Mapinduzi ya Kiislamu; ustaarabu mpya wa Kiislamu (2)
(last modified Mon, 31 Jan 2022 10:42:21 GMT )
Jan 31, 2022 10:42 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu; ustaarabu mpya wa Kiislamu (2)

Taarifa ya 'Hatua (marhala) ya Pili ya Mapinduzi' ulikuwa ujumbe mpya ulioelekezwa kwa taifa la Iran na hasa kwa tabaka la vijana wa nchi hii, ambao ndio nguzo kuu ya "hatua ya pili ya kujijenga, kuzingatia jamii na ustaarabu." Moja ya mahitaji ya ustaarabu mpya wa Kiislamu ni kuwa na uelewa wa juu zaidi na kudumisha umoja na mshikamano.

Umoja na uadilifu wa umma unapatikana kupitia hatua za uongozi makini unaofahamu vyema hali na mazingira tofauti ya zama, unaoainisha njia sahihi katika matatizo na kuamsha ummah mbele ya hatari, madhara na maadui wanaoukabili. Kati ya mataifa yanayokandamizwa, ni wachache mno waliojitolea kufanya mapinduzi; na miongoni mwa mataifa ambayo yameinuka na kufanya mapinduzi, si jambo la kawaida kwao kuweza kukamilisha kazi hiyo na licha ya kubadilisha serikali lakini hushindwa kudumisha maadili ya kimapinduzi. Pamoja na hayo lakini mapinduzi matukufu ya taifa la Iran, ambayo ni mapinduzi ya kipekee na maarufu zaidi katika zama hizi, ndiyo mapinduzi pekee ambayo baada ya miaka arubaini na tatu, bado yanasimama kwa fahari juu ya msingi wa malengo na maadili yake ya mwanzoni na licha ya vishawishi vyote vinavyoonekana kuwa si rahisi kuvishinda, lakini yameendelea kulinda kwa ushujaa, heshima na nara zake za asili.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, kwa kuibuka kipekee, yalimaliza na kukomesha utaghuti wa kihistoria uliokuwa umedumu kwa muda mrefu. Iran, ambayo ilifedheheshwa na kurudishwa nyuma sana wakati wa utawala wa Pahlavi na Qajar, kwa mara nyingine ilianza kufuata mkondo wa maendeleo. Wananchi wa Iran wakiwa na irada ya kitaifa ambayo ndio msingi wa maendeleo ya pande zote na ya kweli, waliugeuza utawala mbovu wa Pahlavi na kuweka mahala pake serikali inayoungwa mkono na wananchi, na kisha wakawafanya vijana kuwa mhimili mkuu wa matukio na kuwaingiza katika uga wa usimamizi na uendeshaji nchi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei amesema kuhusu kubaki nyuma kwa Iran katika zama za utawala wa Pahlavi na maendeleo yaliyopatikana baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran kuwa: "Kabla ya Uislamu kutawala nchini, tulikuwa taifa ambalo lilikuwa limeachwa nyuma sana, tulikuwa tegemezi. Kisayansi tulikuwa nyuma, kisiasa tulikuwa nyuma, kijamii tulikuwa nyuma na pia tulikuwa tumetengwa kisiasa. Leo, maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu yamewalazimu maadui zetu kukiri kuhusu ukweli huo. Leo tuko katika safu ya kwanza kati ya nchi zilizoendelea kisayansi, kiteknolojia na elimu nyinginezo nyingi mpya katika ulimwengu wa sasa. Kwa kufanya juhudi na bidii, Umma wa Kiislamu, unaweza kubuni na kuweka misingi kwa ajili ya kufikia ustaarabu wa Kiislamu unaofaa katika zama hizi, na hivyo kuinufaisha jamii ya mwanadamu."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika maadhimisho ya miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi alitoa taarifa yenye anwani ya "Hatua ya Pili ya Mapinduzi" na kutoa mapendekezo ya kimsingi kwa shabaha ya "jihadi kubwa ya kujenga Iran adhimu ya Kiislamu." Bila shaka, taarifa ya "Hatua ya Pili ya Mapinduzi" ilikuwa ni kujadidisha mwongozo ulioelekezwa kwa taifa la Iran na hasa kwa tabaka la vijana, ambao hutumika kama msingi muhimu wa kutekeleza "hatua ya pili ya kujijenga, kuzingatia jamii na ustaarabu." Kwa hakika, hatua hii ya pili itaharakisha zaidi kufikiwa malengo makuu ya  Mapinduzi ya Kiislamu, ambayo ni "kuundwa ustaarabu mpya wa Kiislamu na kufanya maandalizi ya kuchomoza kwa jua la Wilaya Kuu, ambako ni kudhihiri kwa Imam wa Zama, Imam Mahdi (af)."

Akiarifisha sifa za ustaarabu mpya wa Kiislamu, Ayatullah Khamenei anasema: "Katika ustaarabu mpya wa Kiislamu, umaanawi na hali ya kiroho iko pembeni ya umaada na maadili na umaanawi uko pembeni ya maendeleo ya maisha ya kimaada." Katika muendelezo wa njia hii, ustaarabu mpya wa Kiislamu utapatikana kwa kutambulishwa malengo na thamani za Mapinduzi kwa watu wa nchi za Kiislamu. Katika njia hii, wanazuoni wa Kiislamu na Waislamu wote duniani wanapasa kuwa waenezaji wakuu wa misingi ya ustaarabu mpya wa Kiislamu na wachukue hatua za kivitendo kwa ajili ya kutimiza jukumu hilo.

Ayatullah Khamenei katika ufafanuzi wake kuhusu ustaarabu mpya wa Kiislamu, anauweka katika sehemu mbili za kutumika kama chombo (mbinu/mkakati) na halisi: Sehemu ya chombo (mbinu/mkakati) ya ustaarabu ni maadili yale yale tunayowasilisha leo kama maendeleo ya nchi. Sayansi, uvumbuzi, viwanda, siasa, uchumi, mamlaka ya kisiasa na kijeshi, uitibari ya kimataifa, tablighi na vyombo vya tablighi; yote hayo ni katika ustaarabu wa kimkakati (chombo). Licha ya mashinikizo, vitisho na vikwazo vya maadui, lakini taifa la Iran limeweza kupata mafanikio makubwa katika uwanja huo.

Kwa mtazamo wake, sehemu halisi ya ustaarabu huu mpya wa Kiislamu ni mtindo wa maisha na vitu vinavyounda maisha yetu, kama vile masuala ya familia, mtindo wa ndoa, aina ya makazi, aina ya mavazi, muundo wa matumizi, aina ya chakula, aina ya upishi, burudani, masuala ya biashara na kazi, jinsi ya kuamiliana kazini, tabia na mienendo kwenye vyuo vikuu, shuleni na katika vyombo vya habari, jambo ambalo liko mikononi mwa wanadamu wenyewe, jinsi ya kuamiliana na rafiki, adui na mgeni. Hizi ndizo sehemu kuu na halisi za ustaarabu zinazounda maisha ya mwanadamu na umma unaozingatia mafundisho ya Mwenyezi Mungu umesimama kwenye msingi wa thamani hizi.

Kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, kustawi katika masuala ya kimaada na kisayansi kunachukuliwa kuwa ustaarabu wakati jamii na watu wema wanapokuwa kwenye njia ya malengo yaliyoainishwa na Mwenyezi Mungu. Hivyo, Mtume (saw) anatanguliza Tauhidi kama msingi wa ujumbe wake. Kuujua utume ambao unakuja baada ya Tauhidi pia ni uleule utambuzi wa umoja na ustaarabu wa Kiislamu. Mtume (saw) alianzisha umoja na ustaarabu wa Kiislamu na kufanya mabadiliko mengi ya kijamii, kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi, na hivyo dini ya Kiislamu ikaweza kusimamisha ustaarabu mkubwa duniani katika kipindi kifupi kabisa. Kwa hivyo, umma wa Tauhidi na ustaarabu wa Kiislamu unapatikana kwa msingi wa utawala wa "Allah". Kwa kuthibitisha suala hilo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anaamini kuwa, jamii inayoegemeza kazi zake katika msingi wa Tauhidi hufanikiwa pakubwa katika juhudi zake za kujenga ustaarabu mkubwa, wa kina na ulioimarika katika pande zote.

Kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, katika ulimwengu kuna staarabu mbili mmoja unaoongozwa na Mwenyezi Mungu na mwingine unaoongozwa na mataghuti, kama inavyotwambia Aya ya 257 ya Surat al-Baqara: Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walio amini. Huwatoa gizani na kuwaingiza mwangazani. Lakini waliokufuru, walinzi wao ni mashet'ani. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa Motoni, na humo watadumu. Kwa hiyo, ukweli wa ustaarabu kwa mtazamo wa Kiislamu ni kujiepusha na giza na kuingia kwenye nuru, mwanadamu anapofikia nuru hupata mwanga na kuwa mstaarabu. Kwa mtazamo wa Qur'ani, ulimwengu una njia moja tu ya kupaa kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, na ambayo msingi wake ni umoja wa Umma wa Kiislamu na ustaarabu wa kisasa wa Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei (Mwenyezi Mungu amlinde) anasema hivi kuhusu majukumu ya umma kwa ajili ya kufanikisha ustaarabu mpya wa Kiislamu: "Kama ulivyofanya Uislamu na kama alivyofanya Mtume mwenyewe, Ulimwengu wa Kiislamu leo ​​una jukumu zito la kuleta maisha mapya katika ulimwengu huu, kuunda anga mpya na kufungua njia mpya. Tunaliita jambo hili ambalo tunalisubiri kuwa "ustaarabu mpya wa Kiislamu."

Ni lazima tutafute ustaarabu mpya wa Kiislamu kwa ajili ya ubinadamu. Hili kimsingi linatofautiana na kile ambacho madola ya kibeberu ya Magharibi hufikiri na kukifanya kuhusu jamii ya mwanadamu. Hii haina maana ya kuteka na kukalia kwa mabavu nchi za mataifa mengine, kukiuka haki zao wala kutwisha mataifa mengine maadili na utamaduni watu, bali ni kuwasilisha kwao zawadi tuliyopewa na Mwenyezi Mungu ili yaweze kuchagua njia sahihi kwa hiari na chaguo lao wenyewe. Njia ambayo madola makuu ya dunia leo yameyatwisha mataifa ni njia mbaya na ya upotovu. "Ni jukumu letu leo kurekebisha hali hiyo."

Hii leo, kutokana na kuimarika na kuendelea Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ulimwengu wa Kiislamu una fursa kubwa ya kuunda ustaarabu wa Kiislamu unaofaa. Uislamu Safi unaotoka katika kitovu cha Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kabla ya kuzingatia hitilafu za Waislamu huzingatia mambo ya pamoja yanayowakutanisha. Ndio maana Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi akasema: "Umoja si harakati ya kisiasa na kimbinu, bali ni imani ya dhati juu ya hitajio la umoja wa Umma wa Kiislamu. Hatua ya kwanza katika kuunganisha Ulimwengu wa Kiislamu ni kujizuia jamii za Kiislamu, serikali, makabila na madhehebu ya Kiislamu kushambuliana na kuamua kuungana dhidi ya adui wao wa pamoja. Katika hatua inayofuata, nchi za Kiislamu zinapasa kushirikiana katika masuala ya sayansi, mali, utajiri, usalama na nguvu za kisiasa na kuimarisha juhudi za kubuni ustaarabu mpya wa Kiislamu."

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanaadhimisha mwaka wa arubaini na tatu wa ushindi wake, ambao licha ya maadui wake wenye nia mbaya kuwa na dhana potofu tangu mwanzo na kupanga njama ya kuyaangamiza, lakini marafiki wake duniani ndio waliofanikiwa na kupata ushindi wa mwisho kwa kuyaletea maendeleo makubwa na ya kushangaza baada ya kushinda changamoto na kuvunja njama hizo za maadui. Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa taifa hili na kizazi ambacho kilianzisha  mapinduzi haya na kushikamana na maadili yake hadi mwisho, na huku tukiwa na matumaini ya kudhihiri mwokozi wa ulimwengu, Hadhrat Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) na kuundwa kwa ustaarabu mpya wa Kiislamu unaozingatia Uislamu safi wa Bwana Mtume Muhammad (saw), tunakuageni nyote wasikilizaji wapenzi kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags