Bibi Fatimatu al Zahra (as) katika Ayatu Tat'hir
https://parstoday.ir/sw/radio/uncategorised-i58529-bibi_fatimatu_al_zahra_(as)_katika_ayatu_tat'hir
إِنَّما یُرِیدُ اللَّهُ لِیُذْهِبَ عَنْکُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَیْتِ وَ یُطَهِّرَکُمْ تَطْهِیراً
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 15, 2020 11:19 UTC
  • Bibi Fatimatu al Zahra (as) katika Ayatu Tat'hir

إِنَّما یُرِیدُ اللَّهُ لِیُذْهِبَ عَنْکُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَیْتِ وَ یُطَهِّرَکُمْ تَطْهِیراً

Tarehe13 Jamadi Awwal kwa mujibu wa mapokezi ya baadhi ya wanahistoria ndiyo siku aliyokufa shahidi binti kipenzi wa Mtume Muhammad (saw) Fatimatu Zahra (as). Wanahistoria wengine wanasema bibi huyo mwema alikufa shahidi tarehe 3 Jamadithani yaani siku 95 tu baada ya kufariki dunia baba yake mtukufu, Mtume Muhammad (saw). Kwa msingi huo siku za baina ya tarehe hizo mbili zimepewa jina la Siku za Fatimiyyat ambapo Waislamu wafuasi wa Ahlubaiti wa Mtume (saw) huzitumia kukumbuka na kutaja mema na matukufu ya Bibi Fatima (as).

Bibi Fatimatu Zahra kwa mujibu wa aya ya 33 ya Suratul Ahzab ambayo ni maarufu baina ya wataalamu wa tafsiri ya Qur'ani kwa jina la Ayatu Tat'hir kwa maana ya Aya ya Kutakaswa, amesafishwa na kutakaswa na kila aina ya uchavu na madhambi, kwa maana kwamba alikuwa maasumu. Imepokewa kutoka kwa mke mwema wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ummu Salamah, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake kwamba amesema: Siku  moja Fatima alipika chakula na kukileta kwa Mtume (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake) akiwa nyumbani kwangu. Wakati alipompa chakula hicho, Mtume alimwambia: Ewe Fatima! Nuru ya jicho langu! Mwite Ali na wanao wawili (Hassan na Hussein) ili wapate kula chakula hiki pamoja nami. Walikuja na wote wakala chakula hicho pamoja na Mtume. Baadaye mtukufu huyo alishika shuka na kuwafunika kisha akasoma aya ya 33 ya Suratul Ahzab inayosema: "Hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwaondolea uchafu enyi Watu wa Nyumba ya Mtume na kuwatakaseni barabara." 

Hadithi zinasema: Baada ya kuteremshwa Aya hii, Mtume (saw) alikuwa akipita nyumbani kwa Bibi Fatima na Ali nyakati za alfajiri na kusimama mlangoni kisha anasema: Enyi watu wa Nyumba ya Mtume! Swala, salamu na rehma za Allah ziwe juu yenu. Amkeni kwa ajili ya Swala. Hakika nitapigana vita na atakayekupigeni vita, na nitakuwa amani kwa atakekuwa na amani na nyinyi. Hadithi zinasema Mtume alifanya hivi kwa kipindi cha miezi kadhaa.   

Bibi Fatima al Zahra (as) ni binti wa Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na Bibi Khadija binti Khuwailid, mke kipenzi wa Mtume. Baadhi ya lakabu zake ni al Zahra, Siddiqa, Twahira, Mubarakah, Zakiyyah, Raadhiyah, Mardhiyya, Muhaddathah na Batul. Wanahistoria wengi wa Kishia na Kisuni wanasema kuwa, alizaliwa tarehe 20 Jamadithani mwaka wa 5 baada ya Mtume kubaathiwa na kupewa utume mjini Makka. Wanahistoria wengine wanasema, alizaliwa mwaka wa tatu baada ya biitha huku wengine wakisema alizaliwa mwaka wa pili. Bibi Fatima al Zahra alizaliwa na kukulia katika nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ambako Malaika wa wahyi na ufunuo walikuwa wakiingia na kutoka wakileta ujumbe wa Mola Mlezi. Baada ya kuolewa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) alitambulika kuwa mwanamke kigezo bora cha kuigwa na watu wote katika maisha ya ndoa, ibada na mwenendo mzuri. Baada ya kazi za nyumbani, Bibi Fatima alikuwa akijipinda kwa ibada, dua na kumtaradhia Mola Karima. Tokea awali Bibi Fatima alijifunza elimu na maarifa katika nyumba na ufunuo na wahyi. Elimu na mambo yote ya siri aliyokuwa akifunzwa na baba yake yalikuwa yakiandikwa na mume wake, Ali bin Abi Twalib (as). Bibi Fatima alikusanya elimu na maarifa hayo aliyoambiwa na baba yake na kuandikwa na Imam Ali katika tabu kubwa lililokuwa maarufu kwa jina la 'Mas'hafu Fatima'. Bibi huyu mtakatifu alifanya jitihada kubwa za kuwafunza wanawake wa Kiislamu maarifa ya dini hiyo. Alishika Qur'ani tukufu na kuanisika na kitabu hicho. Bibi Fatima al Zahra (as) alikuwa akipitisha sehemu ya usiku kwa ibada na kumtaradhia Mola Muumba. Swala zake za usiku zilikuwa ndefu kiasi kwamba, miguu ya mtukufu huyo ilikuwa ikivimba kwa kusimama sana katika ibada hiyo. Hassan al Basri aliyefariki dunia mwaka 110 Hijria anasema: "Hakuna mtu katika umma aliyekuwa akifanya ibada kwa wingi, kuipa mgongo dunia na kumcha Mungu zaidi ya Fatima binti Muhammad (as)."

Katika kipindi cha miaka 10 ya serikali ya Bwana Mtume (saw) mjini Madina, kulitokea vita 27 hadi 28 vilivyoongozwa na Mtume mwenyewe na mapigano 35 hadi 90 ambayo Mtume alituma jeshi la Kiislamu kukomboa au kukabiliana na hujuma za maadui katika maeneo mbalimbali. Baadhi ya mapigano hayo yalichukua muda wa miezi miwili hadi mitatu kutokana na kuwa mbali na mji wa Madina, makao makuu ya serikali ya Kiislamu. Katika kipindi kikubwa cha maisha yake ya ndoa na Bibi Fatima (as), Imam Ali bin Abi Twalib (as) alitumia wakati wake mwingi akiwa katika medani za vita na Jihadi ya kulinda mipaka ya utawala mchanga wa Kiislamu. Wakati huo mke wake mwaminifu alichukua majukumu yote ya kuendesha masuala ya nyumba na kulea watoto. Si hayo tu, bali Bibi Fatima al Zahra alifanya hima kubwa katika kusaidia pia familia za wapiganaji wengine wa Kiislamu au familia za mashahidi waliouawa katika vita vya Jihadi na kupigania dini ya Uislamu. Alikuwa pia akiwahamasisha wanawake wa Kiislamu kutibu majeruhi wa vita vya Jihadi wa familia na ndugu zao.

Imepokelewa kwamba, katika vita vya Uhud, Bibi Fatima akiwa pamoja na wanawake wengine, walielekea katika eneo hilo la vita lililoko umbali wa kilomita sita kutoka Madina. Katika vita hivyo Mtume Mtukufu alijeruhiwa vibaya huku Imam Ali bin Abi Twalib aliyekuwa akimhami Mtume wa Mwenyezi Mungu akipata pia majeraha. Bibi Fatima alifanya kazi ya kufuta damu katika kipaji kitukufu cha uso wa Mtume huku Imam Ali bin Abi Twalib akimimina maji kwa kutumia ngao yake ya vita. Baada ya kuona kwamba damu ilikuwa haikatiki na kusimama katika kipaji cha Bwana Mtume, Bibi Fatima alichoma kipande kidogo cha mkeka na akaweka majivu yake kwenye jeraha la Mtume ili kuzuia kuvuja damu kwa wingi.

Wakati wa vita vya Khandaq, Bibi Fatima (as) alimpelekea Mtume (saw) mkate. Mtume aliuliza: "Hiki ni kitu gani?" Bibi Fatima alisema: "Nimepika mkate, lakini moyo wangu haukutulia bila ya kukuletea wewe mkate huu." Mtume alimwambia: "Hiki ndicho chakula cha kwanza kinachoingia mdomoni mwangu tangu siku tatu zilizopita." Bibi Fatima al Zahra (as) alikuwepo pia katika medani ya Fat'hu Makka, yaani wakati wa kukombolewa mji mtakatifu wa Makka.

Bibi Fatima aliendelea kuhudumia Uislamu na Waislamu kwa njia mbalimbali katika kipindi cha uhai wa Mtume Muhammad (saw) na hata katika kipindi kifupi alichoishi baada ya kufariki dunia baba yake kipenzi. Alikuwa na Mtume Muhammad katika hali zote za mashaka, masaibu na hujuma za washirikina na hakusita kujitolea kwa ajili ya kumlinda Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Uimamu baada yake hususan Imam Ali bin Abi Twalib. Aliendelea hivyo hadi katika kipindi cha mwishoni mwa uhai wa Mtukufu Mtume.

Maradhi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu yalishadidi zaidi katika siku za mwishoni mwa umri wake uliojaa baraka. Bibi Fatima (as) alikuwa daima akiketi kando ya kitanda cha baba yake Mtume Mtukufu huku akiangalia sura yake iliyokuwa imejaa nuru ikitokwa na jasho kwa wingi kutokana na homa kali. Bibi Fatima alisikitishwa mno na hali hiyo na daima alikuwa katika hali ya kulia. Mtume Mtukufu pia alishindwa kustahamili kilio na mazonge ya binti yake kipenzi. Alimnong'oneza sikioni na ghafla Bibi Fatima alitulia na kutabasamu. Tabasamu hilo la Bibi Zahra hususan katika kipindi hicho cha kusikitisha liliwashangaza hadhirina. Walimuuliza: "Mtume wa Mwenyezi Mungu amekuambia siri gani?" Alijibu: "Sitatoa siri ya baba yangu maadamu yu hai. Siri hiyo ilifichuliwa baada ya Mtume Mtukufu (saw) kuaga dunia. Bibi Fatima al Zahra (as) alisema: "Mtume aliniambia: "Utakuwa wa kwanza kati ya Ahli Baiti zangu atakayejiunga nami, na nilifurahi kwa sababu hiyo."

Baada ya kuaga dunia baba yake yaani Mtume Muhammad (saw), Bibi Fatima (as) na Ahlubaiti wa Mtume kwa ujumla walipatwa na masaibu makubwa mno. Hatimaye Bibi huyo mwema ambaye kwa mujibu wa hadithi sahihi ya Mtume Muhammad (saw) ni 'Mbora wa wanawake duniani' alikufa shahidi tarehe 13 Jamadil Awwal mwaka 11 Hijria kwa mujibu wa mapokezi ya baadhi ya wanahistoria au tarehe 3 Jamadithani. Aliswaliwa kwa siri na kundi dogo la maumini na kuzikwa usiku wa manane kwa mujibu wasia wake ambapo alitaka watu waliomdhulumu wasishuhudie jeneza na mazishi yake. Sala za salamu za Mwenyezi Mungu, Malaika, na Mitume wake zimshukie Bibi Fatima al Zahra.