Israel yatambua mamlaka ya Morocco kwa eneo linalozozaniwa la Sahara Magharibi
Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umesema unatambua mamlaka ya Morocco katika eneo linalozozaniwa la Sahara Magharibi. Hayo ni kwa mujibu wa serikali ya Morocco kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu wa Israel.
Ofisi ya Mfalme wa Morocco imeashiria barua kutoka kwa waziri mkuu wa Israel na kutangaza katika taarifa kwamba Benjamin Netanyahu amemfahamisha Mfalme Mohammed VI kuhusu "uamuzi wa kutambua mamlaka ya Morocco" juu ya Sahara Magharibi.
Katika barua yake hiyo, Netanyahu amesema, Israel itasajili uamuzi wake huo katika Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa, na katika mataifa yote ambayo Israel ina uhusiano nayo wa kidiplomasia.
Aidha, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni ameendelea kueleza kuwa, utawala huo unafikiria kufungua ubalozi mdogo katika mji wa Dakhla, ulioko katika upande wa Morocco wa Sahara Magharibi.
Maafisa wa utawala wa Kizayuni walitangaza mwezi Juni kwamba, walikuwa wakijadili suala la mamlaka ya Morocco juu ya Sahara Magharibi, lakini baadaye mwezi Julai wakashurutisha kupitisha uamuzi huo na Rabat kuandaa mkutano ambao umeshaakhirishwa mara kadhaa kati ya maafisa wa Israel na mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa manne ya Kiarabu yaliyoridhia kuanzisha uhusiano na Israel kwa upatanishi wa Marekani, ambayo ni Muungano wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Sudan na Morocco.
Hata hivyo mwezi uliopita, Morocco iliahirisha kongamano liitwalo Jukwaa la Negev, ikitaja sababu kuwa ni ukandamizaji na vitendo vya ukatili vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.
Lengo la kongamano hilo ni kuimarisha ushirikiano kati ya Bahrain, Misri, Israel, Morocco, Muungano wa Falme za Kiarabu, na Marekani.
Morocco ililitwaa eneo kubwa la Sahara Magharibi, koloni la zamani la Uhispania mwaka 1975 na tangu wakati huo imekuwa katika mzozo na mapigano na Harakati ya Polisario, inayoungwa mkono na Algeria, ambayo inapigania kuasisi nchi huru katika eneo hilo na kukomesha uwepo wa serikali ya Rabat.../