na uchamungu. Hapana shaka kuwa, kuwakumbuka na kuwaenzi mawalii wa Mwenyezi Mungu waliosabilia na kutoa roho zao katika njia yake na kwa ajili ya kubakisha hai dini yake ni miongoni mwa alama na nembo kubwa za taqwa na uchamungu. Katika shughuli kama hizo za kuwakumbuka mawalii wa Mwenyezi Mungu waliosabilia kila kitu kwa ajili yake na dini yake, Waislamu hujifunza jinsi ya kusimama imara kwa ajili ya dini ya Allah, kusabilia roho na kila ghali kwa ajili yake SW, jinsi ya kupambana na dhulma na madhalimu, kujifunza sira na maisha ya watukufu hao, kupata ibra, kuwajua maadui wa Mwenyezi Mungu na mawalii wake na kadhalika. Aya ya 148 ya Suratu Nisaa inasema: Hapendi Mwenyezi Mungu maneno ya kutangaza uovu ila kwa yule aliyedhulumiwa.

Kwa msingi huo Mwenyezi Mungu amewaruhusu waliodhulumiwa kukusema na kufichua dhulma na uovu unaofanywa na madhalimu. Hapa linajitokeza swali kwamba, ni dhulma na uovu upi mkubwa zaidi kuliko ule wa kuuliwa na kukatwa vichwa watu wa familia ya Mtume wetu Muhammad (saw)? Hivyo basi, inampasa Muislamu wa kweli kupaza sauti yake dhidi ya dhulma na uovu uliofanyika siku ya tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria na kufichua uovu wa madhalimu na wote waliohusika katika mauaji ya kizazi cha Mtume wetu (saw). Kwa kuzingatia ukweli huu Imam Ruhullah Khomeini anasema: Kumlilia aliyedhulumiwa ni kupaza sauti dhidi ya dhulma na madhalimu.   

Katika aya za Qur'ani tukufu pia Mwenyezi Mungu SW amezungumzia suala hili la kulia katika misiba na masaibu yanayowapata watu tunaowapenda na kuwaenzi. Miongoni mwa aya hizo ni zile zinazozungumzia kulia sana kwa Nabii Yaaqub (as) akimlilia mwanaye kipenzi, Yusuf (as). Mwenyezi Mungu SW amelitaja tukio hilo katika aya za Suratu Yusuf na wala hakukemea kitendo hicho cha Nabii wake mwema. Kwa msingi huo kuwalilia mawalii wa Mwenyezi Mungu si tu kwamba si jambo baya bali ni suala linalopendeza na kuhamasishwa baada ya kufanywa na watu adhimu wakiwemo Mitume wa Mwenyezi Mungu na kutajwa kwenye Qur'ani bila ya kukosolewa.

Katika sira na suna za Mtume wetu Muhammad (saw) kunashuhudiwa sana kwamba, mtukufu huyo pia alikuwa akiwalilia vipenzi vyake na kuumizwa na misiba na masaibu yao. Mtume (saw) pia alikuwa akilia kutokana na mauaji ya masahaba wake. Imepokewa katika vitabu vya hadithi na historia kwamba, Mtume (saw) alihuzunishwa sana na kifo cha mwanaye Ibrahim na akalia sana kiasi cha kuwastaajabisha baadhi ya watu. Mtume alisema: Jicho linalia na moyo unahuzunika lakini hatusemi lolote isipokuwa linalomridhisha Mwenyezi Mungu. Ewe Ibrahim! Tunahuzunika kutokana na kutengana na wewe.

Vilevile imepokewa kwamba, wakati Hamza bin Abdul Muttalib, ami yake Mtume (saw) alipouliwa shahidi katika vita vya Uhud, Mtume aliwaamuru wanawake wa Madina wafanye vikao vya maombolezo na wamlilie Hamza. Habari hii utaipata katika vitabu mashuhuri vya wanazuoni wa Ahlusunna kama Ibn Jariri Tabari katika Tarikh Tabari na kadhalika. Vilevile historia imesajili na kuandika jinsi Bibi Fatimatu Zahraa (as) alivyomlilia baba yake kipenzi, Mtume wa Mwenyezi Mungu baada ya kuaga dunia.  

Imepokewa pia kwamba Mtume Muhammad (saw) aliwapasha baadhi ya maswahaba zake habari ya msiba na masaibu yatakayompata mjukuu wake Hussein katika ardhi inayoitwa Karbala. Hadithi zinasema Malaika Jibrilu alimpasha Mtume habari ya kuuliwa mjukuu wake baada ya Hussein kuzaliwa. Imepokewa kwamba, mke mwema wa Mtume Muhammad (swa), Ummu Salamah radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema kwamba, Malaika Jibrail alimpasha Mtume (saw) habari ya jinsi Hussein atakavyouawa shahidi na akamkabidhi Mtume udongo wa ardhi ya Karbala. Mtume (saw) alilia sana baada ya kupewa habari hiyo na alinipa mimi udongo huo kama amana na kuniambia: Wakati wowote utakapoona udongu huu umekuwa na rangi ya damu jua kwamba mwanangu Hussein ameuawa shahidi. Hadithi hii imepokewa katika vitabu vya historia na hadithi vya wanazuoni wakubwa na mashuhuri wa Kiislamu kama al Kamilu fii Tarikh, al Muujamul Kabiir, Kanzul Ummal, Fadhailu Sahaba, al Tabaqaatul Kubra, Tarikhu Dimishq na kadhalika.

Vilevile wanahistoria wamemnukuu Ibn Abbas akisimulia kwamba, Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib alipofika eneo la Karbala wakati wa kuelekea katika vita vya Siffin alisimama na kulia sana hadi ndevu zake zikaloa kwa machozi. Baada ya hapo alitueleza jinsi watoto wake watakavyouawa shahidi kidhulma na watu waovu katika eneo hilo.

Bibi Aisha mke wa Mtume (saw) pia amenukuu kwamba: Mtume amesema: Jibrilu ameniambia kwamba mwanangu Hussein atauawa baada yangu mimi katika ardhi inayoitwa Twaff na ameniletea udongo huu na kunipasha kwamba, kaburi lake litakuwa huko. Hadithi hii imepokewa katika vitabu vya wanazuoni wa Ahlusunna kama al Muujamul Kabiir, Kanzul Ummal na kadhalika.

Maimamu katika kizazi cha Mtume (saw) ambao ni moja na vizito viwili tulivyoachiwa na mtukufu huyo kwa mujibu wa hadithi maarufu ya Thaqalain, walikuwa wakilia na kuomboleza mauaji ya mjukuu wa Mtume (saw), Hussein (as). Hapana shaka kuwa, sira na mwenendo wa watukufu hawa pia ni kigezo na ruwaza njema kwa Waislamu wote isipokuwa wale wanaofuata nyayo za Bani Umayyah waliowaua watoto na wajuu wa Mtume wetu. Vitabu vya sira na historia vinasema Imam Ali bin Hussein Sajjad (as) ambaye wanazuoni wote wa Kiislamu bila ya kujali madhehebu yao wanasema alikuwa pambo la wachamungu, alimlilia sana baba yake na alipoulizwa sababu yake alisema: Nabii Yaaqub alimpoteza Yusuf kwa kipindi fulani tu lakini alilia sana hadi akapofuka macho. Ama mimi nimeshuhudia kuuliwa kwa watu 14 wa familia yangu katika masaa kadhaa tu ya siku na mnatarajia kwamba nisiumizwe na masaibu yaliyowapata?

Kulia na kuwakumbuka vipenzi vyetu ni jambo la kimaumbile linaloakisi hisia za kibinadamu na ni muhali kwamba dini ya Uislamu inayooana na maumbile safi ya mwanadamu itakataza na kupinga suala hilo la kimaumbile. Hii leo sayansi inathibitisha kwamba, wanyama wanawalilia wanyama wenzao na kuhuzunika kutokana na yanayowapata. Iweje basi Waislamu wa kweli na vipenzi vya Mtume (saw) wasimlilie Mtume, Ahlibaiti zake na masahaba na vipenzi vyake? Hususan pale watukufu hao wanapokuwa wameuawa kwa njia za kikatili na zisizo na kifani katika historia ya mwanadamu kama yalivyo mauaji ya Hussein bin Ali bin Abi Twalib, watoto, ndugu na masahaba zake katika ardhi ya Karbala? Hakika hakatazi wala kushangazwa na suala hilo sipokuwa mtu asiye na hisia za kibinadamu, katili na asiye na chembe ya huruma.

Kumlilia Hussein (as) na masahaba zake wema na mashujaa waliosabilia roho zao kwa ajili ya kunusuru dini ya Uislamu na familia ya Mtume (saw) ni kudhihirisha mapenzi yetu kwa Uislamu, Mtume na matukufu ambayo Hussein na masabaha zake waliuliwa shahidi wakiyatetea na kuyalinda.  

Tags