Jul 06, 2025 02:24 UTC
  • Jumapili, 6 Julai, 2025

Leo ni Jumapili 10 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria mwafaka na 6 Julai 2025 Miladia.

Katika siku kama hii ya leo miaka 1386 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Uislamu na mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na majeshi ya batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la A'shuraa. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah SW. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya. Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya. Baada ya kupambana kishujaa, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi katika siku kama ya leo akiwa pamoja na watu wengine wa familia ya Mtume (saw), na wafuasi wake waaminifu.

Karbala katika kumbukumbu ya Ashura

 

 Katika siku kama ya leo miaka 171 iliyopita, alifariki dunia George Simon Ohm mwanahisabati na mwanafizikia wa Ujerumani akiwa na umri wa miaka 67. Simon Ohm alizaliwa mwaka 1789 na kuanza kupenda sana somo la fizikia na kufanikiwa kuvumbua kanuni katika uwanja wa umeme kutokana na utafiti mkubwa aliokuwa akiufanya katika uwanja huo. Alizipa kanuni hizo jina lake yaani "Ohm Laws". Kanuni ambazo zinatumiwa hadi leo hii. ***

 

George Simon Ohm

 

Miaka 63 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. William alizaliwa mwaka 1897. Baada ya kushiriki katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Faulkner alirejea tena nchini kwake. Alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake, Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili Wamarekani wenye asili ya Afrika. Hadithi za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa leo nchini Marekani. ***

William Faulkner

 

Tarehe 6 Julai miaka 61 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Malawi ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kabla ya Malawi kupata uhuru, ilikuwa ikijulikana kwa jina la Nyasaland. Mwaka 1859, makundi ya Wamishonari kutoka Scotland wakiwa pamoja na mvumbuzi David Livingstone waliwasili Nyasaland na kufuatiwa na Uingereza. Uingereza iliunga mkono uvamizi wa Ujerumani na Ureno huko Nyasaland na hatimaye mwaka 1891 nchi hiyo ikawekwa chini ya mamlaka yake. Kwa utaratibu huo Nyasaland ambayo ni Malawi ya leo ikawa miongoni mwa makoloni ya Uingereza katika eneo la Mashariki mwa Afrika. Kijiografia Malawi iko kusini mashariki mwa Afrika ikipakana na nchi za Tanzania, Zambia na Msumbiji. ***

 

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, visiwa vya Comoro vilipata uhuru. Raia wengi wa visiwa vya Comoro walianza kuingia katika dini ya Kiislamu na kueneza utamaduni wa dini hiyo visiwani humo, baada ya wafanya biashara wa Kiislamu kuwasili visiwani humo katika karne ya 12 Miladia. Tangu karne ya 16 visiwa vya Comoro vilikuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno na baadaye Sultan wa Oman alifanikiwa kuhitimisha ukaliwaji mabavu wa visiwa hivyo. Hata hivyo mwaka 1842 sehemu kadhaa za visiwa hivyo ziliingia chini ya udhibiti wa Wafaransa na taratibu wakoloni hao wakaidhibiti ardhi yote ya nchi yote hiyo. Mapambano ya wananchi yalipelekea kutangazwa uhuru rasmi wa nchi ya Kiislamu ya Comoro mwaka 1975. Comoro ina ukubwa wa kilomita mraba 1862 na kijiografia inapatikana kusini mashariki mwa bara la Afrika katika bahari ya Hindi. ***