Jun 04, 2025 02:24 UTC
  • Jumatano, tarehe 04 Juni, 2025

Leo ni Jumatano tarehe 08 Dhulhija 1446 Hijria sawa na tarehe 04 Juni 2025.

Leo tarehe 8 Dhul-Hija ni siku ya Tarwiya.

Siku hii imepewa jina la siku ya Tarwiya kwa maana ya kujitosheleza kwa maji kwa sababu katika zama za Nabii Ibrahim (as) maji hayakuwa yakipatikana katika jangwa na Arafa na kwa msingi huo watu walikuwa wakipeleka maji eneo la Arafa kutoka Makka tarehe 8 Dhul-Hija wakijitayarisha kwa ajili ya mahitaji ya maji ya kesho yake yaani tarehe tisa Dhulhija. 

Katika siku kama ya leo miaka 1386 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Imam Hussein bin Ali (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad SAW aliondoka Makka na kuelekea Kufa nchini Iraq baada ya kukataa kumbai na kutoa kiapo cha utiifu kwa Yazid bin Muawiya.

Miezi minne kabla ya hapo, Imam Hussein alikuwa amewasili mjini Makka akiwa pamoja na familia yake na alikitumia kipindi cha kuweko waumini waliotoka pembe mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufanya ziara katika Nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu, kuwaamsha na kuwabainishia dhulma na ufisadi mkubwa uliokuwa ukifanywa wa utawala wa Yazid mwana wa Muawiya.

Wakati huo huo kutokana na wito wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na njama za utawala wa Yazidi za kutaka kumuuwa, Imam Hussein aliondoka Makka na kueleka Kufa. 

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, tarehe 14 Khordad mwaka 1368 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia sawa na mwezi Juni 1989, Imam Ruhullah Musawi Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87. Ulimwengu wa Kiislamu uligubikwa na majonzi na huzuni kubwa kuutokana na kutangazwa kifo cha Imam.

Imam Khomeini (M.A) alizaliwa tarehe Mosi mwezi wa Mehr mwaka 1281 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 24 Septemba 1902 katika mji wa Khomein ulioko katikati mwa Iran. Alianza kujishughulisha na siasa sambamba na masuala ya kielimu na kiutamaduni. Mapambano ya Imam dhidi ya utawala wa Shah na uingiliaji wa Marekani nchini Iran yalishtadi mwaka 1963 Milaadia sawa na 1342 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, na kupelekea Imam kubaidishwa kwa miaka 13 nchini Iraq, Uturuki na Ufaransa. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi mwaka 1357 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 1979 kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini (M.A).

Imam alibobea katika taaluma mbalimbali, na mbali na kuwasomesha wanafunzi wengi na kutoa hotuba nyingi za kihistoria, alikuwa pia mwandishi hodari wa vitabu. Miongoni mwa vitabu vyake ni Tahrirul Wasilah, Kashful Asrar, Misbahul Hidayah, na Utawala wa Kiislamu na Uongozi wa Faqih.  

Mwili wa Imam ukisindikizwa na wananchi

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Khordad mwaka 1368 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu lilimchagua Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuwa Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Uchaguzi huo ulifanyika masaa machache tu baada ya kufariki dunia Imam Khomeini (M.A) ambapo wasia wa Imam ulisomwa mbele ya hadhirina.

Hadi sasa Ayatullah Khamenei anaendeleza njia ya Imam Khomeini MA kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu na ameyaongoza Mapinduzi ya Kiislamu kwa hekima, tadbiri, uono wa mbali na ustahiki.

Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran inatoa salamu za rambirambi kwa mnasaba huu wa kukumbuka siku ya kuaga dunia hayati Imam Khomeini.   

Tarehe 4 Juni mwaka 1989 yaani siku kama hii ya leo miaka 36 iliyopita, wanafunzi kadhaa wa vyuo vikuu vya China waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa na polisi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beijing.

Siku hiyo maelefu ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya China walikuwa wamekusanyika katika Medani ya Tiananmen mjini Beijing, wenye maana ya 'Amani ya Mbinguni' wakitaka kuwepo mazingira ya wazi ya kisiasa nchini humo, kupunguzwa uwezo wa chama cha kisoshalisti, kuongezwa uwezo wa Bunge na kuchaguliwa wawakilishi wake.

Ingawa serikali ya China ilipiga marufuku maandamano hayo lakini wanafunzi waliendelea kukusanyika na mwishowe askari polisi na vikosi vya jeshi vikatumia silaha kuwakandamiza wanafunzi hao.  

Medani ya Tiananmen

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Watoto Wasio na Hatia Waathirika wa Unyanyasaji (International Day of Innocent Children Victims of Aggression).

Siku hiyo ilitangazwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1982 kwa ajili ya kushughulikia mashaka ya watoto wanaosumbuliwa na unyanyasaji wa kimwili, kiakili na kiroho kufuatia hali mbaya ya watoto wa Palestina na Lebanon wanaosumbuliwa na ukatili wa utawala haramu wa Israel.

Ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto una sura na aina mbalimbali na unasababishwa na uzembe wa wazazi, viongozi wa kitaifa na kimataifa na makatili wasio na chembe ya huruma na wasiojali isipokuwa maslahi yao ya kimaada.    ****