Jan 08, 2026 03:01 UTC
  • Alkhamisi, Januari 8, 2026

Leo ni Alkhamisi tarehe 18 Rajab 1447 Hijria sawa na 8 Januari 2026.

Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita alifariki dunia mtoto mdogo wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ibrahim, akiwa na umri wa miezi 18 tu. 

Ibrahim ambaye alifariki dunia kutokana na maradhi, alikuwa mtoto pekee wa kiume wa Mtume ambaye hakuzaliwa na Bibi Khadija (as). Mama yake alikuwa Maria al Qibtiyya ambaye alitumwa na mfalme wa Misri ya wakati huo kuwa hadimu na mtumishi wa Mtume na aliolewa na mtukufu huyo baada ya kusilimu. 

Kifo cha Ibrahim kilimhuzunisha sana Mtume (saw) kwa sababu mtukufu huyo alikuwa akimpenda sana mtoto huyo.   

Inafaa kukumbusha kwamba kwa mujibu wa riwaya mashuhuri, Mtume Muhammad (SAW) alikuwa na mabinti 4 na wavulana 2 kutoka kwa Hadhrat Khadija, ambao wote, isipokuwa Bibi Fatimatu Zahra (sa), walifariki dunia wakati wa uhai wa Mtume.****  

Tarehe 18 Rajab miaka 1021 iliyopita alifariki dunia Ibn Samh huko katika mji wa Andalucia. 

Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa mtaalamu wa hesabu, nyota na tabibu. Alizaliwa katika mji wa Cordoba, Andalucia mnamo mwaka 370 Hijiria. Msomi huyu wa Kiislamu alifanya utalii na utafiti mwingi katika elimu za hesabu na nyota, sambamba na kuwalea wanafunzi wa zama zake. 

Kuna vitabu kadhaa vilivyoandikwa na Ibn Samh kwa lugha ya Kiarabu na miongoni mwa vitabu hivyo ni "Al Madkhalu Ilal Handasah", "Al Muamalat" na "Kitabuz Ziyj."   

Miaka 384 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia, Galileo Galilei akiwa na umri wa miaka 78.

Alizaliwa katika mji wa Pisa na kusoma fasihi hadi alipofikisha umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu, Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua.

Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya Abu Raihan Biruni, msomi mashuhuri wa Iran, ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, Kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa ni kafiri na akahukumiwa. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake.   

Galileo Galilei

Katika siku kama ya leo miaka 105 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Tabatabai, mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu na maulamaa wapigania uhuru wa Iran.

Wakati wa mapinduzi ya kikatiba nchini Iran, Sayyid Muhammad Tabatabai alikuwa akihesabika kuwa mmoja kati ya viongozi wakubwa wa mapinduzi hayo. Tabatabai alishirikiana na Sayyid Abdullah Behbahani ambaye naye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya kikatiba dhidi ya utawala wa Qajari nchini Iran. 

Sayyid Muhammad Tabatabai

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, yaani tarehe 8 Januari mwaka 1932 ulianza utawala wa kifalme wa Abdul-Aziz Ibn Saud katika eneo la Bara Arabu kupitia msaada wa Uingereza.

Abdul-Aziz Ibn Saud, aliyekuwa mmoja wa viongozi wa makabila ya Hijaz, alianzisha mapigano dhidi ya utawala wa Othmania mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 na kupata ushindi. Mwaka 1903 mtawala wa Kiothmania alitimuliwa katika eneo la ya al-Ahsa huko Hijazi na tukio hilo lilikuwa jiwe la msingi wa kuasisiwa utawala wa Aal-Saud katika maeneo hayo. Katika kipindi cga Vita vya Kwanza vya Dunia, Aal-Saud waliingia ubia wa urafiki na Uingereza. Hatimaye mwishoni mwa vita hivyo vilivyomalizika kwa kushindwa vibaya utawala wa Othomania, utawala huo ulifikia tamati kikamilifu katika eneo hilo la Bara Arabu. Katika vita vilivyopiganwa baina ya Abdul-Aziz Ibn Saud na mtawala Hussein Bin Ali Sharif aliyekuwa mtawala wa mji wa Makkah, Ibn Saud aliibuka mshindi na akatwaa kwa nguvu eneo hilo la Hijaz.

Hatimaye mwaka 1926 na kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwepo kati ya Uingereza na mtawala huyo huyo wa Kiwahabi, Abdul-Aziz Ibn Saud alijitangaza kuwa kiongozi wa Hijaz. Mwaka 1927 Ibn Saud alijitangaza rasmi kuwa mtawala wa Hijaz na Najd na tarehe 8 Januari mwaka 1932  Abdul Aziz alitangazwa kuwa mfalme wa Saudi Arabia. Hadi kutwaa madaraka ya eneo lote la Hijaz, watu wa kizazi cha Aal Saudi walifanya mauaji mengi na umwagaji damu mkubwa na kuwalazimisha watu wa maeneo hayo kufuata fikra na itikadi potufu za kiwahabi.     

Na Tarehe 18 Dei mwaka 1385 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 19 iliyopita alifariki dunia mhakiki na mwanahistoria wa Iran, Hujjatul Islam Ali Dawwani. Msomi huyu alizaliwa mwaka 1308 Hijria Shamsia karibu na mji wa Kazerun ulioko kusini mwa Iran.

Alielekea Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kupata elimu za Kiislamu akiwa na umri wa miaka 14 na kurejea nchini miaka mitano baadaye. Ali Dawwani aliendelea kutafuta elimu katika mji mtakatifu wa Qum na kusoma kwa wanazuoni wakubwa kama Imam Ruhullah Khomeini na Ayatullah Borujerdi hadi alipopata daraja ya ijtihadi. Alibobea sana katika elimu ya historia na ameandika vitabu vingi katika uwanja huo.

Miongoni mwa vitabu vyake ni "Fakhari za Uislamu", "Mbora wa Wanawake Duniani" na "Harakati ya Wanazuoni wa Iran". 

Ali Dawwani