Ubinadamu Kwanza (Siku ya Kimataifa ya Ubinadamu)
https://parstoday.ir/sw/radio/world-i13999-ubinadamu_kwanza_(siku_ya_kimataifa_ya_ubinadamu)
Siku ya Kimataifa ya Ubinadamu ni siku ambayo walimwengu hukusanyika katika maeneo mbalimbali kuadhimisha na kuwapongeza watu wote waliosabilia nafsi zao kuokoa wanadamu wenzao na kufanya jitihada za kuifanya dunia hii kuwa mahala pa amani na usalama zaidi.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Aug 26, 2016 03:20 UTC
  • Ubinadamu Kwanza    (Siku ya Kimataifa ya Ubinadamu)

Siku ya Kimataifa ya Ubinadamu ni siku ambayo walimwengu hukusanyika katika maeneo mbalimbali kuadhimisha na kuwapongeza watu wote waliosabilia nafsi zao kuokoa wanadamu wenzao na kufanya jitihada za kuifanya dunia hii kuwa mahala pa amani na usalama zaidi.

Siku ya Kimataifa ya Ubinadamu

Kila siku inayokwenda kwa Mungu, wako baadhi ya wanadamu wanaojitolewa na kwenda kwa ushujaa  mkubwa katika mistari ya mbele ya vita, maeneo ya majanga na maafa ya kibinadamu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wanadamu wenzao na kutoa huduma mbalimbali katika mazingira magumu na hatari sana.

Kwa kutilia maanani suala hilo tarehe 19 Agosti kila mwaka imetangazwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Ubinadamu kwa shabaha ya kuwaenzi na kutoa heshima kwa waokoaji na watu wanaotoa misaada ya kibinadamu ambao wanahatarisha maisha yao kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanadamu wengine. Siku hii ilitangazwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kukumbuka na kuenzi watu waliouawa katika shambulizi la bomu lililolenga ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Baghdad hapo mwaka 2003. Waokoaji 22 wa Umoja wa Mataifa waliuawa katika shambulizi hilo.

Siku ya Kimataifa ya Ubinadamu ni fursa kwa Umoja wa Mataifa na washirika wake kutoa wito wa kuwepo mshikamano wa kimataifa na watu zaidi ya milioni 130 kote duniani wanaohitajia misaada ya kibinadamu kwa ajili ya kubakia hai. 

Siku ya Kimataifa ya Ubinadamu

Mwaka huu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ubinadamu yalijikita zaidi katika maudhui ya: "Ubinadamu Kwanza" katika mkutano uliofanyika Istanbul, Uturuki ili kujadili njia na mipango ya kuwasaidia wanadamu milioni 130 wanaohitajia misaada.

Kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, mwaka huu pia kumefanyika sherehe za aina mbalimbali za kuwaenzi waokoaji, wafanyakazi wa jumuiya za kutoa misaada ya kibinadamu na wanaharakati katika masuala hayo kote duniani.

Miongoni mwa shughuli za kuadhimisha siku hii ni maonyesho ya picha yaliyofanyika katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York kwa anwani ya "Wakati Nilipokuwa Mkubwa" (When I Grow Up). Kwenye maonyesho hayo kuna picha zinazoakisi matarajio ya watoto na vijana walioathiriwa na migogoro ya aina mbalimbali katika nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jordan, Mali na Niger. 

Mjini New York pia tarehe 19 Agosti kulifanyika sherehe kubwa ya kuwaenzi watu waliosabilia maisha yao kwa ajili ya kuwaokoa wanadamu wenzao na kumeonyeshwa filamu kadhaa za matukio ya kweli ikiwemo ile iliyopewa jina la "Home" au Nyumbani kwa Kiswahili ambayo inaakisi safari ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jordan, Lebanon na Sudan Kusini. Filamu hiyo inazungumzia majukumu ya kibinadamu. Watoaji misaada ya kibinadamu kutoka maeneo mbalimbali duniani pia walisimulia tajiriba na uzoefu wao katika kazi ngumu ya kutoa misaada ya kibinadamu kwenye maeneo hatari na yenye migogoro, simulizi za wakimbizi wa Syria na jinsi wanavyopanda mawimbi ya bahari katika safari ngumu ya kuokoa maisha yao na visa vingine vingi vinavyoakisi mashaka ya wanadamu katika maeneo yenye migogoro duniani. 

Mkimbizi mtoto akiokolewa baada ya kuzama baharini

Siku ya Kimataifa ya Ubinadamu mwaka huu imefanyika baada ya moja ya matukio muhimu sana katika historia ya hatua zilizochukuliwa kwa ajili ya kuwasaidia binadamu wanaopatwa na mashaka, yaani mkutano wa kimataifa uliofanyika Istanbul tarehe 24 Mei. Katika mkutano huo viongozi wa nchi mbalimbali duniani walitangaza uungaji mkono wao kwa mpango mpya wa harakati za  kibinadamu na kuahidi kuchukua hatua kubwa zaidi kwa ajili ya kupunguza mashaka ya wanadamu wanaoishi maeneo yenye migogoro na kutoa huduma bora zaidi kwa mamilioni ya watu wanaohitajia misaada ya dharura.

Siku ya Kimataifa ya Ubinadamu ni siku ambayo wadau hukusanyika pamoja na kujadili njia za jinsi ya kutengeneza dunia yenye amani na ubinadamu zaidi na kufanya jitihada za kuwaenzi watu wanaosabilia roho zao kwa ajili ya kuokoa wanadamu wenzao wanaoishi katika maeneo yenye vita, migogoro na majanga ya aina mbalimbali.

Rekodi ya watu milioni 130 wanaohitaji misaada ya kibinadamu kwa ajili ya kubakia hai inaonesha kuwa, moja ya sita ya idadi ya watu duniani wanaishi katika mazingira na hali ya migogoro. Katika ujumbe wake wa mwaka huu kwa mnasaba wa siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema kuwa: "Kwa hakika kiwango hiki cha wanadamu wanaoishi katika migogoro ni kikubwa sana lakini tunapasa kuelewa kuwa, kinaakisi sehemu moja ya kisa cha mashaka ya wanadamu hao. Nyuma na takwimu hizo kuna watu, familia na jamii za wanadamu walioharibikiwa na maisha ambao hawana tofauti yoyote na mimi na wewe; kuna watoto wadogo, wanawake na wanaume ambao kila siku wanakabiliana na machaguo muhali. Kuna akina baba na akina mama ambao wanalazimika kuchagua moja kati ya machaguo mawili, ama kununua chakula kwa ajili ya watoto wao au kununua dawa. Kuna watoto ambao wanalazimika kuchagua ama kwenda shule au kufanya kazi kwa ajili ya kuzisaidia familia zao. Kuna familia zinazolazimika kukhitari moja kati ya mambo mawili, ama kumiminiwa mabomu ndani ya nyumba na makazi yao au kukimbia nyumba na nchi zao kupitia njia hatari za baharini…  

Ban Ki-moon

Nawaomba wanadamu wote washiriki katika kampeni ya Umoja wa Mataifa iliyoanzishwa kwa kaulimbiu ya "Ulimwengu upi ungefadhilisha wewe kuishi ndani yake? (What world would you rather live in?)," mwisho wa kunukuu.

Miongoni mwa malengo ya kampeni hiyo ni kuzidisha kiwango cha uelewa wa watu kuhusu mashaka yanayowapata wanadamu wanaoishi katika maeneo yenye migororo duniani na kuwahamasisha wanadamu kuwa na mshikamano zaidi na watu walioathiriwa na maafa ya aina mbalimbali. Vilevile kampeni hiyo inalenga kukusanya fedha kwa ajili ya mfuko wa radiamali na hatua za haraka wa Umoja wa Mataifa.

Kama tulivyoashiria hapo awali, mapema mwaka huu watu 9000 wakitanguliwa na viongozi wa nchi mbalimbali, walishiriki katika mkutano wa kwanza wa ubinadamu uliofanyika mjini Istanbul huko Uturuki. Katika mkutano huo viongozi wa nchi mbalimbali duniani waliahidi kuwapa tunu ya matumaini ya uhai wanadamu wanaoishi katika maeneo yenye vita, maafa na migogoro mikubwa. Vilevile walipasisha hati ya misaada ya kibinadamu inayosisitiza zaidi juu ya masuala ya haki za binadamu, kupiga vita umaskini, kuhubiri amani na usalama wa kimataifa na kutoa fursa sawa kwa wanadamu wote.

Kwa msingi huo wanadamu wote tunapaswa kuwa na mchango katika kufanikisha malengo hayo na kuungana kwa jina la ubinadamu ili kuifanya dunia yetu kuwa mahala salama na amani kwa wanadamu wote.