Algeria yaijia juu Israel kwa kutambua mamlaka ya Morocco Sahara Magharibi
Algeria imekosoa vikali uamuzi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wa kutambua mamlaka ya Morocco katika eneo linalozozaniwa la Sahara Magharibi.
Taarifa iliyotolewa jana Alkhamisi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imesema hatua hiyo ya Israel ya kutambua mamlaka ya Morocco kwa eneo linalozozaniwa la Sahara Magharibi inakanyaga wazi sheria za kimataifa.
Morocco ililitwaa eneo kubwa la Sahara Magharibi, koloni la zamani la Uhispania mwaka 1975 na tangu wakati huo imekuwa katika mzozo na mapigano na Harakati ya Polisario, inayoungwa mkono na Algeria, ambayo inapigania kuasisi nchi huru katika eneo hilo na kukomesha uwepo wa serikali ya Rabat.
Hata hivyo siku chache zilizopita, ofisi ya Mfalme wa Morocco iliashiria barua kutoka kwa waziri mkuu wa Israel na kutangaza katika taarifa kwamba Benjamin Netanyahu amemfahamisha Mfalme Mohammed VI kuhusu "uamuzi wa kutambua mamlaka ya Morocco" juu ya Sahara Magharibi.

Katika barua yake hiyo, Netanyahu amesema, Israel itasajili uamuzi wake huo katika Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa, na katika mataifa yote ambayo Israel ina uhusiano nayo wa kidiplomasia.
Aidha, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni ameendelea kueleza kuwa, utawala huo unafikiria kufungua ubalozi mdogo katika mji wa Dakhla, ulioko katika upande wa Morocco wa Sahara Magharibi.
Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, kadhia ya Sahara Magharibi haijapatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu sasa kutokana na unafiki na undumakuwili wa nchi za Magharibi.