Feb 12, 2023 07:26 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu: Ilhamu ya kuhuisha Ustaarabu wa kisasa wa Kiislamu

Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mnaponitegea sikio wakati huu. Nakukaribisheni kwa moyo mkunjufu kusikiliza mfululizo mwingine wa vipindi hivi maalumu tulivyokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Alfajiri Kumi za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambapo maudhui yetu ya leo ni kuhuishwa Ustaarabu wa kisasa wa Kiirani na Kiislamu. Endeleeni kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Mwaka wa 44 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu umeadhimishwa kwa sherehe zilizohudhuriwa na mamilioni ya Wairani walioshiriki kwenye hafla mbalimbali na katika maandamano makubwa yaliyofanyika Februari 11 katika barabara za miji mbalimbali ya Iran ya Kiislamu. Ushindi adhimu wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoongozwa na Imam Khomeini (MA) na kuasisiwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, vilileta mageuzi makubwa na mapana duniani mwishoni mwa milenia ya pili katika uga wa kimataifa; kiasi kwamba kwa kurejea tena kwenye chimbuko la urithi wenye thamani kubwa wa Uislamu, hivi sasa tunashuhudia kuzaliwa kwa uono na mtazamo mpya kuhusiana na ulimwengu, mwanadamu na mahusiano mbalimbali baina ya watu katika nyuga za kisiasa, kijamii na kiutamaduni katika zama hizi.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni mapinduzi yanayotafautiana sana na mapinduzi mengine yaliyotokea duniani kwa upande wa misingi na idiolojia. Tukiyatupia jicho mapinduzi makubwa yaliyotokea duniani tutafikia hitimisho kwamba sababu zilizopelekea kutokea mapinduzi hayo hazioani kabisa na zile zilizochangia kujiri Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Na ndio maana wanafikra na wasomi wengi wamekiri kwamba, walistaajabishwa na mapinduzi hayo na kuyatambua kama mapinduzi yaliyo nje ya nadharia zinazohusiana na mapinduzi.

Mastaajabu hayo yametokana na mtazamo juu ya matukio ya ulimwengu uliojengeka kwenye bongo na wanafikra duniani. Fikra zilizojengeka juu ya mtazamo wa kimaada kuhusu ulimwengu, hutafuta sababu za kimaada na za vitu vya kimaumbile kwa ajili ya kuhakiki mambo, ilhali sababu ya kutokea mapinduzi ya Iran haiwezi kuhakikiwa isipokuwa kwa jicho na mtazamo wa kidini. Kama walivyokiri wengi, mapinduzi ya Iran ni mapinduzi ya kipekee yasiyo na mfano wake miongoni mwa mapinduzi makubwa yaliyojiri duniani.

Ukweli ni kwamba nchini Iran yalitokea mapinduzi yaliyotibua hali zote za mlingano zilizokuwepo, na kuzipa changamoto ya kutiliwa shaka nadharia za Sayansi ya Jamii au Sosiolojia. Hakukuwa na mtu ambaye aliamini kama yangeweza kutokea mapinduzi yasiyo na msukumo wowote wa kichama au harakati maalumu inayojulikana, zaidi ya kutegemea dini na nguzo zake kuu ambazo ni misikiti. Dini ya Uislamu, ambayo katika umri wake wote, hadi sasa imeonyesha kuwa na ustaarabu mkwasi na wa kujitosheleza, imeshuhudia kufifia ustaarabu wake huo katika vipindi kadhaa vya historia. Kwa sababu hiyo, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulichukuliwa kama nukta muhimu sana ya kuurejesha tena utambulisho wa Kiislamu na kuhuishwa na kupatikana tena utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu wa Kiirani. 

Ustaarabu wa kisasa wa Kiislamu ni aina ya uono juu ya mustakabali, ukiwa na maana ya kuainisha upeo unaokusudiwa kufikiwa na taifa adhimu la Iran. Katika zama zote za historia, taifa la Iran limechangia na kujenga ustaarabu; na hivi sasa linaweza pia kurejea kwenye nafasi yake hiyo ya kujenga ustaarabu duniani. Pamoja na hayo, maana ya ustaarabu wa Kiirani na Kiislamu imefungamana na sifa maalumu kwa upande wa elimu na maarifa juu ya ulimwengu, elimu juu ya mwanadamu, na elimu kuhusu utambuzi wa mambo, siasa na dini, zinaoifanya iwe na uimara wa kiutamaduni, ambao ni nadra kupata mfano wake duniani.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hasa baada ya kuporomoka Shirikisho la Kisovieti la Urusi, liliibuka wimbi jipya la mijadala kuhusu ustaarabu na ujenzi wa ustaarabu mpya. Mwanafikra wa Kimarekani Francis Fukuyama alizungumzia dhana aliyoiita Mwisho wa Historia kwa kimombo End of History, na ushindi wa Demokrasia ya Kiliberali, japokuwa miaka kadhaa baadaye alikuja kuifuta mwenyewe dhana na nadharia yake hiyo. Samuel Hantington, ni mwanafikra mwingine wa Kimarekani ambaye mnamo mwaka 1993 aliandika kitabu kiitwacho "Mpambano wa Staarabu" yaani The Clash of Civilizations.

Asili ya nadharia ya Hantington ni kwamba, kwa kumalizika Vita Baridi, enzi za mzozo wa idiolojia pia zinafikia tamati na kuanza zama mpya. Kwa mtazamo wa mwanafikra huyo wa Marekani, nukta kuu ya mzozano baina ya Staarabu itahusisha ustaarabu wa Magharibi katika upande mmoja na staarabu mbili za Ukonfyushasi, yaani Confucius na Uislamu katika upande mwingine. Lengo la nadharia hii ni kujaribu kutoa picha na taswira ya kushtusha ya mahusiano ya kihasama baina ya staarabu kwa kutangaza uwepo wa washindani na maadui katika siku za usoni. Lakini pia ilikuwa na dhamira ya kubainisha michakato tarajiwa ya makabiliano na uhasama, ili kwa njia hiyo kuwashajiisha na kuwahimiza wapangaji wa sera za kisiasa wa Magharibi wachukue hatua zinazohitajika na tahadhari za lazima, sambamba na kuimarisha umoja na mshikamano wa ndani ya ustaarabu wao.

Lakini mkabala na nadharia iliyopigiwa upatu na Hantington ya Mpambano wa Staarabu, Mohammad Khatami, rais wa wakati huo wa Iran alipendekeza na kuzungumzia nadharia ya Mazungumzo Baina ya Staarabu mbalimbali, kwa kimombo Dialogue Among Civilizations wakati alipoelekea New York na kuhutubia mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, rai ambayo ilipokelewa na kuungwa mkono na jamii ya kimataifa.

Katika karne za mwanzoni mwa baada ya kudhihiri Uislamu, Ustaarabu wa Kiislamu ulijengwa juu ya misingi ya kiutamaduni na kielimu; na hivi sasa pia, ustaarabu unaokusudiwa kujengwa na Uislamu unasimama juu ya misingi ya kiutamaduni na kielimu, amani na urafiki baina ya mataifa. Kwa muda wa karne saba, kuanzia mwisho wa enzi za ukomboaji ardhi uliofanywa na Waislamu mpaka walipodhihiri Wamongolia, -kwa mtazamo wa urari na nidhamu za kiakhlaqi, hali ya juu ya kimaisha, uwepo wa uvumlivu na moyo wa kustahamiliana, kujiepusha kwa kiwango fulani na hisia za taasubi na ukereketwa na kustawisha elimu na maadili-, Ustaarabu wa Kiislamu uliongoza ulimwengu mzima wa ustarabu na ukawa ndio mlezi na mwongozaji wa utamaduni wa ulimwengu wa utu.

Hakuna chembe ya shaka kuwa hizo zilikuwa zama za kung'ara kwa ustaarabu wa mwanadamu. Na kama mchango ambao Ustaarabu wa Kiislamu umetoa kwa utamaduni na ustaarabu wa dunia ya leo si mkubwa kuliko uliotoa ustaarabu wa Kigiriki, basi si mdogo kupita huo, isipokuwa kwa tofauti pia kwamba, taathira ya kimaanawi ya utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu ingali inaendelea kushuhudiwa katika dunia ya leo. Mchanganyiko mkubwa mno wa rangi, wa asili na wa kiutamaduni uliokuwepo katika Ulimwengu wa Kiislamu hata katika zama za mjumuiko wa kaumu na tamaduni za kila aina, ulionekana kitu kigeni na kisicho cha kawaida kwa kadiri kwamba, kila mwanahistoria anabaki akijiuliza, mahusiano ya kidini yana uimara wa kiasi gani mpaka yanaweza kuziunganisha hali hizo kinzani na kuzifanya kuwa kitu kimoja! 

Kwa mtazamo wa kihistoria, tunaweza kuigawa historia ndefu ya Ustaarabu wa Kiislamu katika vipindi vitatu. Kipindi cha kwanza ni kuanzia ulipodhihiri Uislamu katika karne ya saba miladia na kuendelea mpaka iliponyakuliwa Baghdad na kuingia mikononi mwa Wahulagu wa Kimongolia. Kipindi cha pili nia cha kusilimu na kuupokea Uislamu Wamongolia  na kuasisiwa tawala kadhaa kama ya Safawiya na Othmaniya na kuishia katikati ya karne ya 18 miladia; na hatimaye kipindi cha tatu ni kupata nguvu madola ya Ulaya na kuzitawala moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja ardhi za Waislamu katika zama za Ukoloni, na kuendelea hadi zama za sasa. Kwa mtazamo wa wanahistoria, Ustaarabu wa Kiislamu ulifikia kilele cha adhama yake katika kipindi cha kwanza, yaani katika zama Uislamu ulipotawala kwa karne kadhaa katika ardhi nyingi za zama hizo zilizokuwa na ustawi na kuweka chini ya mamlaka yake sehemu kubwa ya maeneo ya Asia, Afrika na sehemu fulani za Ulaya. Maeneo yote hayo yaliunganishwa na dini na utamaduni mmoja na wakazi wake wakajihisi kuwa sehemu ya ustaarabu mmoja, mpana na mkwasi wa zama hizo.

Sambamba na hayo, kitu kilichoupambanua Ustaarabu wa Uislamu na staarabu zingine katika zama hizo ni kwamba, Ustaarabu wa Kiislamu ulijenga moyo wa uchukulivu na kustahamiliana badala ya ukereketwa na taasubi za ulimwengu wa enzi za kale; na kwa upande wa muhtawa na mafunzo yake, ulileta sura mbadala ya muundomchanganyiko wa urithi wa staarabu zilizopita. Abdulhussein Zarin Kub, ni mwanahistoria mashuhuri wa Kiirani ambaye katika kitabu chake cha Rekodi ya Uislamu, ameandika yafuatayo kuhusu Ustaarabu wa Kiislamu wa karne za mwanzoni mwa baada ya kudhihiri Uislamu:

"Ustaarabu wa Uislamu, ambao kwa namna ulivyo ulikuwa mrithi wa utamaduni mkongwe wa Mashariki na Magharibi, haukuwa muigaji wa kila ulichokuta katika tamaduni zilizopita, wala  mwendelezaji wao kwa kila jambo: ulikuwa ni mchanganyaji na mkamilishaji. Enzi za ukamilikaji wake, zilizofikia tamati kwa kutawala Wamongolia, zilikuwa za kipindi cha ujengaji - ujengaji wa utamaduni wa ulimwengu mzima na wa kiutu - na katika eneo la ustaarabu huo uliokuwa imara na madhubuti, michango ya jamii zote, kuanzia ya Kiebrania, Kigiriki, Kihindi, Kiirani, Kituruki mpaka ya Kichina...ilifinyangwa pamoja na kuzalisha mseto wa kile kinachojulikana kama ustaarabu na utamaduni wa Kiislamu. Kwa hakika Uislamu ulikuwa na sura ya utu na ya kidini - si ya Mashariki wala Magharibi; ilikuwa jamii ya Kiislamu, mrithi wa ustaarabu huo adhimu; ilikuwa jamii yenye urari, mhimili wake mkuu ukiwa ni Qur'ani, si Sham wala Iraq".

Lakini kipindi cha tatu cha Ustaarabu wa Kiislamu ni kipindi cha mdororo na uzorotaji, kilichoandamana na kutawaliwa jamii za Kiislamu na ulimwengu wa Magharibi. Pamoja na hayo, katika hali isiyotarajiwa, Mapinduzi ya Kiislamu yalitokea nchini Iran na kuweka tena jiwe la msingi la kipindi kipya cha historia ya ustaarabu wa Kiislamu. Kwa hakika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyojiri mwaka 1979 yalifufua na kuhuisha tarajio tukufu la ustaarabu mpya na wa kisasa wa Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelizungumzia hili kama ifuatavyo: "taifa hili lina uwezo katika hali na pande zote hizi; kwa hiyo kama litafanya bidii na hima na likaamua, litaweza kufika. Iran hii, haiwezi kubaki kuwa Iran ya enzi za Qajar na Pahlavi. Iran hii, ni Iran ya zama za Uislamu; inapasa tuwe na uwezo wa kufikia kilele cha ustaarabu wa mwanadamu".

Katika kulizungumzia suala hili, Ayatullah Khamenei amekumbusha pia kwamba, kufanikisha fikra na lengo hilo ni jambo gumu, kwa sababu manufaa na maslahi ya baadhi ya watu katika dunia ya leo yanapatikana kwa kutilia mkazo upande wa vitu na wa kimaada wa ustaarabu. Kwa sababu hiyo, amesisitiza pia kwa kusema: "mwanadamu anahitaji maendeleo ya kisayansi na anahitaji uvumbuzi kimtawalia; kama ambavyo leo hii mwanadamu anashughulika na uvumbuzi na ugunduzi huo na kupata maendeleo ya kustaajabisha. Lakini pamoja na hayo, Mfumo wa Kiislamu kwa upande wake, ni mfumo ambao unataka kurejesha umaanawi kwenye mazingira ya maisha ya mwanadamu, kitu kilichopotea katika ustaarabu na maisha ya watu. Kulieleza hili kwa maneno ni kazi nyepesi; lakini kulitekeleza ni kazi ngumu na yenye wapinzani wababe na wenye nguvu kubwa sana. Watu wote ambao manufaa na maslahi yao duniani yanaendana na kuanzisha vita, wanapinga na hawakubaliani na hili; watu wote ambao kueneza ngono ndio kazi na shughuli wanayofanya duniani kwa ajili ya kupatia fedha, hawakubaliani na hili; watu wote wanaotaka kuutia mkononi na kuuhodhi utajiri muhimu wa mataifa, hawakubaliani na hili; watu wote ambao, kuwa na nguvu na sauti kuu ndilo lengo kuu kwao - katika tawala ndogo na kubwa duniani - hawakubaliani na hili; maana yake ni kwamba, suala hili lina wapinzani wababe wenye nguvu kubwa".

Wapenzi wasikilizaji, mfululizo huu wa vipindi maalumu tulivyokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Alfajiri Kumi za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran umefikia tamati. Tunakushukuruni kwa usikivu wenu na tunakutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu.../

Tags