Jan 16, 2026 02:15 UTC
  • Leo katika historia
    Leo katika historia

Leo ni Ijumaa tarehe 26 Rajab 1447 Hijria sawa na tarehe 16 Januari 2027.

Siku kama ya leo miaka 1450 iliyopita, Abu Twalib ami ya Mtume Muhammad (SAW) na baba wa Imam Ali (A.S) alifariki dunia wakati Waislamu walipokuwa chini ya mzingiro wa washirikina wa Makka.

Abu Twalib alikuwa pamoja na Waislamu wengine na watu wa ukoo wa Bani Hashim katika Shiibi Abi Twalib. Mtume Muhammad (SAW) alikuwa chini ya uangalizi wa Abu Twalib tangu alipokuwa na umri wa miaka minane, baada ya kuaga dunia babu yake, Abdul Muttalib. Abu Twalib alisilimu baada ya kubaathiwa Mtume na alikuwa muungaji mkono na mtetezi mkubwa wa Mtume Mtukufu dhidi ya washirikina wa Kiquraishi. 

Kabla ya kuaga dunia, Abu Twalib aliwausia jamaa na marafiki zake kufuata Uislamu na kumtetea Mtume Muhammad (saw).

Katika siku kama ya leo miaka 180 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Januari 1846, vilianza vita baina ya Marekani na Mexico baada ya Washington kuishambulia nchi hiyo.

Vita hivyo vilivyochukua muda wa miaka miwili, vilitokea baada ya Marekani kudai kwamba wahajiri wa nchi hiyo wanateswa nchini Mexico. Hata hivyo ukweli ni kuwa, Marekani ilianzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kuyatwaa baadhi ya maeneo ya Mexico hususan eneo la Texas.

Katika vita hivyo, Marekani iliyakalia kwa mabavu majimbo ya Texas, California, Nevada, Utah, Arizona na New Mexico. 

Tarehe 26 Dey 1357 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi, mfalme wa mwisho wa Iran alitoroka nchini kwa kisingizio cha kwenda kupata matibabu nje ya nchi, baada ya kushadidi wimbi la harakati za Mapinduzi.

Muhammad Reza Pahlavi alichukua kiti cha ufalme mwaka 1320 Hijria Shamsia baada ya serikali ya Uingereza kumpeleka uhamishoni baba yake, Reza Shah, kwa sababu aliiunga mkono Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Siku chache kabla ya tukio hilo, Imam Ruhullah Khomeini ambaye wakati huo alikuwa Ufaransa, alitoa ujumbe mzito akisema kuwa: "Safari ya Shah bila ya kung’oka madarakani haitabadilisha lolote na utawala wa kifalme nchini Iran unapaswa kuangushwa kikamilifu." 

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita yaani tarehe 16 Januari 2001, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alipigwa risasi na mmoja wa walinzi wake katika ikulu ya Rais na kujeruhiwa vibaya.

Baada ya tukio hilo kulienea habari za kutatanisha juu ya hatima ya kiongozi huyo. Tarehe 18 Januari yaani siku mbili baadaye, serikali ya Kinshasa ilithibitisha kufariki dunia Rais Laurent Desire Kabila. Kabila alizaliwa mwaka 1939 huko Katanga na kupata elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania.

Aliingia madarakani mwaka 1997 baada ya vikosi vya askari aliokuwa akiwaongoza kuuteka mji wa Kinshasa na kumlazimisha Mobutu Sese Seko, rais wa wakati huo wa Zaire ya zamani kukimbilia nje ya nchi. 

Laurent Desire Kabila